Siku chache baada ya Mbunge wa Tabora mjini Bw. Aden Rage kujikuta matatani na vyombo vya usalama nchini baada ya kupanda jukwaani akiwa na silaha ya bastola sakata jingine lenye kumhusisha limeibuka tena huko Iguunga ambapo gari dogo aina ya Toyota Noah T.836 AZP ya Kituo cha Redio cha Voice Of Tabora (VOT) limeuparamia mkutano wa kampeni za Chama cha Wananchi (CUF) mjini hapa.
Tukio hilo la aina yake ambalo huenda lingesababisha msiba mwingine mkubwa kwa taifa, lilitokea juzi eneo la Ziba barabarani wilayani Igunga mkoani Tabora.Mamia ya watu waliojitokeza kusikiliza mkutano wa kampeni uliohutibiwa na Mbunge wa CUF Jimbo la Mkanyageni Pemba Mohamed Habib Mnyaa walipigwa butwaa baada ya gari hilo kuparamia mkutano likiwa katika mwendo kasi na kupita katikati ya watu.
Kitendo cha gari hilo kupita katikati ya watu kilisababisha wananchi katika eneo hilo kukimbia hovyo huku wengine wakikanyagana na kupoteza watoto kwa muda mchache.Gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Mbwana Shaa lililizunguka gari la muzuki la CUF FUSO kwa kuingilia upande wa Kaskazini kisha kupita upande wa Magharibi na kuelekea upande wa Kusini kabla ya kusimama likiwa limeelekea upande wa Mashariki.
Mpaka gari hilo linafanikiwa kusimama pamoja na watu kukimbia huku na huko wakijitahidi kuokoa roho zao hakuna mtu yeyote aliyekanyagwa wala kujeruhiwa zaidi ya baiskeli moja kugongwa.Hata hivyo msaada mkubwa wa askari polisi waliokuwa wakilinda mkutano huo wa kampeni walikuwa msaada mkubwa mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Askari hao zaidi ya saba wakiongozwa na Inspekta Msaidizi Aloyce walikwenda eneo iliposimama gari na kumshusha dereva na watu wengine ndani ya gari, pamoja na kushushwa kwa dereva huyo pia alijikuta akipokea kichapo cha nguvu kutoka kwa askari polisi hao na kumpakia kwenye gari na kumpeleka kituo cha polisi Igunga.
Baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo walisikika wakidai kuwa kama si kuwapo kwa polisi katika mkutano huo wangehakikisha gari hilo wanalichoma moto na kuwateketeza wahusika wote.Mwandishi wa Habari hizi aliyekuwapo kwenye mkutano huo alilishuhudia gari hilo likiwa katika mwendo wa kasi likitokea upande wa Kusini mwa mji wa Ziba iliko Hospitali ya Nkinga.
Kutokana na mwendo kasi dereva huyo alishindwa kupunguza mwendo ili kujiandaa kuingia barabara kuu ya lami inayoelekea mjini Igunga takribani kilomita 35 hivi, ambapo badalaya kuelekea upande wa Mashariki aliamua kuliingiza upande wa Kaskazini Magharibi kulipokuwa na watu.Hata hivyo kabla ya kutokea kwa tukio hilo takribani dakika saba au tisa msafara wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Philip Mangula ulikuwa umepita barabara hiyo ya vumbi inayotokea Nkinga.
Kwa upande wake Mbunge Mnyaa akizungumzia tukio hilo lililotokea akiwa amesimama katikati ya mkutano huo alimshukuru Mungu kwa gari hilo kutoelekea upande aliosimama.“Ni tukio linaloshangaza na kusikitisha sana, siamini kama ilikuwa ni makusudi au vipi, lakini ninachoweza kusema huenda ni uzembe wa dereva kwani walikuwa katika mwendo kasi mpaka anazunguka gari letu la muziki.
“Nimesikia watu wanadai pale kuwa alikuwa ananuka pombe sasa huenda amezidisha ulevi na akashindwa kuwa makini katika kuliongoza gari lake,” alisema Mbunge Mnyaa na kuongeza “Lakini pia siwezi kujua kama mpango wao ulikuwa ni wakuvuruga mkutano wetu au laa! Hiki ni kipindi cha kampeni kama mnavyojua yote yanawezekana, lakini tuna mwachia Mwenyezi Mungu na vyombo vya dola,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Dodoma Moza Said alisema kwa ujumla tukio hilo lilimshtua na kusababisha shinikizo la damu (PB) kuanza kumsumbua.“Unajua nilikuwa nimekaa meza ya mbele kwenye mkutano gafla nikaona gari inaparamia mkutano wetu kwa kasi bahati nzuri ikakata kona kuelekea upande mwingine. Imenishtua sana ukichukulia juzi tu nimetoka kupata ajali ya gari,” alisema Moza.
Mkazi mmoja wa Ziba Joseph Maziku (45) alisema, kama tukio hilo lingetokea wakati tayari mkutano huo ukiwa umefungwa basi huenda vifo vya watu vingekuwa vingi zaidi.“Namshukuru Mungu watu walikuwa bado wamekaa kwa utulivu tena maeneo ya pembeni na kuacha eneo la wazi ilipokuwa gari ya muziki. Ndio maana hakuna maafa yaliyotokea ila kama mkutano ungekuwa umemalizika leo tungekuwa na msiba wa kitaifa hapa Ziba,” alisema Maziku.
Picha za Tukio
Habari na Eliya Mbonea