FOLENI za Jiji la Dar es Salaam zimenifanya nijifunze mambo mengi sana ya kijamii. Kwa jinsi zilivyo ndefu, hususan hii ya Barabara ya Mandela kama unatoka Ubungo, unaweza kutumia hata saa tatu kutoka Tabata Matumbi hadi kuvuka taa za Tazara.
Ni wakati huo – uwe kwenye daladala au gari binafsi – utaona akinamama wengi wakiwa na mabeseni vichwani mwao. Wanauza vipande vya nazi na mihogo.
Naam. Kipande kidogo cha muhogo chenye urefu usiozidi inchi mbili kinauzwa kwa shilingi 200, na watu wanaichangamkia kweli kweli, pamoja na vipande vya nazi.
Hii ni kwa sababu ‘wameambiwa’ mihogo inaongeza ‘heshima ya ndoa’. Si unajua Watanzania wakielezwa tu kitu fulani kinarudisha hesima ya ndoa wanavyochangamkia.
Lakini hiyo ni faida mojawapo tu, na huenda unafahamu faida tatu au nne tu za muhogo ambazo ni kuutafuna mbichi, kuuchemsha au kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama kuni.
Inawezekana hujui kama maganda ya mihogo baada ya kumenywa ni chakula bora cha mifugo yakikaushwa au mabichi.
Siyo ajabu pia hujui kwamba muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.
Muhogo ni zao linalochukuliwa na wengi kama la ziada hasa kwenye ukame, lakini wengi hulifanya kama mlo wa hamu bila kutambua kwamba zao hilo lina manufaa makubwa kwa lishe na kibiashara.
Wengi wanauchukulia muhogo kama chakula cha maskini, hawa wale wanaojitiahidi kulima zao hilo, huyapa kipaumbele mazao mengine kuliko muhogo.
Lakini muhogo ni zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha jamii na baa la njaa huku katika baadhi ya mataifa likitumika kama chanzo cha nishati ili kukabiliana na bei ya mafuta na nishati nyinginezo.
Baa la njaa ni tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwa miongoni mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima muhogo, bado wanalipuuza zao hilo na kuliona kama zao fulani la mizizi tu.
FikraPevu inafahamu kuwa, Umoja wa Mataifa ulipitisha Malendo Endelevu 17 ya Dunia, yaani SDGs, mnamo Septemba 22, 2015, ambapo malengo mawili ya kwanza ni kutokomeza umaskini uliokithiri pamoja na kukabiliana na baa la njaa na kuwa na uhakika wa chakula.
Ikumbukwe kwamba, takribani watu milioni 8 bado wanaishi kwenye dimbwi la umasikini; lishe duni, njaa, kutegemea kilimo cha mvua huku wakitegemewa kuilisha dunia kwa asilimia 80.
FikraPevu inaamini kwamba, malengo mawili ya kwanza yakitekelezwa barabara yanaweza kutoa taswira chanya pia katika kuyatekeleza na kuyatimiza malengo mengine.
Kilimo endelevu na chenye tija, kikiwemo cha zao la muhogo, kitainusuru jamii hasa katika kipindi hiki ambapo dunia imekumbwa na tatizo la mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Katika mikoa kama Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi inalima kwa wingi muhogo, chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.
Licha ya kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta mlo wa siku hiyo umetokana na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana kuni zilizopikia ni matawi ya muhogo, ugali wa muhogo na mboga ni kisamvu cha muhogo!
Lakini utashangaa, eti wakulima wengi katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara wanakula ugali wa muhogo pale wanapokosa unga wa mahindi, ambapo wanaokula ugali huo wa muhogo (Wazaramo wanasema ‘bada’ na Wamakua wanauita ‘matamba’) huonekana maskini wa kutupa.
Leo hii wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya kustahimili ukame, bado wengi wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa muhogo unatoa bidhaa nyingi zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao hilo na kulima kibiashara.
Inafurahisha sana siku hizi kuona watu wengi wakikimbilia ugali wa muhogo hata hotelini, lakini hiyo bado haijatosha kulirasimisha zao hilo ili liwe na tija kubwa.
Mkate uliotengenezwa kwa unga wa muhogo
Kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula nje.
Zao la muhogo ni zaidi ya linavyofikiriwa kwa sababu licha ya faida hizo chache, lakini pia linazalisha bidhaa zaidi ya 300, zikiwemo kuzalisha unga pamoja na chips, unga ambao unaweza kutengeneza bidhaa lukuki zenye ubora kama chapatti, maandazi, skonzi, biskuti, tambi, keki na nyinginezo nyingi.
FikraPevu inafahamu kwamba, faida za muhogo ni nyingi kama zilivyoelezwa hapo juu, lakini kwa msisitizo ni kwamba, unga wake hutumika kutengeneza vyakula mbalimbali, baadhi ni uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, mandazi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, kuni, mboga, huksi pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Mazao yanayopatikana katika mzizi wenyewe, miti na majani huweza kuzalisha bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta, kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga (starch) hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup).
Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalisha takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.
FikraPevu inatambua kwamba, Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Congo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar.
Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa Kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania.
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi sana na magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.