Wakati serikali ya Tanzania ikitekeleza sera ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, serikali ya Morocco inakusudia kupeleka mswada wa sheria bungeni ili kufikia tamati ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi nchini humo.
Kutokana na uamuzi huo wa serikali ya Morocco ambayo inaongozwa na Mfalme Mohammed VI imeibua hasira za wanafunzi, wasomi na wadau wa elimu nchini humo ambapo wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani wameungana kuupinga mswada huo ambao unalenga kuongeza gharama za elimu nchini humo.
Mswada huo utaifanya elimu ya msingi kuendelea kuwa bure kwa Wamorocco wote lakini ada itakuwa inalipwa kwa wanafunzi wa sekondari na elimu ya juu ambao wanatoka kwenye familia tajiri. Wanaopinga mswada huo wameonya kuwa sheria hiyo ikipita itaathiri ubora wa elimu na mfumo mzima jamii.
Abdul Razzaq el-Idrissi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Taifa la Elimu akihojiwa na vyombo vya habari amesema sheria hiyo itasababisha, Wanafunzi kuacha shule kwasababu ya familia zao kushindwa kulipa ada.
Wanafunzi wengi wa Morocco wanalalamika juu ya gharama kubwa za elimu licha ya serikali kutoa elimu bure na serikali itoe zaidi ruzuku kwa wanafunzi ili kufidia gharama zilizopo.
“Ninasoma katika miji tofauti, mbali sana na nyumbani; silipi gharama za shule lakini ninalipa gharama zingine za nyumba, chakula, usafiri na mengine”, amesema Intissar Louah, mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu.
Mazingira ya elimu ya Morocco na Tanzania hayatofautiani, licha ya serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuanza kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne bado kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wazazi kutozwa michango mbalimbali ikiwemo fedha ya karatasi za mitihani, ulinzi wa shule na masomo ya jioni.
Kwa kutambua mzigo wanaobebeshwa wazazi, Rais Magufuli amepiga michango ya aina yoyote shuleni na gharama zote za elimu zitalipwa na serikali. Wadau wa elimu nchini wametilia shaka agizo hilo ikizingatiwa kuwa ruzuku inayopelekwa katika shule haitoshelezi mahitaji yote ya kitaaluma.
Shule hulazimika kukaa na wazazi na kukubaliana kutoa kiasi fulani cha fedha ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
Godwin Mwambene, ambaye ana mtoto aliyemaliza darasa la saba na kupangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Makumbusho aliambiwa na uongozi wa shule kuwa anatakiwa kulipa sh.65,000 ndipo mtoto wake aruhusiwe kuanza masomo.
“Nilienda kuchukua fomu ya mwanangu shuleni lakini gharama za kuanza shule ni 65,000 ambazo ni michango mbalimbali ya shule”, ameeleza Godwin.
Licha ya serikali kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari bado ubora wa elimu inayotolewa nchini inashuka kila mwaka.