Dodoma: Hali bado tete, wajawazito wasafiri zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za uzazi

Jamii Africa

HUDUMA ya afya katika Kata ya Malolo, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma bado zina changamoto kubwa ambapo mpaka sasa wajawazito wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za uzazi, FikraPevu inaripoti.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, wajawazito hao wanatumia hospitali za St. Kizito mjini Mikumi mkoani Morogoro au Hospitali ya Ilula wilayani Kilolo katika mkoa wa Iringa ambako kuna huduma za uhakika za kliniki na uzazi.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Bosco Mwaluga, ameambia FikraPevu wiki hii kwamba, huduma za afya, hasa ya uzazi hazipatikani katika kijiji cha Malolo kutokana na sababu mbalimbali, kubwa zaidi ikiwa ni ukosefu wa watumishi katika zahanati ya kijiji.

Hospitali kubwa ambayo ni ya Wilaya iko umbali wa kilometa 155 kutoka Mpwapwa mjini na haifikiki kwa urahisi kwa vile hakuna usafiri kutokana na miundombinu mibovu ya barabara, hali inayowalazimu wajawazito pamoja na wagonjwa wengine kusafiri kwenda Mikumi au Ilula ambako ‘ni karibu’ na kuna huduma za uhakika.

“Kwa huduma za kliniki, wanatumia zahanati ya Al Jazeera iliyoko Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo katika Mkoa wa Iringa, umbali wa takriban kilometa 25 kutoka hapa kijijini,” alisema Mwaluga.

Zahanati hiyo ina mganga mmoja tu, tena mwanamume, hali ambayo kwa mujibu wa Mwaluga, imekuwa changamoto kwa akinamama wajawazito ambao wanashindwa kupata huduma za uzazi, hususan za kliniki.

Hata hivyo, licha ya kutokuwa na huduma za uhakika za uzazi, likiwemo suala la kujifungua, baadhi ya wajawazito wanazuiwa na waume zao kuhudumiwa kwenye zahanati hiyo kwa kile wanachosema hawataki wake zao ‘wakapekuliwe’ na mwanamume mwenzao.

Suala la utumiaji wa njia za uzazi wa mpango nalo limekuwa na mtazamo hasi kwa jamii ambapo kwa mujibu wa Mwaluga, ni wanajamii wachache wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Mwaluga alisema kwamba, kukosekana kwa watumishi wa sekta ya afya kwenye zahanati hiyo kumeendelea kuwa changamoto kubwa, ambapo licha ya kutokuwepo kwa mtumishi wa kike, lakini huyo mmoja tu aliyepo hawezi kumudu kazi zote na mara nyingi anaposafiri huwa hakuna huduma zinazotolewa.

“Hivi ninavyozungumza na wewe ndiyo zahanati imefunguliwa leo hii baada ya kufungwa kwa wiki nzima kutokana na bwana mganga kusafiri kwenda mjini Mpwapwa,” alisema.

FikraPevu ilimtafuta kwa nia ya simu bwana mganga huyo, Elias Mlwande, ili kuzungumzia changamoto mbalimbali, lakini hakuweza kupatikana.

Takwimu rasimu za watumishi wa idara ya afya zinaonyesha kwamba, hadi Desemba 2014, kulikuwa na watumishi 69,864 nchi nzima.

Mkoa wa Dodoma wenye watu 2,187,955 una jumla ya watumishi wa afya 2,861.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *