Siku chache zilizopita Rais John Magufuli alipiga marufuku michango ya aina yoyote katika shule za msingi na sekondari nchini kwa madai kuwa serikali inatoa elimu bila malipo, lakini agizo hilo limeendelea kuchukua sura mpya juu ya mustakabali wa elimu nchini.
Rais alitoa agizo hilo alipokutana na mawaziri wa elimu na TAMISEMI ambapo alisema amepokea malalamiko kuwa walimu wanawatoza wazazi michango kwa ajili ya kufidia ufinyu wa ruzuku inayotolewa na serikali.
Kauli hiyo iliibua mjadala ambapo kumezuka makundi mawili ya watu ambao wanaunga mkono na wale wanaopinga kauli ya Rais.
Ili kuondoa utata huo, Waziri wa Elimu, sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa bungeni wiki iliyoipita alisema michango haijakatazwa kabisa lakini kama mzazi ataamua kutoa kwa hiari yake mwenyewe hazuiliwi.
Kauli ya Prof. Ndalichako ilijikita kwenye Waraka namba 3 wa mwaka 2016 ambao umeainisha majukumu ya wadau mbalimbali wakiwemo wazazi ambao wana wajibu wa kuchangia sehemu ndogo ya michango kwenye shule za msingi.
Ufafanuzi wa waziri wa elimu ulizidisha mkanganyiko zaidi kwa wananchi kuhusu sera ya elimu bure hasa wazazi kuchangia sehemu ndogo ya gharama za elimu shuleni.
Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu (2017) juu Matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Ada kwa Elimumsingi nchini Tanzania umebaini kuwa uelewa wa wananchi kuhusu sera ya Elimu Bure bado hauridhishi na ikiwa hali hiyo haitatatuliwa ubora wa elimu utashuka kila mwaka.
Utafiti umeonesha kuwa kulikuwa na mkanganyiko na tafsiri potofu kuhusu sera hii miongoni mwa wadau. Kwa mfano, karibu asilimia 45 ya walimu wakuu walieleza kwamba sera ya elimu bila ada ina maana gharama zote za Elimumsingi zinalipwa na serikali. Wengine 23% walitafsiri sera ya Elimumsingi bila ada kama elimu inayotolewa bila kulipa ada ya shule pekee.
Lakini 32% walisema elimu bila ada ni ile inayoendeshwa kwa wazazi kuchangia sehemu ndogo ya gharama. Idadi kubwa ya wazazi (51.3%) walisema sera ya Elimumsingi bila ada ina maana ya kuwaondolea gharama zote wazazi zinazohusiana na watoto wao kusoma kwenye shule za umma.
Mkanganyiko huo unatokana na kueleweka vibaya kwa waraka namba 5 wa mwaka 2015 kuhusiana na nani mwenye wajibu wa kugharamia elimu kwasababu wazazi walionekana kujitoa katika kugharamia chochote kinachohusiana na shule.
Matokeo yake, serikali ilitoa Waraka namba 6 wa mwaka 2015, ambao baadaye ulifuatiwa na Waraka namba 3 wa 2016, ambao uliweka wazi zaidi majukumu ya wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi.
Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015
Pamoja na majukumu mengine, waraka uliwataka wazazi kubeba majukumu ya kugharamia masuala ya sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia kama vile madaftari na kalamu/penseli, na gharama za chakula kwa wanafunzi wa kutwa.
Madhumuni ya wazazi kuchangia gharama kidogo ni kwasababu ruzuku inayotolewa na serikali kwa wanafunzi haitoshelezi mahitaji yote ya wanafunzi na shule. Utafiti huo umegundua kuwa ruzuku ya wanafunzi iliyopokelewa na shule ilitofautiana kulingana na makundi ya shule.
Kwa wastani, wakati shule za sekondari zilipata 13% zaidi ya kiasi tarajiwa cha Sh. 12,500 katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2016, shule za msingi zilipokea 7% pungufu ya kiasi kinachotarajiwa cha Sh.3,000.
Kwa muktadha huo, wazazi wanabaki kwenye mkanganyiko mkubwa kwamba wafuate kauli za viongozi wa serikali au watekeleze waraka Namba 3 wa mwaka 2016?
Mapendekezo ya wazazi
Inaelezwa kuwa michango ya wazazi ya kugharamia masuala yanayohusiana na shule bado ni muhimu. Tofauti na utata na tafsiri potofu ya Waraka namba 5 wa Serikali wa 2015, Waraka namba 3 wa Serikali 2016 umeweka bayana majukumu ya serikali, wazazi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, utayari wa wazazi kuchangia unaweza kutafsiriwa kama fursa kwa serikali kuhamasisha wazazi kuisadia serikali kugharamia elimu, ambayo inaweza kusaidia pia kutatua matatizo yanayotokana na elimu bila ada.
Mbali na kusaidia matumizi ya serikali kwenye elimu, michango ya wazazi pia inakuza hisia ya umiliki wa shule, kitu ambacho ni muhimu sana kwenye kuboresha ushiriki wa wazazi, uboreshaji wa miundombinu ya shule na hatimaye kuboresha kiwango cha ufaulu wa shule.
Suluhisho
Dk Richard Shukia, mwandishi wa ripoti ya utafiti wa HakiElimu ameshauri kuwa “kuna haja ya serikali kushirikiana na wadau wengine kuandaa vikao na wadau muhimu wa elimu ili kufafanua na kuwaelewesha zaidi kuhusu sera hii. Hili linaweza kufanyika kwa mbinu isiyo na gharama ya ngazi moja kuwaelimisha ngazi ya chini yake.
“Serikali inapaswa kuhakikisha ruzuku inazifikia shule kwa wakati na kwa kiasi sahihi kwa mujibu wa sera ya “elimu bila ada. “ Mbali na hilo, ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kupitia upya na kurekebisha kiwango cha ruzuku ya kila mwanafunzi kinachopokelewa shuleni kwa mwaka, kwasababu kiasi kinachopokelewa ni kidogo mno na hakina uwezo wa kulipia mahitaji ya shule”.