HAKUNA anayejali kama mjamzito iwe kijijini au mjini anapotaabika na mimba yake wakati mtoto anayezaliwa ni mali ya taifa. Hakuna mtaalam wa afya anayejali kuona mjamzito anateseka na kushindwa kusukuma mtoto wakati wa kujifungua na hakuna anayejali kuona watoto wachanga hasa vijijini wanapokufa baada ya kuzaliwa.
Hakuna anayejali kuona wanawazito kukokotwa kwenye mikokoteni ya punda na baiskeli kufuata huduma ya kujifungua. Hakuna anayejali wakunga wa jadi wanaosaidia wajawazito kujifungua salama na hakuna anayejali kutimiza ahadi kuhakikisha huduma bora za afya kwa mama na mtoto chini ya miaka mitano.
Hakuna anayejali kutenga bajeti za uhakika kwa ajili maji safi vijijini. Hakuna anayejali kusogeza kwa vitendo huduma za afya katika vitongoji na hakuna anayejali kuona kupunguza mila na desturi kwamba wajawazito kujifungulia nyumbani ni ujasiri.
Hakuna anayejali kusikia wajawazito wakitolewa kauli chafu kutoka kwa baadhi ya watoa huduma za afya. Hakuna anayajali kutatua kwa dhati tatizo la uhaba wa vitendea kazi katika huduma za afya. Hakuna anayejali ukosefu wa maji safi katika vituo vya afya hospitali na zahanati.
Hakuna anayajali kutenga na kuweka sehemu ya kupumzika wajawazito kabla na baada ya kujifungua hasa kwenye zahanati. Hakuna anayejali kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa jinsi zote badala yake elimu hiyo inatolewa kwa upande wa wanawake ambao ‘’wanaiba’’ kutumia huduma hiyo na wakibainika na waume zao wanapigwa na wengine wamepoteza maisha.
Hakuna anayejali kuona mimba za utotoni zikiendelea kutokea kila siku kutokana na mila na desturi, hakuna anayejali sheria mbaya ya ndoa na mkanganyiko kati ya sheria ya ndoa inayoruhusu msichana wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi wake na katiba inayomtambua mtu mzima kuwa ni yule mwenye miaka 18.
Hakuna anayejali kuona wanaume wananyanyaswa na wake zao na kulazimika kukimbia ndoa na kuwaacha watoto wakiteseka huku wengine wakipoteza maisha na hakuna anayejali kuona watoa huduma za afya wakiishi umbali mrefu na maeneo yao ya kazi.
Inasikitisha kuona hakuna anayejali malalamiko ya wataalamu wa afya kuendelea kununua dawa za wagonjwa kwa mfumo mbovu wa MSD wakati mfumo huo ni mbovu na dawa zinazotakiwa kuuzwa kwa shilingi 10,000 zinauzwa shilingi 30,000 kupitia watendaji wa serikali wanaohusika na manunuzi.
Hakuna anayejali kuona mtumishi anaacha taaluma yake ya awali na kujiunga na masomo ya ununuzi wa umma kwasababu huko ndiko kwenye rushwa na uchafu usioandikika wa wizi wa fedha na mikataba mibovu.
Mambo kadhaa niliyoyaanisha hapo juu yapo wilayani Bunda mkoani Mara ambako kuna idadi kubwa ya vifo vya akina mama na watoto wenye umri chini ya miaka mitano vinavyotokana na uzazi nchini Tanzania.
Baadhi ya wananchi wanaopata huduma za afya katika kituo cha afya cha Ikizu kilichopo katika kijiji alichozaliwa Jaji Joseph Sinde Warioba wananungunika kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi yake ya kupeleka gari la wagonjwa katika kituo hicho.
Wanasema kuwa kukosa gari kwa kituo hicho cha afya kunasababisha wagonjwa wakiwemo wajawazito wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji kukodi ‘’Toyo’’pikipiki ili kupelekwa hospitali teule ya wilaya.
‘’Tunalazimika kukodi ‘’Toyo’’ au ‘’michomoko’’ tax kwa Sh.30,000 ili kuwapeleka wagonjwa ‘’DDH’’ hospitali ya wilaya’’ walisema baadhi ya wananchi ambao waliomba hifadhi ya majina yao.
Mbali na hilo, baadhi yao wanaulalamikia uongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu kuwa unawauzia damu ya kuongezea wagonjwa kati ya Sh.15,000 mpaka Sh. 20,000 kwa unit moja(mfuko).
Mganga mkuu kiongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu kilichopo eneo la kata ya Nyamuswa tarafa ya Ikizu Dr.Abahehe Kanora, anasema kuwa kituo hicho hakina gari la wagonjwa na walitegemea kuwa Rais Kikwete angewapelekea kutokana na ahadi yake alipokuwa akiomba kura kwa wananchi wa eneo hilo mwaka 2010.
‘’Hapa kulikuwa na gari Pick up lakini iliuzwa na kuharibika mwaka 1996 na wilaya ina ambulance moja tu, tegemeo letu kubwa pamoja na wananchi ilikuwa ni kutimia ahadi ya Rais Kikwete ambapo aliahidi pale njia panda kwenye mti wa kumbukumbu ya Chifu Makongoro aliposimamishwa na wananchi mwaka 2010’’ anasema Dr. Kanora.
Kuhusu usafiri kwa wajawazito wanaokwenda kujifungua katika kituo hicho, anasema wanasafiri kwa pikipiki na wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji wanalazimika kukodi gari maarufu kwa jina la michomoko kisha kupelekwa hospitali teule ya wilaya (DDH) iliyopo umbali wa kilomita 24.
Akizungumzia uhalisia wa kituo hicho ha afya, Dr. Kanora anasema kuwa mbali na tatizo la gari la wagonjwa, pia kuna tatizo la upatikanaji wa dawa kutokana na mfumo wa manunuzi ya umma unaowalazimisha kununua dawa zote katika bohari ya serikali yaani MSD ambapo dawa hupelekewa pungufu tofauti na mahitaji.
Alipoulizwa kama wajawazito na watoto hupatiwa matibabu bure kama inavyoelekezwa na sera ya afya ya mwaka 2007 ili kupunguza vifo vya makundi hayo, alisema kuwa kwanza hakuna dawa zinazopelekwa maalumu kwa ajili ya makundi hayo lakini wajawazito hupatiwa bure huduma za kujiandikisha Kliniki, kujifungua na vipimo.
Kuhusu wagonjwa wakiwemo wajawazito kuuziwa damu kwa Sh. 15,000 mpaka 20,000. Alisema malalamiko hayo si ya kweli bali uongozi wa kituo ulikubaliana na kamati ya afya ya eneo hilo kuwa kutokana na uhaba wa vitendanashi ikiwemo vifaa na dawa za kupimia damu kila anayeongezewa damu anachangia Sh. 2000.
‘’Malalamiko hayo si kweli bali kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wagonjwa na ndugu zao wanaohitaji damu wakiambiwa kuwa hatuna damu ndipo wanalazimika kuwatafuta watu nje ya kituo na kuja nao ili kuwatolea damu hao ndiyo wanaowauzia lakini sisi hapa anayechangia damu na anayeongezewa kila mmoja hutozwa Sh. 2000’’ alisema Dr. Kanora.
Kuhusu maji alisema kuwa mpaka sasa kuna tatizo kubwa la maji na kila mgonjwa wakiwemo wajawazito lazima aende na ndugu yake ambapo baadhi ni lazima waende na maji eneo la kituo hicho cha afya.
Mpaka waandishi wa habari wanaondoka eneo hilo la kituo cha afya, wameacha na kushuhudia familia mbili za watumishi wa kituo hicho wakiwa hawana vyoo na kulazimika kujisaidia katika choo cha wagonjwa kilichopo umbali wa mita 25 baada ya choo walichokuwa wakichangia kubomoka.
Baadhi ya wajawazito na akima mama wanaonyonyesha wanaoishi katika maeneo ya Bukama, Makongoro kata ya Nyamuswa, Nyabuzumu na kijiji cha Kambubu kata ya Nyamang’uta walisema kuwa kutokana na huduma zisizoridhisha katika kituo hicho cha afya na hospitali teule ya wilaya hiyo, wanaona ni bora kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
‘’Mimi uzao wangu huu ni wa nane lakini nina watoto watato walio hai na wengine nilijifungulia kwa mkunga wa jadi Mama Nyangi Kisizile kwasababu hospitalini kuna matusi na fedheha nyingi na wala hatusaidiwi’’ alisema Anna Japhet(35) mkazi wa Kijiji cha Kambubu.
Utafiti nilioufanya umebaini kuwa katika kijiji hicho kuna wakunga wa jadi watatu ambapo eneo la Mugara linaongoza kwa wajawazito kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
Takwimu zinaonesha kuwa akina mama mama 185 walijifungulia kwa wakunga wa jadi waliopata mafunzo na akina mama 71 walijifungulia kwenye zahanati ya Mugara mwaka 2009.
Ingawa wakunga wa jadi wanapuuzwa na kudharaulika na wasomi wengi lakini ukweli wa utafiti unaonesha kuwa kujifungulia kwa wakunga wa jadi hasa waliopata mafunzo kunapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la vifo vya akina mama wajawazito, lakini hakuna msomi anayejali kuwapa mafuzo kwa dhati wakunga wote wa jadi nchini.
Naye mjamzito Agness Baraka (23) anasema mimba aliyonayo ni ya nne lakini ana mtoto aliye hai mmoja na kwamba anahudhuria kliniki lakini bado halidhishwi na huduma za hospitalini hivyo anaona bora kujifungulia kwa mkunga wa jadi ama nyumbani kama alivyojifungua mtoto wake wa kwanza.
‘’Ukienda hospitali mfano kule DDH, wanasema kuwa mjamzito anayepaswa kusaidiwa kujifungua ni yule mwenye mimba ya kwanza lakini tuliowahi kuzaa wanatulazimisha tujifungue wenyewe bila msaada wao na kama hauna pesa unaweza kufa’’ anasema Anna.
Mkunga wa jadi Veronica John Leopard(64), alisema kuwa yeye ni mmoja wa wakunga wanaosaidia wajawazito kujifungua katika wilaya ya Bunda na hata hospitali wanamjua lakini halidhishwi na huduma zinazotolewa na kituo cha afya cha Ikizu maana kila kitu ni pesa na hivi karibuni alimpeleka mwanaye kujifungulia katika kituo hicho na kujionea huduma zisizoridhisha.
Umefika wakati kama taifa kujisahihisha kwa vitendo mfano suala la bajaji za kubeba wajawazito bila kutafuna maneno hazifai na mpaka sasa hazitumiki kwasababu hazikati kona upande wa kushoto hivyo rai yangu kwa Rais Kikwete ni kuliona hilo na kutatua kero hizo hapo juu kwa vitendo ili kujenga taifa imara lenye watu wenye afya njema kwa kuanzia katika makundi hayo yaani wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Mwandishi 0754 440749 barua pepe; [email protected]