Daktari Feki afanya ziara gharama ya Halmashauri Ngara; apewa ulinzi na Polisi

Jamii Africa

Kama vile mlolongo wa vituko na kashfa havijaisha serikalini huko Ngara mtu aliyejitambulisha kuwa ni daktari wa magonjwa ya binadamu na afisa kutoka Wizara ya Afya ameivuruga wilaya ya Ngara mkoani Kagera na kuitia hasara baada ya kufunga kituo cha afya Bukililo na kushuhudia kazi ya upasuaji wa wagonjwa katika hospitali ya misheni Rulenge. Yote yakigharimiwa na kufanyika chini ya halmashauri ya Ngara inayoongozwa na CCM.

Mtaalamu huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Dr. Illongo Mlawa kabla ya kugundulika kuwa ni tapeli aliongozana na msafara wa watendaji wa halmashauri akiwa na ulinzi wa polisi kwa kile alichodai ni kukagua shughuli zilizoko chini ya wizara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo John Shimilimana aliyekuwa pia katika msafara huo,alijitambulisha kuwa ni Naibu Katibu mkuu idara ya Utumishi.

Aidha mtaalamu huyo’feki’ alikaa kwenye halmashauri hiyo kwa siku tatu huku akigharamiwa kila kitu kama kiongozi kutoka wizarani, na kupewa ulinzi wa jeshi la polisi ambalo hivi karibuni limejikuta likikumbwa na kashfa ya kutumia nguvu zaidi . “Ameitia halmashauri yetu hasara kubwa nimeishamuagiza mkurugenzi ahakikishe gharama zote zilizotumika kwa ajili yake zinarudishwa,alikuwa na msafara mkubwa wa magari wakati akizungukia vituo vya afya”alieleza mwenyekiti huo.

Aidha mwenyekiti huyo alilalamika kuwa alilazimika kuwaita madiwani siku ya Jumamosi ili wakutane na kiongozi huyo,ambaye alitoa maelekezo ya kutaka watumishi wa idara ya afya kulipwa stahili zao haraka baada ya kupokea malalamiko ya kutolipwa kila alipopita.

Mgeni huyo katika wilaya ya Ngara alikifunga kituo cha afya Bukililo kwa madai kuwa hakuridhika na kiwango cha huduma zilizokuwa zinatolewa,na mwenyekiti kudai kuwa halmashauri iliingia gharama kubwa kuwahamisha wagonjwa kwenda vituo vingine. Pia John Shimilimana aliiambia Fikrapevu kuwa baada ya kuagiza kufungwa kwa kituo hicho walimbembeleza kuwa wagonjwa wangeweza kupoteza maisha kwa uamuzi huo wa ghafla,jambo alilodai angelifikilia baadaye baada ya kuwa wametekeleza agizo lake.

“Kama mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngara nilimbembeleza asikifunge kituo cha Bukililo kwani wagonjwa wengi wangeteseka na kupoteza maisha,tuliwahamishia katika vituo vingine”alisema Shimilimana.

Pia kutokana na wadhifa wake na kujitambulisha kuwa ana taaluma ya udaktari na ni kiongozi wizarani  aliruhusiwa kuingia katika chumba cha upasuaji wa wagonjwa katika hospitali ya Misheni Rulenge na kushuhudia madaktari walivyokuwa wakiendelea na majukumu yao. Hata hivyo mwenyekiti huyo alidai kiongozi huyo alianza kushtukiwa baada ya kuingia na kutoka katika chumba cha upasuaji katika hospitali ya Rulenge ambapo pamoja na kuvaa mavazi yanayotumiwa na madaktari tayari kwa upasuaji hakuweza kuhoji wala kuuliza suala lolote linalohusiana na taaluma hiyo.

Mwenyekiti huyo amedai baada ya halmashauri kufanya mawasiliano na wizara iligunduika kuwa hakuna kiongozi yeyote aliyetumwa huko na hakuna rekodi zozote za jina linalohusiana na mtu huyo.

Kwa mujibu wa Shimilimana Dk Ilongo Mlawa baadaye alikamatwa juzi na kuwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Henry Salewi  alipopigiwa simu kuhusu tukio hilo aliomba apewe muda kwa maelezo kuwa alikuwa anaendesha kikao.

(Phineas Bashaya, Fikra Pevu)

7 Comments
    • Kumbe hii nchi unaweza hata kuingia ikulu ukajitambulisha mgeni wa mkuu wa nchi ukaingizwa hadi chumbani, tehe tehe tehe. Jamaa anastahili heshima.

  • waliompokea na msafara wake wanastahili adhabu kwanini hawakuwasiliana na wizara kabla ya ujio wake na mhuni huyu wakampokea na kuanza kumkarim bila kuhoji uhalali wa ujio wake .NANI KAMTUMA NA KWANINI ,NA KWANINI ASILIPWE NA WIZARA .HUU NI UHUNI Mimi siwezi kukurupuka hapa nilipo na kwenda h/mashauri fulani na kupokewa na kuanza kulipwa mafao bila kuhoji

  • Kweli tunakoelekea ni kubaya aisee!!.hii inaonyesha jinsi gani viongozi wetu walivyo wazito kujua mabosi wao kwa majina.ona sasa gharama zisizo na kichwa wala mdomo walizoingia.

  • sasa inamana hakuna mawasiliano kati ya mikoa na wizara? au utaratibu wa kutambulisha mgeni ni mbovu kiasigani gadi mtu huyo kutikisa wilaya bila kujulikana kwa siku 3? hii ni aibu kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *