CHADEMA yawavaa Kikwete, Bosi wa Usalama na IGP

Jamii Africa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetuma ujumbe mzito kwa Rais Jakaya Kikwete, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, juu ya kauli za Naibu Katibu Mkuu wa CCM (bara) Mwigulu Nchemba kukihusisha chama hicho cha upinzani na njama za mauaji, kuwa tafsiri ya maneno ya kiongozi huyo yanatangaza uasi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia FikraPevu, zinasema kuwa hatua hiyo ya jana ya CHADEMA kuamua kutoa kile walichodai ni 'elimu' kwa Rais Kikwete, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na IGP Mwema, ni moja ya hatua zinazoandaliwa kuchukuliwa dhidi ya Mwigulu, hasa baada ya chama hicho kupata kile kinachodaiwa kuwa ni mpango 'mzima' ulioko nyuma ya kauli za Mwigulu.

Jana, CHADEMA kupitia kwa Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila, mbele ya waandishi wa habari, kilisema "CHADEMA kiko tayari kushika dola, kuwatumikia wananchi. Tunajua mipango yao katika hayo maneno ya Mwigulu. Tunaelewa wanachotaka kufanya. Tuko imara."

Kauli hiyo ya Benson, ilifuatia baada ya kusema kuwa chama hicho kimeamua kutoa tafsiri kiliyoita kuwa ni sahihi kimantiki juu ya kauli za Mwigulu, kutokana na viongozi hao waandamizi wa masuala ya ulinzi na usalama, kuendelea kukaa kimya, hivyo kukubaliana na maneno yanayoenezwa kuwa CHADEMA kinafanya mipango ya mauaji.

"Tunataka kuwaambia wahusika wa usalama na ulinzi nchini, hususan Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid, nini maana ya tafsiri ya habari za kutunga, za Mwigulu Nchemba.

"Kwamba suala la yeye kusema CHADEMA inapanga mauaji, tunataka kumwambia Rais, IGP Said Mwema na Othman Rashid kuwa, kwa sababu wamekuwa kimya na kukubaliana na uzushi wa hatari wa Mwigulu, tafsiri yake ni kwamba Jeshi la Polisi limeasi na sasa linafanya kazi kwa maelekezo ya CHADEMA. Linatekeleza amri za CHADEMA!

"Tunasema hivyo kwa sababu, Watanzania na dunia inajua kuwa mauaji yenye utata yanayohusishwa na siasa, yamefanywa na Jeshi la Polisi. Ushahidi upo. Polisi wameua watu Arusha, polisi wameua watu Songea, polisi wameua mtu Morogoro, polisi wameua mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, polisi wameshiriki kuua, dunia nzima inajua.

"Orodha ya mauaji ya vitendo vya mauaji vinavyofanywa na Jeshi la Polisi nchini ni ndefu, kwa malengo ya kisiasa ya CCM. Lakini kama Mwigulu anasema hiyo ni mipango ya CHADEMA, maana yake ni kwamba kwa sababu jeshi ndilo linaua na ushahidi upo, basi Jeshi la Polisi linatekeleza mipango ya chama CHADEMAtafsiri yake ni kwamba Mwigulu anamaanisha jeshi limeshaasi," alisema Kigaila na kuongeza;

"Sasa mtu anayetangaza ‘uasi’ wa jeshi kwa kiwango cha kutekeleza mipango ya chama cha siasa badala ya kumsikiliza Amri Jeshi Mkuu, serikali inamnyamazia na kumchekea. Tumeitaka serikali kufanya uchunguzi huru kwenye matukio ya mauaji yanayohusishwa na siasa, ikiwemo tukio la kifo cha kada na kiongozi wa CCM huko Ndago, Singida, lakini wamekaa kimya. Badala yake unatungwa uongo ambao Mwigulu anaendelea kuueneza

"Tafsiri nyingine ya maneno hayo ya kutungwa anayoeneza Mwigulu ni kwamba vyombo vinavyohusika katika ulinzi na usalama, vimeshindwa kazi. Ni maneno ya aibu kwa Rais Kikwete, IGP Mwema na Othman Rashid.

"Kwamba wao wameshindwa kazi zao na sasa wamemkabidhi Mwigulu, ambaye ndiye anaweza kuingia kwenye vikao vya CHADEMA, akarekodi, kisha badala ya kuwapelekea hao wenzake, ili serikali ya chama chake ichukue hatua, anazunguka nao kulia kwenye vyombo vya habari! Na wahusika wamekaa, wanamsikiliza na kumchekea," alisema Kigaila.

Kuhusu kauli za Nape

Jana kulikuwa na maoni ya baadhi ya wanachama wa JamiiForums, baada ya kuwepo kwa taarifa za kuwa CHADEMA watakutana na waandishi wa habari jana makao makuu ya chama hicho, kuwa bila shaka kingezungumzia pia kauli za hivi karibuni za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuwa chama hicho kinakufa kwa kukumbatia ubaguzi, hivyo kukumbana na laana ya Mwalimu Nyerere juu ya dhambi hiyo.

Akijibu hoja hizo, Benson alisema kuwa chama hicho kitajibu upuuzi na hoja kwa uzito tofauti tofauti, lakini hakitakubali propaganda za CCM ziwapoteze mwelekeo wa katika kufanya kazi na kutimiza wajibu wa kila siku, katika kuwatumikia Watanzania.

"Kwanza, CCM kupitia kwa viongozi wao waandamizi, akiwemo Nape na Mwigulu,wanazunguka zunguka huko, kuwaambia Watanzania kuwa CHADEMA inakufa, tena wanatengeneza hata sababu za kifo, wanasema ni ubaguzi na kutokana na laana ya Mwalimu Nyerere.

"Tunataka kuwaambia hivi: Kwamba CHADEMA haina ubaguzi na hivyo haiwezi kufa leo wala kesho, mpaka iwe imetimiza kazi yake ya kuwakomboa Watanzania. Na bahati mbaya, CCM wanaona CHADEMA kitakufa, wanasahau kuona kuwa chama chao tayari kinakufa. Kama suala ni laana ya Nyerere. Laana hiyo haiko CHADEMA; iko ndani ya CCM kwa sababu mbalimbali, leo hapa tutataja chache," alisema Kigaila.

Alizitaja baadhi ya sababu hizo zinazoiua CCM, kuwa ni pamoja na laana ya mwasisi wake, Mwalimu Nyerere, ambaye aliwahi kukisema hadharani chama hicho, ikiwemo kukitungia kitabu kuwa kinanuka rushwa na kina kansa ya uongozi. Kigaila aliongeza kuwa sababu zingine ni dhambi ya ubaguzi waliyonayo CCM, akitolea mifano namna wana CCM wa kundi la mtandao, walivyomwita Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa ni mwarabu na alihusika kumuua, Rais Abeid Karume.

Alisema pia CCM kina laana inayotokana na ubaguzi wa kutowezesha upatikanaji wa haki za msingi kwa makundi mbalimbali katika jamii, akitolea mifano ya wafanyakazi, wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu na hata manyanyaso wanayopata wazee wastaafu waliokuwa watumishi wa EAC.

"Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake, kwa kushirikiana na waasisi wengine,alijenga misingi ya utaifa wetu, ambapo CCM wameamua kuivunja kwa maslahi ya wachache. Akiwa bado hai, Mwalimu alitunga hata kitabu akasema CCM kimeoza na kinanuka rushwa. Akaongeza CCM kuna kansa ya uongozi na uchaguzi ndani ya chama hicho, ni gulio la wala rushwa (kura). Maneno hayo ni laana tosha.

"CCM kinapata laana ya Mwalimu Nyerere kwa sababu kimerasimisha ubaguzi kwa wanachama wao, viongozi wao na Watanzania kwa ujumla. Ni hawa hawaCCM wanaoeneza uongo wa hatari, wakiwatisha wananchi kwa kusema CHADEMA kina ukabila, mwaka 2005 walimzushia Dk. Salim Ahmed Salim uongo kuwa ni Mwarabu na alihusika na kifo cha aliyekuwa mmoja wa wasisi wa taifa hili, Abeid Amani Karume. 

"Uchafu ulifanywa na wana CCM wa kundi la wanamtandao ambao leo ndiyo wanaongoza chama na serikali na ubaguzi huu dhidi ya Dk. Salim ndiyo uliowafanya washinde uchaguzi wa ndani ya chama chao, kwenye kura za maoni;

"CCM kinakufa pia kwa sababu ya laana ya ubaguzi wa kuwezesha raia kupata haki zao na badala yake vyombo vya dola chini ya Serikali inayoongozwa na CCM viko mstari wa mbele kukiuka haki za raia. Ninyi ni mashahidi namna ambavyo baadhi ya makundi ya wafanyakazi yamekuwa yakibaguliwa katika kupata stahiki zao. CCM na serikali yake, imekuwa ikijibu kwa kauli za kejeli na vitisho, ikiwemo kutekwa na kuteswa kwa mmoja wa viongozi wa wafanyakazi na kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande.

"CCM inayokufa tayari imeacha misingi yake ya kuwa chama cha wafanyakazi na badala yake imejichimbia kaburi kwa kuongeza pengo la tofauti za mishahara na maslahi ya wafanyakazi katika utumishi wa umma. Kwa upande mwingine, unaweza kuielezea vipi hali ya serikali ya CCM kutowalipa wazee wastaafu waliokuwa watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama si ubaguzi! Wazee ambao wametumikia taifa hili kwa uwezo wao, akili zao na miili yao.

"Wenzao wote katika nchi nzingine zilizokuwa zikiunda EAC wakati ule, walishalipwa, isipokuwa hapa Tanzania ambapo chama kinachotawala kimeamua kufanya ubaguzi wa haki za watu, nani apate na yupi asipate. Itakumbukwa kuwa wazee wale kutokana na kuyumbishwa na kubaguliwa katika kupata haki zao, waliamua kuvua nguo barabarani, pia kwa kiburi na ukosefu wa heshima ya serikali ya CCM kwa wananchi, wakawachapa viboko wazee wale! Laana ya wazee hawa inakiua CCM," alisema Kigaila.

CHADEMA waibua upya hoja ya familia ya Nape

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Kigaila alisema kuwa kabla Nape hajahangaika kufanya utabiri wa kifo cha CHADEMA, kazi ambayo haiwezi, aanze kwa kutafuta ukoo wake, kwani inawezekana mambo ya 'hovyo' anayoyafanya au kutamuka, yanatokana na matatizo ya malezi tangu akiwa mtoto.

Akitumia tangazo la kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Marehemu Brigedia Jenerali, Moses Nnauye, Kigaila alisema Nape haonekani sehemu youote, kuanzia kwa watoto, wakwe, wajuu, hivyo kuendelea kutumia jina la mtu mwenye heshima kama baba yake, wakati haoneshi kuwa na heshima hiyo kama alivyokuwa Mzee Nnauye ni fedheha.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *