Katika siku za hivi karibuni umezuka mjadala juu ya kukithiri kwa vitendo vya uhalifu unaohusisha wezi kuingia kwenye nyumba za watu nyakati za usiku na kuwapulizia dawa ya usingizi na kisha kuchukua chochote wanachokitaka ndani ya nyumba.
Baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha aina hiyo ya uhalifu na ushirikina lakini ukweli ni kwamba ipo dawa mojawapo ya usingizi ambayo hutumiwa na wezi wengi kutekeleza uhalifu huo.
Lakini pia kwa watu ambao wanaangalia filamu za kihalifu ni wazi kwamba wanaweza kuona mfanano wa jambo hili au lingine la kuendana nalo ambapo Mtuhumiwa humnyatia mtu kwa nyuma na kumfunika na kitu puani halafu muda mfupi baada ya hapo aliyefunikwa huanza kulegea au kuzimia kabisa.
Kama huwa unachunguza sana kuhusu matukio haya yawezekana umeshawahi kujiuliza, Je, ni dawa gani inayotumika kumlegeza au kumzimisha mtu kiasi kwamba ashindwe kujitambua na kuhisi chochote na wahalifu wakafanya chochote wanachoweza kwa muda wa kutosha.Dawa hiyo inajulikana kama ‘Chloroform’ ambayo imekuwa ikutumiwa na wataalamu wa afya katika shughuli za kitabibu hasa wakati wa upasuaji.
Chloroform ni nini?
‘Chloroform’ ni dawa isiyo na rangi na yenye harufu nzuri yenye jina la ‘IUPAC’ lijulikanalo kitaalamu kama ‘Trichloromethane’ na ina fomula ya CHCl3. Chloroform inaweza kukufanya usinzie hata kama itatumiwa kwa dozi ndogo.
Chloroform ni kimiminika chepesi na chenye harufu nzuri ambacho kimekuwa kikitumika kwa miaka mingi kama dawa za ya usingizi wakati wa upasuaji (surgery). Kutokana na kuwa na nguvu hiyo kimepewa sifa ya kufanya mtu alegee au kuzimia kabisa hata pale kinapotumika kwa kiwango kidogo.
Chloroform kama dawa ya usingizi
Chloroform ilitumiwa kwa mara ya kwanza kama dawa ya usingizi mwaka 1847 na mtaalamu wa masuala ya uzazi aitwaye James Young Simpson; yeye aliitumia kwa watu wawili kama njia ya burudani.
Siku chache baadaye, ilitumiwa kwenye ufanisi wa afya ya meno huko Edinburgh na haikuonesha madhara yoyote. Baadaye umaarufu wake kama dawa ya usingizi ulikua kwa kiwango kikubwa na kuvuka mipaka, kiasi kwamba iliweza kutumiwa kwenye uzalishaji wa watoto wawili wa mwisho wa Malkia Victoria katika miaka ya 1850.
Lakini baadaye umaarufu wake ulianza kupungua baada ya kupatikana kwa dawa zingine nzuri zaidi na zenye madhara kidogo zaidi ya Chloroform.
Choloform inavyofanya kazi
Chloroform huathiri mfumo mzima wa fahamu na kuathiri ini pamoja na figo na kwa kiwango kikubwa huweza kuathiri mfumo wa hewa na kusababisha mtu kulala muda mrefu hata miaka (coma). Utumiaji kidogo wa dawa hii hufanya mtu kulegea au kuzimia kabisa na ikitumika kwa kiwango kikubwa huweza kusababisha kifo kwa yule aliyepewa.
Madhara ya Chloroform kwa binadamu
Madhara ya Chloroform kwenye mwili wa mwanadamu hutegemea kipimo cha dozi na njia iliyotumika kuisambaza.
Kwa mujibu wa Idara ya Huduma za Afya ya taasisi ya Wisconsin wanasema, “Mara tu au muda mfupi baada ya mtu kuvuta kiwango cha 100 ppm (100,000 ppbv) ya Chloroform katika hewa, mtu huyo huanza kuhisi uchovu, kizunguzungu na kuumwa kichwa.”
Hata hivyo watu wengi tunachanganya Chloroform na kimiminika kinachowekwa kwenye kitambaa kinachotumika kuwazimisha watu kwenye filamu, lakini madhara ya Chloroform ni makubwa zaidi na yasipodhibitiwa haraka huweza kusababisha kifo.
Madhara ya Choloroform kwa binadamu huongezeka sambamba na kiwango cha dozi yake. Wakati kiwango kidogo kinasababisha kutojielewa, kadiri dozi inavyoongezeka huweza kukufanya uzimie kabisa au usisikie mguso wowote. Kwa kiwango kikubwa zaidi huweza kusababisha upumuaji wa shida, misuli ya mwili kutulia kabisa, misuli ya kifua kupooza na mwishowe kupelekea kifo.
Inachukua muda gani kwa Chloroform kukuzimisha?
Wakati Chloroform iliyowekwa kwenye kitambaa huweza kukuzimisha kabisa, lakini huchukua muda mrefu zaidi ya vile inavyoonekana kwenye filamu nyingi (Huwezi kuzimia ghafla tu baada ya kuinusa). Inaweza kuchukua angalau dakika 5 mpaka mtu kuzima kabisa.
Dhana ya kupotea hewani
Chloroform ni kimiminika mvuke, hivyo hupoteza nguvu yake ya kufanya kazi pale tu kinapokutana na hewa ya Oksijeni. Hivyo basi muhalifu aliyeshika kitambaa chenye Chloroform na kumuwekea mtu usoni inakuwa sio mazingira halisi maana Chloroform inapokuwa kwenye kitambaa inakuwa imepoteza nguvu yake hata kabla haijawekwa kwenye pua ya muhanga.
Je, tunaweza kunywa Chloroform? Inaua?
Jibu ni ndiyo. Kwa kuangalia jinsi inavyotumika kwenye filamu unaweza kudhani ni kimiminika tu kama vile visivyo na madhara kwa watumiaji. Hilo ni uongo.
Inaweza kusababisha mauti kwa mtumiaji pale itakapotumika kwa kiwango kisicho sahihi au kitambaa chenye Chloroform kikiwekwa haraka kwenye uso wa mtu. Muhanga anaweza kushindwa kupumua na baadae kufa.
Wataalamu wa afya hawatumii Chloroform siku hizi kwasababu ni vigumu kutambua kiwango halisi cha dozi ili kumzimisha mtu bila kuathiri mfumo wa fahamu. Hivyo kunywa tu hata kwa kiwango kidogo kunaweza kusababisha mauti.
Tunahitaji tahadhari hasa kwa wasambazaji wa dawa hii ambayo imekuwa ikileta hasara kwa mali za watu kuibiwa katika nyumba zao nyakati za usiku.
Hiyo Chloroform ni hatari,lakini swali langu ni je Wizara yetu ya Afya inasemaje juu ya dawa hiyo ?