Dhahabu: Acacia Mining walikuwa wapi kuhoji usawa wa mikataba?

Daniel Mbega

JUMATANO, Mei 24, 2017 Rais Dkt. John Magufuli alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ajiuzulu mara moja kufuatia upotevu wa mabilioni ya fedha katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makanikia).

FikraPevu inaelewa kwamba, uamuzi huo aliutoa wakati akipokea Ripoti ya Kamati ya Kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ambayo aliiunda kuchunguza kuhusu makanikia yaliyozuiliwa katika bandari mbalimbali nchini, ambayo ilionyesha kumekuwepo na uzembe mkubwa ulioikosesha Serikali mabilioni ya fedha.

Mbali ya kumtaka Waziri Muhongo ajiuzulu, aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) pamoja na kumsimamisha kazi mkurugenzi wa wakala huo huku akiagiza wafanyakazi wa wizara wachunguzwe na vyombo vya dola.

Mambo hayo yote yamekuja baada ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa dhahabu baada ya kuelezwa kwamba mchanga huo ulikuwa na kiasi kikubwa cha madini mengine ambayo hayakuainishwa kwenye mikataba, hivyo kuifanya Tanzania ipoteze fedha nyingi.

Uamuzi wa kuzuia usafirishaji huo ulikuja baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam Machi 3, 2017 na kutoa amri ya kuzuia makontena 20 yaliyokuwepo pamoja na mengine yaliyokuwa kwenye bandari nyingine nchini hadi hapo yatakapochunguzwa na kujua kiasi halisi ya madini yaliyomo kwenye makanikia hayo.

Mikataba haina usawa

FikraPevu inafahamu kwamba, mara baada ya zuio hilo la Serikali, wadau mbalimbali wa sekta ya madini walipinga uamuzi huo huku wakiwatetea wawekezaji katika sekta hiyo kwamba wanafanya shughuli zao kihalali kwa mujibu wa mikataba.

Aidha, ilielezwa kwamba, kiwango cha dhahabu kilichokuwemo kwenye makanikia hayo kilikuwa ni asilimia 0.02, ambacho walisema ‘ni cha kawaida’ kabisa.

Mgodi wa North Mara.

Lakini FikraPevu inatambua kwamba, zuio hilo lilimuibua Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Acacia Mining, Brad Gordon, ambaye katika mahojiano na gazeti la Telegraph la Uingereza Machi 12, 2017 alisema kwamba mikataba ya madini ilikuwa ya kisheria ingawa ‘haina usawa’.

Acacia Gold inaendesha migodi mitatu nchini Tanzania ambayo ni North Mara Goldmine, Bulyankulu na Buzwagi, ambao mkataba wake ulikuwa na utata mkubwa baada ya kudaiwa kusainiwa katika chumba cha hoteli nchini Uingereza mwaka 2007.

FikraPevu inafahamu kwamba, kuibuka kwa Mtendaji Mkuu wa Acacia Mining na kueleza ‘udhaifu’ wa mikataba hiyo kulikuja baada ya mauzo ya hisa ya kampuni hiyo kuporomoka ghafla baada ya zuio la usafirishaji wa makanikia.

Inaelezwa kwamba, kabla ya zuio hilo, kampuni hiyo ilikuwa imetangaza kugundua hazina kubwa ya dhahabu Magharibi mwa Kenya, ingawa inaendelea kutafiti dhahabu nchini Mali na Burkina Faso.

Brad Gordon, Mtendaji Mkuu wa Acacia

Aidha, FikraPevu inafahamu pia kwamba, mwezi Januari Acacia (zamani ikijulikana kama African Barrick Gold), ambayo inamilikiwa kwa asilimia 64 na Barrick Gold ya Canada, ilikuwa katika mazungumzo ya kuuza hisa zao kwa kampuni ya Endeavour Mining iliyoko jijini Toronto, Canada, ambayo inamiliki migodi mitano katika nchi za Mali, Ivory Coast, Burkina Faso na Ghana.

Inaonekana mazungumzo hayo yalivuja kabla ya kufikia mahali pazuri, lakini Gordon akasema kwamba bado yanaendelea.

Acacia hawasemi moja kwa moja kwamba mikataba ya madini ni ‘dhaifu’ bali wanatumia lugha ya ‘haina usawa’ katika kutetea kile ambacho Watanzania wamekuwa wakilalamika kwamba kuna uporaji mkubwa wa rasilimali zao, hasa madini.

“Sekta hii inajipalia makaa yenyewe wakati inapotulia na kukubaliana na masharti haya, madhara yake ni kwamba itakuja kututafuna. Na katika suala hili (la kuzuia usafirishaji wa makanikia) imekwishatutafuna,” Gordon alikaririwa na gazeti la Telegraph.

Tena kampuni hiyo inajitetea kwamba ni mlipaji kodi mzuri huku ikitoa kiasi cha Dola 162 milioni kwa kodi mbalimbali mwaka 2016.

Inapinga kila kitu

FikraPevu inafahamu kwamba, mapema Jumatano, Mei 24, 2017, muda mfupi kabla Rais Magufuli hajakabidhiwa Ripoti ya Uchunguzi wa Makanikia, kampuni Acacia Mining ilitoa taarifa kuhusu ripoti hiyo (bila hata kuona), na kuendelea kusisitiza kwamba taarifa zake ni sahihi.

Acacia walisema huwa wanatoa taarifa kamili ya kila kitu chenye thamani ya kifedha ambacho wanazalisha na huwa wanalipa kodi zote stahiki kwa kila madini yanayotakiwa kulipiwa.

Makontena yenye mchanga wa dhahabu yaliyozuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Muda mfupi baada ya Rais Magufuli kupokea taarifa hiyo, Mtendaji Mkuu wa Acacia Mining, Brad Gordon, alitoa taarifa akipinga vikali matokeo ya uchunguzi wa Kamati teule ya Rais kwamba thamani ya madini yaliyomo kwenye makanikia yaliyozuiliwa ni mara 10 ya thamani ambayo wao waliionyesha kwenye nyaraka.

“Hatukubaliani na matokeo ya Kamati yanayoeleza kwamba thamani ya madini kwenye makanikia yaliyozuiliwa kwenye makontena katika Bandari ya Dar es Salaam ni mara 10 ya tuliyoainisha. Tuna uhakika na usahihi wa taarifa zetu ambazo zinapitiwa na kuthibitishwa na SGS, ambayo ni moja ya kampuni kubwa za upimaji duniani,” alisema Gordon kwenye taarifa yake.

Hata hivyo, katika taarifa hiyo ambayo FikraPevu imeiona, Mtendaji Mkuu huyo wa Acacia alikiri kwamba wastani wa madini yaliyomo kwenye kila kontena ni Shs. 300 milioni ambapo yanahusisha Shaba 3,000kg, Dhahabu 3kg na Silver 3kg.

“Makanikia tunayozalisha yana viwango tofauti, na kila kontena lina viwango tofauti vilivyoainishwa kwenye nyaraka, lakini kwa uhakika kwamba tunaamini kila kontena lina wastani wa 3,000kg za Shaba, 3kg za dhahabu na 3kg za silver. Kwa pamoja, madini haya yana thamani ya Shs. 300 milioni kwa kila kontena,” ilisema taarifa ya Gordon.

Ripoti ya uchunguzi ya Kamati teule ya Rais ilieleza kwamba, katika makontena 277 yaliyochunguzwa imebainika kuwepo kwa viwango vya juu vya madini ya dhahabu, shaba, chuma na mengine tofauti na inavyoonyeshwa kwenye nyaraka za wawekezaji hao.

Ripoti ya kamati hiyo imeeleza kwamba, baada ya uchunguzi imebainika kuwa makontena yote hayo yalikuwa na jumla ya tani 1.2 za dhahabu yenye thamani ya Shs. 7.5 bilioni, silver gramu 202.7 – 351 kwa tani, lakini iliripotiwa nusu tu ya gramu zilizomo kwenye kila kontena.

“Madini ya Sulphur ni 16.7 – 50.8 kwa tani (kwa tani zilizopatikana 2,161 kwa makontena 277) ambazo zina thamani ya Shs. 1.4 bilioni,” ilisema ripoti hiyo.

Aidha, madini ya Chuma ni 13.6 – 30.6 kwa tani (kwa makontena yote 277) yakiwa na thamani ya Shs. 2.3 bilioni, na madini ya shaba ni 17.6 – 23.3 kwa tani (kwa makontena 277) ambayo yana thamani ya Shs. 13.6 bilioni.

“Madini yote haya yalikuwa na thamani ya jumla ya Shs. 261.5 bilioni,” alisema Profesa Mruma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo. “Mheshimiwa Rais, hivyo ndivyo viwango na mapato tuliyopoteza.”

Kwa msingi huo, Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti hiyo alisema Tanzania inapoteza kati ya Shs. 676 bilioni hadi Shs. 1.5 trilioni kupitia madini ambayo hayarekodiwi, jambo ambalo linaitia umaskini nchi hiyo.

“(Shilingi) Bilioni 676 hadi trilioni 1.5 tunazipoteza Watanzania, madini mengine hawakujali hata kuyarekodi. Tunaweza tukaona kwa miaka 17, tulipaswa kuwa donor country (nchi hisani) kwa vitu tulivyopewa na Mungu,” alisema.

Lakini FikraPevu inatambua kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kukanusha taarifa zinazotolewa kuihusu, kwani hata katika migogoro inayotokea kwenye migodi yake baina yake na wananchi imekuwa ikipinga takwimu halisi zinazotolewa.

Mgodi wa North Mara, ambao unagusa vijiji saba wilayani Tarime, kwa muda mrefu umeripotiwa kuwa na migogoro na wananchi, ambapo ripoti moja ya serikali iliwahi kusema kwamba kati ya mwaka 2006 hadi 2014 jumla ya raia 65 waliuawa na polisi na wengine 270 kujeruhiwa kwa madai ya kuvamia mgodi huo.

Lakini katika mahojiano na gazeti la Telegraph la Uingereza, Gordon alisema hazitambui takwimu hizo.

“Tunajua kuna watu waliouawa kila mwaka. Lakini idadi ambayo ipo kwa miaka mitatu au minne iliyopita, haijitokezi tena sasa,” alisema na kuongeza kwamba asingeweza kutaja idadi ya waliokufa. “Nisingependa kusema. Kwa sababu nitakapoingia kwenye hilo (takwimu), utamhusisha nani na utamtoa nani?”

Wanavyosema wadau

Wadau mbalimbali wanahoji uhalali wa mikataba mibovu ambayo haina maslahi na umma wa Watanzania kwamba imesainiwa kwa maslahi ya nani.

“Sera ya Madini ni kweli haina shida imeandikwa vizuri tu, tatizo hapo ni hiyo mikataba mibovu tuliyoingia ambayo imetokana na sheria zetu mbovu kuhusu madini,” wanasema wananchi hao.

Hata hivyo, wapo wanaopinga hatua hiyo kwa kusema uamuzi huo utaligharimu taifa kwa madai kwamba kuna baadhi ya vitu vimepotoshwa.

Mchangiaji wa JamiiForums anayejiita Second July, amedai kwamba mapato yanayodaiwa kupotea kati ya Shs. 676 bilioni na Shs. 1.147 trilioni ya dhahabu siyo sahihi.

“Hizi ni true value (thamani halisi) ya dhahabu iliyomo kwenye makontena ambayo ikiuzwa, serikali kupitia TRA itachukua kodi/tozo/mrabaha wa 4% kwa Sheria ya sasa,” alisema.

Lakini Mzee Mwanakijiji, mmoja wa wachangiaji wakongwe wa mtandao wa JamiiForums, amepongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti hiyo.

“Baada ya ripoti ya jana (Mei 24, 2017), na yote yaliyosemwa, Rais alikuwa anatakiwa afanye nini? Aunde kamati nyingine kuthibitisha matokeo ya kamati ile; au aanze tena uchunguzi wa kuchunguza alichounda kuchunguzwa?” alihoji mchambuzi huyo.

Akaongeza: “Tuchukulie kwa mfano baada ya ripoti ile iliyojaa "madoido" ya Prof. Mruma, Rais angesema ni ripoti nzuri anawashukuru halafu watu wakaondoka zao bila hatua yoyote kali; kwamba alitaka kujua tu kinachoendelea; ni sauti gani zingepazwa? Siyo kwamba Magufuli angeonekana anambeba tena Muhongo?”

Mzee Mwanakijiji amesema kwamba, baadhi ya wananchi wanategemea Rais Magufuli atakwenda mbele zaidi ya kumtimua Muhongo, maana tayari kuna watu wengine wengi wamekwenda na maji na kupoteza nafasi zao na kwamba hatashangaa wengine wakajikuta kizimbani.

Amesema kwamba, majibu ya kampuni ya Acacia yamejaa ujanja wa maneno na inapuuzia ukweli ambao wengi wanaujua – kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye ufisadi wa kutisha.

“Suala la ufisadi Tanzania halijakoma kwenye sekta moja; sekta ya madini ni miongoni mwa sekta ambazo zimeathirika sana na ufisadi. Zipo ripoti nyingi zinazoonesha jinsi makampuni makubwa ya uchimbaji madini yanavyotumia mbinu mbalimbali nyingine za kibabe (bullying tactics) katika kuzibana nchi na serikali zisizokaa kwenye mstari wao.

“Namna pekee ya kuelewa uzito wa ripoti hii na hatua za Rais ni kuangalia ufisadi kama sehemu kubwa ya haya yanayotokea. Ni nani ambaye hajui jinsi gani ni rahisi kupenyeza rupia ili kupitisha au kujaza fomu fulani ziseme kile ambacho kitaridhisha macho ya wakubwa fulani?” akabainisha.

Amesema ni lazima ifike wakati kujua kuwa kuna umaskini unaoweza kutokana na mtu kupoteza vitu fulani, lakini umaskini wa Watanzania ni wa kuamua kwa hiari na kwa kushirikiana wenyewe kupoteza mali zao ili wasiwaudhi wakubwa.

“Wakati umefika tuwe tayari kuwaudhi wakubwa ili angalau watoto wetu waje kufurahi baadaye. Ndugu zetu wanaotaka tuingiwe na hofu ya kuwa sasa tutakiona cha moto wanasikitisha sana; ina maana wenzetu hawa watakuwa wanapiga magoti kila wakipigwa mikwara na makampuni haya makubwa? Ina maana wenzetu watatuma washenga kwenda kuwabembeleza wasiondoke?” anahoji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *