Matumizi ya njia za mpango wa uzazi zenye kubadilisha vihemuko (hormones) ambazo zimekuwa zikitumiwa na wanawake wengi katika maeneo ya Afrika chini ya Jangwa la Sahara zimeonekana kuonesha uwezekano wa kuongeza uwezekano wa maambukizi ya virusi vya HIV-1 ambavyo husababisha ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa wanawake wenye kutumia njia hizo za mpango wa uzazi kwa kujidunga sindano wana uwezekano wa karibu mara mbili kuweza kuambukizwa HIV kulinganisha na wanawake ambao hawatumii njia hizo. Vile vile utafiti huo unaonesha pia kuwa kama ni mwanamke ndiye ameshambukizwa basi anaongeza pia uwezekano wa kumuambukiza mwenza wake.
Utafiti huo umefanywa na wataalamu toka Vyuo Vikuu vya Washington na Seattle huko Marekani. Utafiti huo umehusisha karibu watu 4000 huku ukifanyika katika nchi saba za kiafrika Tanzania ikiwa ni miongoni mwao. Nchi nyingine zilizohusishwa katika utafiti huo ni pamoja na Botswana, Kenya, Rwanda, na Afrika ya Kusini. Nyingine ni Uganda na Zambia.
Katika utafiti huo wenza wawili walichunguzwa ambapo mmoja wao alikuwa anajulikana tayari ana HIV. Watafiti walitaka kuangalia ni njia gani za uzazi wa mpango ambazo zinatumika na kasi ya mtu kuambukizwa HIV. Matokeo ya utafiti wao yamechapishwa katika jarida la kimataifa la magonjwa ya maambukizi la The Lancet Infectious Diseases.
Katika nchi nyingi za Kiafrika Tanzania ikiwa ni mojawapo wanawake wengi wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za uzazi wa mpango (Nyota ya Kijani) na kati ya mbinu nyingi DM-Depo Plovera imekuwa ni maarufu sana hasa kutokana na urahisi wa matumizi yake na kwa vile mwanamke anadungwa sindano mara moja kwa mwezi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wengi wa washiriki 3790 walioshiriki utafiti huo walikuwa ni wanawaka waliokuwa na HIV-1 na wengi wao walikuwa na wameolewa na wana watoto. Umri wa kati ni miaka ya thelathini. Asilimia 24 ya ambao walikuwa hawajaambukizwa walikuwa ni wanawake wenye chini ya umri wa miaka 25.
Utafiti huo haudai kuwa dawa ya uzazi wa mpango ndio inasababisha maambukizi ya virusi vya UKIMWI bali inasema tu kuwa kuna uhusiano kati ya matumizi ya dawa hizi za uzazi wa mpango na kasi ya kuongezeka kwa uwezekano wa kuambukizwa HIV. Kwa maneno mengine, matumizi ya dawa kama DM-Depo Plovera kwaweza kumfanya mwanamke au mwanamme kuambukizwa virusi (na mtu aliyeambukizwa tayari) kwa urahisi zaidi kuliko kama mwanamke asingetumia njia hiyo ya uzazi wa mpango.
Hata hivyo, matokeo haya ni matokeo ya awali na ambayo bila ya shaka yatahitaji kurudiwa na watafiti wengine kabla hayakubaliwa kabisa. Lakini kwamba upo uwezekano huo ni jambo ambalo wataalamu wetu wa afya wanapaswa kuliangalia kwa umakini kwani matumizi ya uzazi wa mpango kwa kutumia dawa zenye kubadilisha vihemuko ndiyo ya juu zaidi kuliko njia nyingine yoyote. Utafiti mwingine umewahi kuonesha huko nyuma kuwa kwa nchi za Afri ya Mashariki matumizi ya dawa kama Depo Plovera yanafikia asilimia 58 ya njia nyingine zote za mpango wa uzazi huku matumizi ya mipira ya kiume (Kondom) yakiwa ni kama asilimia 22 tu. Kwa Tanzania kiwango cha matumizi hayo kiliripotiwa ni kuwa ni asilimia 65.7 kwa wale waliofanyiwa utafiti.
Kwa namna yoyote ile endapo utafiti zaidi utaweza kuonesha uhusiano wa moja kwa moja (direct relation) kati ya matumizi ya njia hizi za mpango wa uzazi na kasi ya maambukizi ya HIV-1 kutalazimisha fikra mbadala zipendekezwe katika kusaidia kuchangia kupunguza maambukizi ya virusi hivi kama taarifa ya jando ya wanaume ilivyobadilisha na kuchangia kupunguza maambukizi ya virusi hivi. Miaka michache iliyopita iligunduliwa (kwanza huko Afrika ya Kusini) kuwa wanaumewa waliofanyiwa jando wanauwezekano mdogo wa kuambukizwa na kuambukiza virusi kulinganisha na wanaume wasiofanyiwa na matokeo yake nchi nyingi za kiafrika zilianza kuhamasisha wanaume kutahiriwa.
Na. M. M. Mwanakijiji
Unaweza kusoma hapa: RIPOTI KAMILI