Dk. Chegeni atishia kuishtaki DIRA ya Mtanzania

Jamii Africa

dira-ya-mtanzaniaALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Busega Wilayani Magu mkoani Mwanza, Dk. Raphael Masunga Chegeni (CCM), ametoa muda wa siku saba kwa gazeti la DIRA ya Mtanzania kumuomba radhi, kutokana na kile alichodai kuandika habari zisizo na ukweli dhidi yake,  la sivyo atakwenda mahakamani kudai haki yake.

Dk. Chegeni ambaye pia ni Mkurugenzi wa hoteli ya Isamilo Lodge ya Jijini Mwanza, aliwaambia leo waandishi wa habari Jijini hapa kwamba, Desemba 5 mwaka huu, gazeti hilo lilichapisha habari ambayo yeye aliiita ni ya uongo, na kwamba ililenga kumchafulia heshima yake ndani na nje ya chama chake cha CCM na jamii kwa ujumla.

Alisema Mhariri wa gazeti hilo pamoja na mwandishi wa habari hiyo iliyoandikwa ukurasa wa mbele, hawakumtendea haki kisheria, kwani hawakumpa fursa ya kuzungumzia tuhuma hizo, hivyo anaamini kwamba habari hiyo imeandikwa kwa malengo ya kisiasa na kutaka kumpaka matope mbele ya jamii ya Kitanzania na nje ya nchi.

“Desemba 5 mwaka huu, gazeti la DIRA ya Mtanzania lilichapisha habari za uongo dhidi yangu. Wameniandika eti nimewahi kuiba sh. milioni 3 katika Idara ya Ujenzi na Ukarabati wakati huo (TRM), huko Bukoba nikaachishwa kazi, eti nimekisaliti chama changu cha CCM. Taarifa hiyo naikanusha, maana imejaa uongo mtupu.

“Kwanza hawakunihoji kupata maelezo yangu katika hili. Kwa maana hiyo, natoa muda wa siku saba waniombe radhi kwa kukanusha habari yao hiyo ukurasa wa mbele, vinginevyo nitawapeleka mahakamani”, alisema Dk. Chegeni kwa msisitizo mkubwa.

Dk. Chegeni alieleza kushangazwa na taarifa hizo alizodai zimeandaliwa na wabaya wake wa kisiasa, na kusema kamwe hajawahi kukisaliti chama chake wala kuiba fedha zozote katika TRM, na kwamba hajataifisha wala kujimilikisha nyumba yoyote, bali anazo nyumba zaidi ya tano huko Bwiru.

Juzi gazeti hilo la DIRA ya Mtanzania liliandika habari iliyodai kwamba mwaka 2009 Dk. Chegeni alikisaliti chama chake cha CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwaunga mkono wapinzani, alimuwezesha Diwani mmoja wa CUF kuiangusha CCM, kagushi vyeti vya shahada ya Falsafa (PhD), Kaiba sh. milioni 3 TRM  na amejimilikisha nyumba moja huko Bwiru.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

2 Comments
  • Namshauri Dk. Raphael Masunga Chegeni (CCM),kwenda mahakamani kama hataombwa msamaha ili mbivu na mbichi ziwekwe wazi,ila ila ajue kama wameandika na wanaushahidi itatusaidia kumfunga Dkt huyu wa ccm na itakuwa fundisho kwa wenzake mafisadi kama Lowasa,Rostam,Chenge,Karamagi,Mkapa,kikwete…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *