Vitambulisho vya Taifa kuwanufaisha wananchi wengi

Jamii Africa

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kwa ajili ya kupewa vitambulisho vya Taifa katika maeneo ambako zoezi hilo linaendelea ili kutoa fursa kwa kila mwananchi mwenye sifa kupata kitambulisho.

Usajili unaenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wananchi wanaoomba kupewa vitambulisho vya Taifa chini ya Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya Mitaa na Vijiji kabla ya kutoa nafasi kwa wananchi kuweka mapingamizi ya wazi kwa wale waombaji wanaotiliwa shaka uraia wao kabla ya kuendelea na mchakato wa uzalishaji.

Zoezi hili la usajili kwa ajili ya vitambulisho vya taifa linafanyika baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe kutoa agizo la utekelezaji wa zoezi hili ambalo lilianza rasmi tarehe 14 Septemba 2016 katika ofisi zote za NIDA zikiwemo ofisi za Wilaya zilizoanza usajili na mikoa ya Zanzibar.

Mikoa mingine ni Dar-es-salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma pamoja na Wabunge wa Bunge la Tanzania.

Vitambulisho vilivyotengenezwa hapo awali vilikuwa na makosa hivyo kusababisha kuanzishwa kwa zoezi jipya la usajili japokuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alisema kuwa vitambulisho vya zamani viendelee kutumika.

Image result for vitambulisho vya taifa

Muonekano mpya wa kitambulisho cha taifa

Afisa Usajili wa NIDA mkoa wa Iringa, George Mushi amesema wamejipanga kutoa vitambulisho vya Taifa mapema na kuondoa usumbufu uliojitokeza katika zoezi lililopita ambapo wananchi wengi hawakusajiliwa na kuhakiki taarifa zao.

“Wananchi wanaosajiliwa ni wale wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Zoezi hili linahusisha ujazaji wa fomu za taarifa muhimu za raia, uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya Kielektroniki na uhakiki wa taarifa kwa kila mwombaji.

“Mamlaka ya vitambulisho vya taifa nchini (NIDA) imejipanga kuhakikisha kuwa katika kila hatua vitambulisho vinatolewa mapema iwezekavyo ili kuruhusu kuanza kwa matumizi ya Vitambulisho hivyo katika huduma mbalimbali” amesema Mushi.

Wilaya ya Kilolo ni ya mwisho kukamilisha zoezi hili kwa mkoa wa Iringa na hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kielektroniki. Mbali na Iringa mikoa mingine inayoendelea na zoezi hilo ni ya Kanda ya Ziwa ikiwemo; Geita, Shinyanga, Mwanza, Manyara na Singida.

Wananchi wa mikoa mingine wameshauriwa kuandaa nyaraka muhimu ambazo zitatumika kuhakiki taarifa zao na kuwawezesha kupata vitambulisho hivyo kwa wakati.

Nyaraka muhimu zinazohitajika katika kuthibitisha uraia

  1. Cheti cha kuzaliwa
  2. Cheti za elimu ya msingi,
  3. Pasi ya kusafiria (Pasipoti)
  4. Cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha iv na vi)
  5. leseni ya udereva
  6. Kadi ya bima ya afya
  7. Kadi ya mfuko wa hifadhi ya jamii
  8. Kadi ya mpiga kura
  9. Nambari ya mlipa kodi (Tin. No)
  10. Kitambulisho cha Mzanzibar Mkazi
  11. Barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa

Mabadiliko ya uongozi: NIDA yashindwa kukamilisha ahadi

Zoezi la usajili wa vitambulisho vya Taifa linaloendelea sasa limekuja baada ya zoezi la awali la kutoa vitambulisho kwa kila mwananchi kutotekelezeka.  Mwanzoni mwa mwaka jana NIDA ilikumbwa na kashfa za matumizi mabaya fedha ya bilioni 179.6 ambayo yalipelekea rais John Magufuli kumsimamisha kazi  Mkurugenzi Mkuu wa wakati huo, Dickson Maimu  ili kupisha uchunguzi.

Rais alidai kuwa vitambulisho milioni 2.2 vilivyotolewa vilikuwa na mapungufu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na taarifa  muhimu na sahihi ya mmiliki wa kitambulisho kama vilivyo vitambulisho vya mpiga kura.

Picha hapo chini ni mfano wa vitambulisho milioni 2.2 ambavyo havikuwa na sahihi ya mmiliki:

 

Image result for vitambulisho vya taifa

Muonekano wa zamani wa kitambulisho cha taifa

Aliongeza na kusema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitumia bilioni 70 kutengeneza vitambulisho  milioni 22.7 vya wapiga kura vikiwa na sahihi na  kuhoji iweje NIDA watumie bilioni 179.6 kutengeneza  vitambulisho milioni 2.2 ambavyo havina sahihi ya mmiliki.

Kutokana na kashfa hiyo, Rais John Magufuli alimteua Dkt. Modestus Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi wa NIDA na kumtaka kukamilisha kazi ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa kwa wakati.

Mwezi Machi 2016, Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Dk Modestus Kipilimba aliahidi kukamilisha kazi hiyo ambapo alisema “lengo kubwa la NIDA ni kuongeza ufanisi katika utendaji ili kuhakikisha kwamba ifikapo Desemba, 31 2016 mwaka huu kila mwananchi awe na kitambulisho chake”.

 

Wafanyakazi wa NIDA wafukuzwa kazini

Pamoja na mabadiliko hayo ya uongozi NIDA, Mnamo tarehe 7 Machi 2016, Uongozi wa NIDA uliwaachisha kazi wafanyakazi 597 kwa madai ya ufinyu wa bajeti na ufanisi mdogo katika kuzalisha vitambulisho vya Taifa.

Tangazo hilo lilitolewa na  Kaimu Mkurugenzi wa NIDA, Dk Modestus Kipilimba  ambapo alisema mamlaka hiyo imekuwa na wafanyakazi wengi, lakini kazi iliyokusudiwa ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa haifanyiki kikamilifu.

Dk Kipilimba alisema wafanyakazi 1,399 waliopo NIDA walitakiwa kuzalisha vitambulisho 24,000 kwa siku, lakini waliweza kuzalisha vitambulisho 1,200 kwa siku nchi nzima ambayo ni sawa na asilimia tano ya idadi inayotakiwa.

“Kuanzia leo ninawatangazia watumishi wa mkataba kwamba NIDA hakuna kazi kwa sasa. Tutapitia upya masharti ya mikataba yao na kufuata utaratibu wa kisheria,” alisema Kipilimba.

Siku chache baada ya NIDA kuwaachisha kazi wafanyakazi 597, wafanyakazi hao walimuandikia raisi Magufuli barua ya wazi kumuomba kuingilia kati mgogoro huo wakidai wamefukuzwa kazi kinyume cha sheria.

“Mheshimiwa Rais Tunapenda Umma wa watanzania ujue kuwa usitishwaji wetu wa ajira haukuwa wa halali, kwasababu haukufuata sheria, kanuni na utaratibu za kazi kama inavyoelezwa chini ya kifungu cha sheria ya Ajira na mahusiano ya kazi ya mwaka 2004”. Inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Serikali ilisikia kilio chao na kukubali kuwalipa wafanyakazi hao ambapo ilitoa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya mishahara yao ya miezi minne na mshahara wa mwezi mmoja wa notisi ya kusimamishwa kazi pamoja na malimbikizo ya madeni yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

 

Raisi amteua Bosi mwingine NIDA

Mnamo tarehe 25 Agosti 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alifanya mabadiliko mengine ya uongozi na kumteua Andrew Wilson
kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Kabla ya uteuzi huo Bw. Andrew Wilson Massawe alikuwa Mkurugenzi wa Mifumo ya Kompyuta katika Benki Kuu Tanzania (BOT).  Andrew Wilson Massawe alichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Modestus Kipilimba ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Licha ya serikali kufanya mabadiliko mbalimbali ndani ya NIDA ili kuongeza ufanisi bado mpaka sasa wananchi hawajapata vitambulisho hivyo. Umepita mwaka mmoja sasa tangu wananchi waahidiwe kupata vitambulisho vya taifa lakini hakuna majibu ya uhakika ni lini kila mwananchi mwenye sifa atapata kitambulisho chake.

Faida ya Vitambulisho vya Taifa

Vitambulisho vya Taifa vina umuhimu kwa mtu binafsi na maendeleo ya Taifa. Tanzania ikifanikiwa kutoa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kutakuwa na faida mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Vitasaidia kuongeza wigo wa mapato ya Serikali na kumtambua mhusika kirahisi anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.

Vitarahisisha kuwatambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye benki na asasi mbalimbali za kifedha nchini.

Pia vitasaidia kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari la kumbukumbu la kielektroniki, na vitawezesha kumtambua mtu anapofanya biashara au shughuli nyengine kwa kutumia majina tofauti.

Mbali na hayo vitasaidia kuhakikisha kuwa kila mtu anapata stahili zake za jamii. Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia wa Tanzania anastahili kupata kirahisi kwani kupitia kitambulisho mtu atatambulika kirahisi.

Utendaji kazi Serikalini utaimarika kwa kuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao, hasa pale wanapostaafu.

Vitasaidia kuondoa watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara ‘payroll’ ya Serikali ambapo jambo hili limesumbua sana serikali ya awamu ya 5 na Raisi aliliwekea mkazo sana.

Pia vitarahisisha ufanyikaji wa zoezi la  kuhesabu watu (sensa) na kurahisisha zoezi la kuhuisha daftari la wapiga kura, ambapo kwa sasa hufanyika mara mbili kabla ya uchaguzi mkuu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *