Dk. Chami ajibu mapigo sakata la TBS bungeni

Jamii Africa

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Cyril Chami amejitetea kwamba yeye na wizara yake hawamlindi Mkurugenzi Mkuu wa TBS Bwana Charles Ekelege kama alivyotuhumiwa na baadhi ya wabunge mjini Dodoma katika kikao cha Bunge kinachoendelea sasa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami

Dkt Chami amesema kilichotokea ni Wizara yake kufuata sheria na kanuni zote za usimamizi wa mashirika ya Umma kama zinavyoainishwa katika Waraka wa Msajili wa Hazina wa mwaka 2004 unaoelezea utaratibu wa wizara kufuata katika kuyasimamia mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara hizo.

 

Amesema kwa kipindi chote cha uongozi wake, ameutumia utaratibu wa “eyes on, hands off” ambao ndio utaratibu unaokubalika wa kusimamia mashirika yaliyo chini ya wizara yoyote. Utaratibu huu unautaka uongozi wa wizara zote kuyasimamia mashirika ya umma lakini pia kutokuyaingilia katika utendaji wake wa kazi.

 

Dkt Chami anaeleza kuwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, mamlaka ya kwanza ya usimamizi wa Shirika la Umma ni ile ya bodi za wakurugenzi ambayo mara nyingi wenyeviti wake ni wateule wa Rais.

 

“Wengi wanadhani Waziri anaweza kuamua kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Shirika la Umma bila kupata maoni ya Bodi na kibali cha Rais, lakini siyo sahihi. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umma akituhumiwa na yeyote, kanuni zinaelekeza kuwa Waziri anapaswa kupata ushauri wa Bodi ya Wakurugenzi juu ya tuhuma zilizotolewa, na baada ya ushauri huo naye, kwa Wakurugenzi walioteuliwa na Rais, atamshauri Mheshimiwa Rais ipasavyo ili Mheshimiwa Rais aelekeze inavyofaa,” alisema Dkt Chami.

 

“Hata hivyo, pale ambapo Bodi itaona kuwa uwepo wa Mkurugenzi mhusika ofisini wakati anachunguzwa utaufanya uchunguzi usiende vema, Bodi hiyo hiyo inaweza kuishauri Serikali ili Mkurugenzi husika asimamishwe kwa muda hadi hapo uchunguzi kamili juu yake utakapokamilika,” anasema.

 

Dkt Chami alisema tuhuma kwamba TBS haifanyi kazi yake sawasawa zilitolewa kwa mara ya kwanza na waheshimiwa wabunge katika Bunge la Tisa, jambo lililomfanya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kusimamia Mashirika ya Umma wakati huo, Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, aunde kamati Ndogo iliyoongozwa na Makamu wake wakati ule, Mheshimiwa Esterina Kilasi, aliyekuwa Mbunge wa Mbarali.

 

Taarifa ya Kamati hii ndogo iliyotiwa sahihi na Mheshimiwa Kilasi inaanisha changamoto, matatizo na mafanikio ya TBS katika ukaguzi wa magari nje ya nchi. Katika kuhitimisha taarifa yake, Kamati hiyo teule iliupongeza uongozi wa TBS na ule wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, kwa kulisimamia vema zoezi la ukaguzi wa magari pamoja na changamoto nyingi walizokuwa wanakumbana nazo.

 

Kamati ilitoa mapendekezo ya mambo ya kufanya ili kuboresha ukaguzi huo, mojawapo likiwa pendekezo kuwa TBS iwezeshwe kukagua magari nchi nyingi zaidi na la pili, TBS isijikite kwenye ukaguzi wa magari tu bali wakague na bidhaa nyingine. TBS na Wizara zikapokea na kuyafanyia mapendekezo hayo kazi.

 

Dkt Chami anasema moja ya mambo yaliyoonekana yanafaa kwa wakati ule ni kurekebisha sheria iliyoanzisha TBS ili, pamoja na mambo mengine, kuipa TBS jukumu la kukagua kwa lazima magari na bidhaa muhimu zinazoingia nchini kabla hazijasafirishwa kutoka katika nchi zilikozalishwa.

 

Ndipo Bunge likaipitisha sheria namba 2 ya mwaka 2009 inayolitaka shirika hilo kutekeleza zoezi hilo. Anasema Dkt Chami kuwa sheria hiyo iliyowasilishwa Bungeni na mtangulizi wake Mheshimiwa Dkt Mary Nagu na kupitishwa na Bunge mwezi Februari 2009 ilianza kutekelezwa Februari mosi 2012, baada ya Wizara kukamilisha uandishi wa kanuni za uendeshaji wa zoezi hilo na kanuni hizo kusainiwa na mtangulizi wake Dkt Nagu.

 

“Kazi ya TBS na Wizara ni kuitekeleza sheria hii iliyotungwa na Bunge. Kama Wizara na TBS tungeacha kuitekeleza sheria hii ya Bunge tungekuwa tumekwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi yetu. Kama kuna matatizo ya utekelezaji, hapo ndipo tunakaribisha maoni ya kila mdau ili utekelezaji uende vema. Na kama sheria yenyewe haifai, taratibu ziko wazi zinazomruhusu mheshimiwa mbunge yeyote kupeleka kwa Mheshimiwa Spika hoja ya kuliomba bunge liibadili sheria husika, ” alfafanua Chami.

 

Chami alisema njia ya pili ni wizara mama kuanza mchakato wa kuibadili sheria kwa kuipeleka kwenye Baraza la Mawaziri na baada ya kurithiwa, kuipeleka bungeni. Kwa sheria hii ambayo imeanza kutekelezwa Februari mosi 2012, itakuwa kichekesho kama TBS inaanza kuitekeleza sheria na baada ya miezi miwili Wizara inayoisimamia TBS iende tena kwenye Baraza la Mawaziri kuiomba sheria hiyo ibadilishwe, kabla hata ya kupata muda wa kutosha wa kutathmini utekelezaji wa sheria yenyewe.

 

“Jamani nitaonekana waziri wa namna gani endapo nitapendekeza mabadiliko katika sheria ambayo haina hata miezi mitatu katika utekelezaji? Si nitaonekana ndiyo nasukumwa na maslahi binafsi?” alihoji Dkt Chami.

 

Kuhusu madai ya utendaji kazi dhaifu wa TBS na kwamba yeye binafsi na Katibu Mkuu wake wanamlinda Ndugu Ekelege, Dkt Chami alikanusha vikali tuhuma hizo. Alijitetea kwa kusema kwamba hakuna wakati hata mmoja ambako Wizara yake imetakiwa kutoa ushirikiano katika jambo hilo ikasita au ikatoa taarifa zisizo sahihi.

 

Kwa mfano, mwezi August mwaka 2011 Mheshimiwa Zitto aliunda tena Kamati ndogo kwenda kukagua tena shughuli za makampuni yaliyokuwa yamepewa mikataba ya kukagua magari na TBS huko Singapore na Hong Kong. Japokuwa wabunge wale hawakuieleza wizara walichokiona huko, mara baada ya uongozi wa wizara kuona na kusoma kwenye vyombo vya habari jinsi wabunge wale walivyomtuhumu Mkurugenzi Ekelege tarehe 27 Januari 2012, Wizara iliomba kutoka Ofisi ya Spika taarifa ya ziara ya hao waheshimiwa wabunge na walichokiona huko ili Wizara iifanyie taarifa hiyo kazi. Dkt Chami alilieleza gazeti hili kwa masikitiko huku akiwa ameshikilia nakala ya barua kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda kwa Katibu wa Bunge, kuwa hadi leo Wizara haijapokea taarifa hiyo.

 

Badala yake, Wizara ilipata barua kutoka Ofisi ya Bunge ikiutaka uongozi wa Wizara kukabidhi kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) takwimu zinazoonyesha idadi ya magari yaliyokaguliwa na TBS na fedha zilizopatikana tangu TBS ilipoanzishwa mwaka 2002. Wizara ililifanyia kazi agizo hilo lililo kwenye barua ya tarehe 6 Februari 2012 na kukabidhi kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu taarifa hizo tarehe 18 Februari 2012.

 

“Taarifa yenye takwimu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara ndizo zimemwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoa taarifa yake inayotumiwa na waheshimiwa wabunge hivi sasa, sasa hapo mimi na Mama Mapunjo (Katibu Mkuu Viwanda na Biashara) tunamlindaje Ekelege?” alihoji Dkt Chami.

 

Dkt Chami, ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, alisema tuhuma nyingine anayotuhumiwa nayo ni ile ya kutokumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu Ekelege kama ambavyo Kamati tatu zilizokaa Februari 10, 2012 ziliagiza. Katika utetezi wake, anasema aliomba barua kutoka Ofisi ya Spika juu ya agizo hilo lakini hadi jana alikuwa hajapokea barua hiyo japokuwa Bunge linaelezwa kwamba barua hiyo ipo.

 

“Hebu tupime sote. Katika kupata takwimu, Ofisi ya Bunge iliuandikia uongozi wa Wizara ikiagiza kwamba Wizara ipeleke takwimu zinazoihusu TBS kwa CAG. Kwa nini katika hili la kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu tusipate maagizo ya maandishi pia kutoka ofisi ya Spika? Lipi rahisi, kutoa takwimu za magari au kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TBS? Nina hakika hili la kumsimamisha kazi Mkurugenzi ni zito na lilihitaji barua pia, ikizingatiwa huyu ni mteule wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Alifafanua Dkt Chami.

 

Dkt Chami anasema kama angepata barua hiyo asingesita kuomba ushauri wa Bodi na kuwasiliana na mamlaka ya uteuzi (Mheshimiwa Rais) juu ya jambo hilo ili kupata uamuzi wake, kama sheria inavyoelekeza.

 

Hata hivyo Dkt Chami alisema baada ya kusikia tuhuma nyingi hasa kupitia vyombo vya habari juu ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, alimuomba Mheshimiwa Rais aharakishe uteuzi wa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TBS ambayo ilikuwa imemaliza kipindi chake Desemba 2011. Mara baada ya Mheshimiwa Rais kumteua Ndugu Oliver Mhaiki kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi, Dkt Chami aliizindua Bodi hiyo mara na kuiagiza ifanyie kazi tuhuma zilizokuwa zimeenea kuhusu utendaji mbovu wa TBS na Mkurugenzi wake Mkuu na kuishauri Serikali mara moja.

 

“Mapendekezo hayo ya Bodi ndiyo yatafanyiwa kazi na Serikali. Mara nyingi Mawaziri wanaoamua kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Umma bila kupata maoni ya Bodi husika wametuhumiwa kwenda kinyume cha kanuni, na hata kuonekana kusukumwa na maslahi binafsi katika uamuzi wao huo. Mimi naielekeza Bodi ifanye kazi yake na mapendekezo yake yatazingatiwa na Serikali kama inavyoelekezwa katika Waraka wa Msajili wa Hazina Kuhusu Mashirika ya Umma wa mwaka 2004, nimekosea wapi?” Alihoji Dkt Chami.

 

Anasema jambo lililomsononesha ni pale taarifa ya ukaguzi wa CAG juu ya TBS ilipotolewa kwa waheshimiwa wabunge bila yeye mwenyewe au Wizara kupewa nakala kwa kipindi cha wiki nzima.

 

Anasema kutokana na kusikia kuwa waheshimiwa wabunge wengi wanayo taarifa hiyo na hata Naibu wake kukiri bungeni kwamba taarifa imetoka wakati yeye hana, alikwenda kwa Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashillilah na kuiomba nakala ya taarifa hiyo. Kwa mastaajabu hata Dkt Kashillilah alisema alikuwa hajaipokea taarifa hiyo.

 

Alipouliza Wizarani aliambiwa nako pia hawajapatiwa taarifa hiyo. Katika ufuatiliaji, Katibu Mkuu wa Wizara yake alipiga simu ofisi ya CAG, nao wakakiri kuigawa kwa waheshimiwa wabunge na kudai kwamba eti walighafilikiwa wakaisahau Wizara husika.

 

“Ndugu mwandishi, hapa wasomaji wako na wapime wenyewe. Inawezekanaje taarifa ya CAG iliyoandikwa kutokana na takwimu zilizotolewa na Wizara yangu, iwafikie waheshimiwa wabunge huku Wizara yangu itakayotakiwa kuifanyia kazi taarifa yenyewe haipewi nakala, eti kwa kughafilika? Ni ukweli ofisi ya CAG walighafilikiwa, au jambo hili limesukwa ili kuniaibisha mimi mbele ya Watanzania, Rais aliyeniteua na hasa wapiga kura wangu wa Moshi Vijijini?” alihoji Dkt Chami

 

Anadai Dkt Chami kuwa waliopanga asipate nakala hiyo ya taarifa ya CAG walifanikisha lengo lao kwani katika kujumuisha taarifa ya Kamati yake ya Mahesabu ya Serikali Kuu, Mheshimiwa John Cheyo alimkebehi kwa kumwonyesha kama Waziri asiyejua kufuatilia mambo, ndiyo maana waheshimiwa wabunge walikuwa na nakala za taarifa hiyo na yeye hakuwa nayo. Alisema jambo hilo lilimdhalilisha sana lakini anamuachia Mungu aonaye siri za watu.

 

Dkt Chami alisema tuhuma nyingine zinazoelekezwa kwa Wizara yake ni kwamba makampuni yaliyopewa kazi ya ukaguzi wa magari nje yana uhusiano na watendaji wakuu wa wizara yake.

 

Anakumbusha kuwa ukiondoa makampuni haya makubwa matatu yaliyoanza kazi ya ukaguzi mwaka huu, na ambayo yote ni ya kigeni, makampuni yote matano yanayoendelea na ukaguzi wa magari yalipata tenda hizo mwaka 2007, yeye akiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Hata Naibu Waziri Nyalandu, Katibu Mkuu Mama Mapunjo na Naibu Katibu Mkuu Dkt Mwinjaka walikuwa hawajateuliwa kuiongoza Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2007. Anahoji kuwa kama makampuni hayo ni yale yale, iweje leo Watanzania wafanywe kuamini kwamba viongozi waandamizi wa Wizara ndio wamiliki wasio wa moja kwa moja (indirect owners) wa makampuni hayo?

 

Dkt Chami aliwaomba wale wote wanaomkosoa watambue kwamba yeye anafuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, na kwamba kama asingefuata taratibu hizo, malalamiko juu yake yangekuwa makubwa kuliko yalivyo sasa. Kwa mfano, anadai kuwa kama angemsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS bila kupata barua Ofisi ya Spika na wala kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi katika uamuzi huo, sasa hivi angekuwa anatuhumiwa kwa kuvunja kanuni ya uendeshaji bora wa mashirika ya umma, na wengine wangedai kuwa ana maslahi binafsi.

 

“Jamani Waziri akimfukuza kazi au kumsimamisha Mkurugenzi wa Shirika la Umma bila kufuata sheria na kanuni zilizoainishwa analaumiwa na kutuhumiwa kuwa analinda maslahi binafsi. Waziri mwingine akifuata sheria na kanuni kabla ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lingine la Umma, naye analaumiwa kwa kumlinda mkurugenzi husika na kuonekana kuwa naye ana maslahi binafsi. Kipi ni kipi? Naomba sote tukubali kuwa maadam nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, na kama mawaziri wameapa kuzilinda sheria na kanuni hizo, basi tukubali tu sheria na kanuni vichukue mkondo wake hata pale ambapo tuna hisia kali juu ya Mkurugenzi fulani. Kwa njia hiyo, haki haitakuwa inatendekea tu, bali pia itaonekana kuwa inatendeka,” alizidi kufafanua.

 

 

“Kama Waziri, niliapa kuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  kuilinda katiba ya nchi yetu na kumshauri Mheshimiwa Rais kwa ukweli na uaminifu. Nikikiuka sheria au kanuni za nchi ili nionekane tu kuwa shujaa huku nikimtosa mtu ambaye ametuhumiwa, na tuhuma hizo ziko katika hatua za kuhakikiwa, na zoezi hilo halijakamilika kadiri sheria inavyotaka, nitakuwa navunja kiapo hicho nilichokitoa huku nimeishika Biblia Takatifu,” alimalizia Waziri Chami.

 

7 Comments
  • Namuunga mkono sana Waziri wa Viwanda ba Biashara katika sakata la TBS. Nchi inaendeshwa kwa kuzingatia sheria, na wala sio kukurupuka na kutoa maamuzi kwa kufuata utashi wa kundi fulani wakati mwingine ni sababu ya maslahi binafsi, ebu wabunge wasitumie tofauti/bifu na baadhi ya watendaji na kulitumia bunge kutoa hoja zisizokuwa na msingi. Kile kinachotokea katika Halmashauri za Wilaya ya namna madiwani wanavyowashughulikia watendaji wao baada ya kukosana katika mambo binafsi, sasa ndio kinachotokea katika bunge sasa

  • Watanzania tujifunze kutoa maamuzi MGUMU. ingekuwa busara kama Dr. Chami angemtimua huyo mkurugenzi halafu akaja kuraumiwa kwa hilo. kuliko kusubiri na kisingizia bodi na kibali cha rais. HATUPISHE.

  • ni muongo hata gereji aritudanganya kuwa ziko hongkong kumbe kiboko nyerere anajua zio bongo

  • Mimi ninapenda wanajamii tutafakari ni lini mwana siasa alituhumiwa akakosa maelezo licha ya kuwa utumbo kama alivyobabwaja Dk.Chami.

    Nayaandika haya nikiwa safari kuelekea Lushoto toka Dodoma,jana nimeshinda pale Dodoma hotel ona jinsi vile watu wanavyoishi kama peponi kisa ubunge,uwaziri walipatikanaje! Leo tafiti zinaoenesha uozo mtu anasema “eyes on, hands off“mwalimu mwenzangu mbunge Kasulu mjini amesema ikidhihirika wanyongwe.

    Mbunge kachelewa kujua maisha magumu hivi si uthibitisho wa uozo huu? Ni dhahiri hatuna falsafa ya nchi baada ya NYERERE kutoweka wafanya biashara wameshika nchi,wamehodhi executive,wanatunyonya kweli kweli kila mmoja sasa anabweka tunakufa! Kupona kwenu tutumeni bungeni vijana sisi tusio na elimu ya kuangalizia,eti baba kufa tufutwe machozi kwa kupewa ubunge.

    Tutabweka hadi patachimbika tu.!!!!!!

  • Hivi kuna mtu yeyote hapa aliyesoma hayo maelezo? Hiyo sheria imeanza kufanya kazi Februari 2012, na ilipitishwa na bunge mwaka 2009, chini ya Mary Nagu. Kubadilisha sheria iliyoanza kufanya kazi miezi miwili iliyopita haimake sense! Vile vile, amesema mwenyewe kuwa taarifa zilizotolewa na CAG kwa wabunge hawakutuma wizarani. Je, kama angekuwa anasema uongo, CAG na Kashilila si wangekanusha statement yake? Hawajakanusha! Tatizo tunatafuta excuse ya kulaumu waziri, lakini tusome maelezo aliyotoa. Kama angekuwa anamtetea Ekelege, asingetuma ripoti ya magari kwa CAG, na asingeharakisha uteuzi wa bodi mpya. Watanzania tuna haraka sana ya kukosoa, lakini mmesoma hayo maelezo hapo juu kweli? Ni kheri yeye aliyetoa maelezo ya maana kuliko mawaziri wengine ambao hawajafafanua maelezo yao, au kama Mkullo ambaye mpaka sasa anasema haelewi kwa nini anashutumiwa. CAG nao waseme, hiyo ripoti walimpa nani kwanza? Kama waliwapa wabunge bila kufikisha kwa wizara husika, basi kosa hapo ni la waziri au la CAG? Hebu watanzania someni vizuri bwana. Sioni kosa la kufuata sheria. Kuharakisha mambo just because watanzania wanataka sio uongozi mzuri bali ni uongozi wa ‘Yes man’. Big up kwa maelezo Dr. Chami, tusubiri tuone na ukweli mwingine upi utafichuka. Kama kweli umetenda kosa, sheria itachukua mkondo wake. Kwa sasa, sioni kosa ulilofanya mpaka ujiuzulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *