MKOA wa Geita ni maarufu kwa utajiri wa madini ya dhahabu iliyotapakaa katika eneo mbalimbali mkoani humo, hasa maeneo maarufu la Nyarugusu.
Katika miaka ya themanini na mwishoni mwa tisini, ilikuwa ni ufahari kwa kila kijana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria (Mara, Mwanza, Tabora na Shinyanga) kwenda kutafuta maisha kwa kuchimba madini katika migodi ya madini ya dhahabu; Nyamongo Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara au Nyarugusu Mkoa wa Geita.
Hata hivyo, kwa Mzee Emmanuel Simon (58), mkazi wa Kijiji cha Igate pamoja na wakazi wa Tarafa ya Bungando Wilaya ya Geita, hadithi hiyo imebadilika.
“Kwetu sisi wakazi wa Igate, utajiri wa Geita ni zaidi ya madini ya dhahabu kwa sababu tumevumbua madini mengine yanayopandwa, kuota na kuvunwa baada ya miezi kumi na nane,” anaanza kusema Mzee Simon
Mzee Simon, mtumishi mstaafu wa serikali. Anataja zao la nanasi kuwa ndiyo dhahabu mpya iliyogundulika Geita.
“Hatuna tena hofu ya mdororo wa kiuchumi kutokana na kushuka au kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la Kimataifa. Hii ni kwa sababu tuna uhakika wa kuvuna dhahabu yetu mpya, ambayo ni nanasi,” anatamba mkulima huyo
Anasema baada ya kuingia kwa makampuni makubwa ya uwekezaji, hali ya maisha ya wakazi wengi wa Kata ya Igate, tarafa ya Bugando, Wilaya na Mkoa wa Geita kwa ujumla iliyumba kutokana na maeneo ya wachimbaji wadogo kutwaliwa na wawekezaji.
Pamoja na Kata ya Igate, nanasi pia linalimwa katika Kata zingine nne za tarafa ya Bugando za Nkome, Nzera, Kagu na Kakubilo chini ya Ushirika wa Wakulima wa Matunda na Mbogamboga Igate (Uwamami), chini ya msaada, ushauri na uwezeshaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Acord.
Namna ya kulima nanasi
Zao la nanasi hustawi katika aina zote za udongo kuanzia ule wa mvinyanzi, kichanga na tifutifu.
Tangu kupandwa hadi kuanza kuvunwa, nanasi huchukua muda wa miezi kumi na nane na huvunwa mfululizo kwa kipindi cha miaka saba kabla ya kung’olewa na kupandwa miche mipya.
Baada ya miaka saba, shamba lililolimwa nanasi hupumzishwa kwa kupandwa aina nyingine ya mazao ikiwemo mihogo ili kurejesha rutuba angalau kwa misimu miwili kabla ya kupanda miche mipya ya mananasi.
Gharama ya kulima nanasi
“Gharama ya kulima hekari moja ya nanasi kuanzia kuandaa shamba, kulima, kununua miche, kupanda, kupalilia hadi kuvuna hugharimu kati ya Sh1 milioni hadi Sh1.5 milioni,” anaeleza mkulima mwingine Hamisi Ramadhani kutoka Kata ya Nzera
Tofauti na mazao mengine, nanasi halihitaji matumizi ya mbolea wala viatilifu zaidi ya kupaliliwa kila gugu linapoota.
“Kwa mwaka mmoja, mkulima wa nanasi hupata mavuno mara tatu katika shamba la nanasi linaloweza kupwandwa hadi miche 3, 000 kwa hekari,” Hamisi anaieleza FikraPevu.
Ingawa bei ya zao hilo hubadilika kulingana na msimu wa mavuno, tunda moja huweze kuuzwa kati ya Sh500 hadi Sh1, 300 kwa bei ya jumla huku mkulima akipata fursa ya kuvuna kwa kipindi cha miaka saba mfululizo kabla ya kung’oa miche na kupandi mipya.
Soko la nanasi
Katibu wa ushirika wa Uwamami, Flavian Budadu anasema zao hilo lina soko kuanzia ndani ya Wilaya na Mkoa wa Geita pamoja miji mingine Mikuu kama Mwanza, Arusha, Dar es Salaam na Dodoma kwa hapa nchini.
Ofisa wa Shirika la Acord, Rachel Nassari, amwiambia FikraPevu kuwa wakulima wa nanasi kutoka Tarafa ya Bugando kupitia Ushirika wa Uwamami na kwa msaada wa shirika lake, wamefanikiwa kupata soko la zao hilo nchi jirani za Uganda na Kenya.
Changamoto kilimo cha nanasi
Kukosekana viwanda vya vidogo, kati na vikubwa vya kusindika mazao ya kilimo ni miongoni mwa changamoto zinawakabili siyo tu wakulima wa nanasi Igate, bali mazao kadhaa ya chakula na biashara nchini.
“Hii inasababisha wakulima wengi kuuza mazao yao walanguzi na watu wa kati bei ya hasara kulinganisha na gharama halisi ya uzalishaji,” Geoffrey Masanja, mkulima Mshauri Kata ya Kakubilo anaiambia FikraPevu.
Wakulima wa nanasi pia hawajaachwa nyuma katika changamoto kadhaa zinayoikabili sekta ya kilimo nchini ikiwemo ukosefu wa zana, viatilifu na pembejeo za kilimo kama matrekta na ushauri wa kitaalam.
“Ushirika wetu wa Uwamami, wenye jumla ya wanachama 105, kati yao wanawake wakiwa 48 pia inakabiliwa na ukosefu wa vifungashio ikiwemo chupa na mifuniko yake kwa ajili ya mradi wa mvinyo wa nanasi tunaotengeneza,” anasema Katibu wa Ushirika huo, Flavian Budadu
FikraPevu imebaini kuwa hivi sasa wanaagiza mifuniko ya chupa hizo kutoka nchini Uganda kwa bei ya Sh.300 kwa kila kimoja, huku chupa za kuhifadhi mvinyo huo wakitumia za kampuni nyingine baada ya kuzikusanya, kubandua nembo na kuziosha.
“Chupa moja ya mvinyo wa nanasi inayotengenezwa na kikundi cha Uwamami inauzwa kwa bei ya rejareja ya Sh2, 500. Hatujaanza kuuza kwa jumla kwa sababu hatuzalishi kiasi kikubwa,” anasema Budadu.
Ushirika huo kupitia mwanachama mmoja mmoja unamiliki na kulima zaidi ya hekari 193 za mashamba ya nanasi na mbogamboga, huku zingine 27 zikiwa zimehifadhiwa kwa ajili ya kuboresha uoto wa asili kwenye eneo la mradi.
Kauli ya viongozi, mtaalam wa kilimo
Gladstone Mlaki, Mtaalam wa kilimo Kata ya Sungusila wilayani Geita anasema mafanikio ya wakulima wa nanasi tarafa ya Bugando yanatokana na wao kufuata na kuzingatia ushauri wa kitaalam na uwezo wa kuhifadhi mazao yao unatokana na ghala la kuhifadhi matunda lililojengwa na shirika la Acord.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ameiambia FikraPevu kuwa serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Geita imewaunga mkono wakulima wa nanasi kupitia ushirika wao wa Uwamami kwa kuwapa mikopo kusaidia kugharamia shughuli za uzalishaji.
“Julai 8, mwaka jana Halmashauri iliwapa mkopo wa Sh5 milioni kupitia kikundi cha mradi wa maendeleo ya vijana,” anasema Kupufi na akiwahimiza wakulima hao kuimarisha ushirika wao ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo.