Dodoma: Licha ya kuwepo kwa mito, ndoo moja ya maji yauzwa Shs. 700

Jamii Africa

MANENO Chegula (42) anaonekana akihangaika kukokota baiskeli yake ili kuvuka Mto Sasima, jasho linamtoka, huku akiwa amebeba madumu matano yenye maji ili kupeleka katika Kijiji cha Malolo, wilayani Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma, ambako ndiko anakoishi, umbali wa kilometa mbili kutoka hapo mtoni.

Lakini maji hayo ameyachota katika Mto Chabi uliopo ng’ambo ya pili ya Mto Sasima, yapata kilometa tatu kutoka kijijini.

Japokuwa Mto Sasima unatiririka maji, lakini Chegula anasema maji hayo hayafai kwa kunywa kwa vile yana tope jingi.

“Nakwenda kuuza kijijini, ndoo moja Shs. 700, kwa hiyo hapa nitapata Shs. 3,500,” anasema Chegula na kuongeza kwamba hiyo ilikuwa safari yake pili na kwa kutwa hufanya safari tatu.

Kwa Chegula, biashara ya kuuza maji imekuwa chanzo cha kipato, lakini kwa wakazi wa Malolo hiyo ni gharama nyingine ya maisha ambayo wanalazimika kuikabili kutokana na uhaba wa maji ya kunywa.

“Siyo haba, napata fedha ya kutosha kwa matumizi ya familia, tatizo la kijiji chetu ni kukosekana kwa miundombinu, hususan visima vya maji baridi ambayo yangefaa kwa kunywa, kuna maji pale kijijini, lakini ya chumvi kiasi kwamba hata kupikia maharage ni shida, achilia mbali kufulia nguo,” anasema Chegula akiieleza FikraPevu ambayo ilikutana naye wakati akivuka Mto Sasima.

Kwa Kijiji cha Malolo chenye vyanzo vya kutosha vya maji, ikiwemo mito miwili ya uhakika ya Sasima na Chabi iliyoko umbali wa kilometa tatu, kununua ndoo moja kwa Shs. 700 linaonekana kama suala la ajabu.

FikraPevu ilijionea yenyewe changamoto ya njia za kupita hadi kuufikia Mto Chabi wenye maji safi ni kubwa, kwani huwalazimu kupita kwenye mashamba ya mpunga na kuvuka Mto Sasima kwenda na kurudi, jambo ambalo pia ni la hatari kiusalama.

Akinamama, ambao ndio waathirika wakubwa na tatizo la ukosefu wa maji, wanapata shida zaidi pindi inapotokea familia ikakosa fedha za kununulia ndoo za maji kwa matumizi ya nyumbani, ambalo hulazimika kutembea umbali huo wa jumla ya kilometa sita kwenda na kurudi ili kupata huduma hiyo muhimu, huku wakipita katika mazingira hayo hatarishi.

Katika kipindi hiki cha masika, huomba Mungu anyeshe mvua ili waweze kukinga kwenye paa, lakini inapotokea mvua hazijanyesha, hali inawawia vigumu zaidi.

Suzana Magawa (35), mkazi wa Kijiji cha Malolo, ameieleza FikraPevu kwamba, ukosefu wa maji safi na salama kijijini hapo ni mzigo mzito kwa mwanamke na unawaweka katika mazingira hatarishi.

“Siyo wote ambao tunaweza kumudu kununua maji, hasa ya kunywa, hivyo tunalazimika kutembea umbali huu na kwa mazingira haya hatarishi, tunaweza hata kubakwa, kudhalishwa ama kutekwa,” anasema na kuongeza kwamba, hali hiyo inawafanya wasichana wadogo kupata mimba za utotoni bila kutarajia.

Anasema, japokuwa kijiji hicho kina neema kubwa ya chakula kutokana na shughuli za kilimo zinazofanyika majira yote ya mwaka huku wakitegemea umwagiliaji, lakini wananchi wanajikuta wangali maskini kwa kuwa wanalazimika kuuza mazao yao ili kupata huduma muhimu kama maji kwa gharama kubwa.

Suzana anasema, ahadi nyingi za wanasiasa zinazotolewa nyakati za kampeni hazitekelezwi na kwamba matatizo yao yamekuwa kama mtaji wa kuombea kura.

“Miaka nenda-rudi tunaahidiwa tutapatiwa maji ya bomba, lakini watoto wanazaliwa na kuzeeka hakuna kinachofanyika, hapa tuna vyanzo vya kutosha vya maji safi, wanashindwaje kutuchimbia visima virefu vya maji baridi?” anahoji.

Zuberi Said Mlinji ambaye ni Ofisa Ugani wa Kata ya Malolo, anakiri kwamba tatizo la maji ni changamoto kubwa inayowatesa wakazi wa kata hiyo.

“Kweli kuna vyanzo vya kutosha hapa, maji yapo mengi na hayapatikani mbali, lakini visima vilivyochimbwa pale kijijini ni vya maji chumvi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu,” anasema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Malolo, Bosco Paulo Mwaluga, anasema changamoto ya ukosefu wa maji salama ni ya muda mrefu lakini haijapatiwa ufumbuzi kutokana na ukosefu wa bajeti.

Mwaluga, ambaye ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo yenye vijiji vya Idodoma, Nzugilo na Malolo yenyewe, anasema tatizo la maji salama ni la kata nzima kwani hakuna visima vya kutosha.

Anakiri kwamba, tatizo hilo linakwamisha maendeleo ya wananchi, kwani wanalazimika kutumia gharama kubwa kupata huduma hiyo muhimu na kupunguza mapato ya familia.

“Shs. 700 kwa ndoo moja ya maji ni fedha nyingi sana, pengine kwa kima cha chini mwananchi analazimika kutumia Shs. 6,300 kwa mwezi ili apate wastani wan doo tatu za maji safi kila siku,” anasema.

Aidha, anasema visima vilivyopo kijijini hapo ni vifupi na vya maji chumbi ambavyo vilichimbwa miaka mingi, hivyo jitihada zinafanywa na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha kero hiyo inatatuliwa.

“Kuna mwekezaji mmoja amejitokeza, ni mkulima ambaye anatokea huko Ruaha Mbuyuni mkoani Iringa, ambaye amesema yuko tayari kuchimba kisima kirefu cha maji baridi na atasambaza mfumo wa mabomba kijijini, tumemkubalia kwa sababu tunachotaka huduma bora kwa jamii zipatikane,” anasema.

Diwani wa Kata ya Malolo iliyoko Jimbo la Kibakwe, Maulid Mangile, hakuweza kupatikana kuzungumzia changamoto hiyo ya wapigakura wake.

Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa mingi ambayo tatizo la uhaba wa maji ni sugu kwa muda mrefu kutokana na hali ya ukame na nusu jangwa, lakini hata palipo na vyanzo vya kutosha vya maji, hakuna jitihada za makusudi ambazo zimefanyika kuhakikisha serikali inajenga miundombinu ya uhakika kuwapatia wananchi huduma hiyo muhimu.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, katika maeneo mengi ya mkoa huo, wananchi wanatumia maji ya visima na mabwawa yasiyo safi wala salama, huku maeneo mengine wakichangia pamoja na mifugo, hali inayowafanya wawe hatarini kupata magonjwa wa milipuko yanayosababishwa na uchafu wa maji.

Upatikanaji wa maji safi na salama ni lengo namba sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) kuelekea mwaka 2030, lakini licha ya msisitizo uliopo, maeneo mengi, hasa ya vijijini, bado yana changamoto kubwa kuyafikia malengo hayo.

Upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na nishati ya uhakika ni haki za msingi za binadamu ambazo wananchi wengi wa mataifa yanayoendelea, ikiwemo Tanzania, wananyimwa.

Wakati wa Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nchi Zinazoendelea (Least Developed Countries – LDC-IV) uliofanyika jijini Istanbul, Uturuki ilielezwa kwamba karibu watu bilioni 2.5 duniani walikuwa wakishindwa kupata haki zao za msingi kama maji safi na salama na umeme.

Mwanaharakati Maria Lourdes Tabios Nuera, kutoka asasi ya Jubilee South-Asia/Pacific Movement on Debt and Development, alisema kwamba upatikanaji wa maji safi na salama ni wa lazima kwa kila mtu na huduma hiyo haipaswi kutolewa kwa malipo.

"Vyanzo vya maji lazima vitumiwe kwa usawa na wote na vinapaswa kulindwa na kutunzwa kwa uhakika,  kidemokrasia na kwa nia ya kuviendeleza. Udhibiti wa vyanzo vya maji lazima uwe wa umma na usibinafsishwe," alisema Nuera.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba kwa zaidi ya miongo miwili sasa kumekuwepo na harakati za kubinafsisha maji, huku mashirika machache yanayojihusisha na maji yakimiliki vyanzo na huduma za maji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *