Wanaume wengi hawajui matumizi sahihi ya kondomu

Gordon Kalulunga

WANAUME wengi nchini wakiwemo wasomi hawajui matumizi sahihi ya mipira ya kiume ‘’Kondomu’’. Ikiwa ni kuvaa kabla, wakati wa tendo na kuvua baada ya kujamiiana na wenza wao.

Hali hiyo imeendelea kudhoofisha jitihada za serikali katika kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi vya Ukimwi (VVU) ambapo kwa sasa vijana wengi wanakabiliwa na magonjwa kama Gonorea, kaswende na syphilis ambapo baadhi yao walitumia kondomu na baadhi hawakutumia.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii kwa miezi mitatu sasa, umebaini kuwa wanaume hao hasa walioko kwenye mahusiano ya ngono, mapenzi na hata ndoa, baadhi wamekuwa wakitumia mipira hiyo kwa mazoea.

Baadhi ya wanaume waliohojiwa katika mikoa ya Mara, Mwanza na Mbeya, walisema kuwa wanatumia mipira hiyo kwa kuvaa wenyewe na kuvua wenyewe baada ya kujamiiana na wanawake na kwamba hawajawahi kupata elimu zaidi ya hapo na hata wanapovua wanatumia mikono yao bila karatasi.

Hali hiyo ya kutumia mpira huo wa kiume kisha kuutoa bila hata kushika na karatasi kisha kujifuta, inasababisha wanaume wengi kushika majimaji ya uke kisha kujipaka katika sehemu zao za siri na baadhi kuambulia ‘’kujiambukiza’’ magonjwa ya zinaa.

Wanaume wengine na wanawake wamepata magonjwa hayo kwa kutumia kitambaa kimoja kujifutia baada ya tendo la ndoa licha ya kutumia mipira hiyo.

Kuhusu maelezo yanayokuwepo katika baadhi ya makaratasi ya kuhifadhiwa kondomu ikiwa ni pamoja na michoro ya picha.

Wengi walisema kuwa hawazingatii kusoma na hata kuangalia michoro hiyo ambayo inaonesha jinsi ya kuvaa kondomu kabla, wakati na baada ya kutumia.

Uchuguzi zaidi umebaini kuwa wengi hawapendi kutumia kondomu zinazotolewa bure na zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa dhana kwamba kondomu hizo hazina ubora.

Hata hivyo baada ya mwandishi kufika katika zahanati ya Bunda mkoani Mara na kuomba kupewa kondomu hizo, alipewa boksi moja ambalo licha ya kuwa na kondomu nyingi hakuna maelekezo yeyote jinsi ya kutumia mipira hiyo ya kiume hali inayoonesha kuwa elimu inahitajika zaidi kuanzia wizara ya afya mpaka kwa jamii.

Utafiti huo uliohusisha mahojiano ya baadhi ya wananchi wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) wilayani Ileje mkoani Mbeya, wananchi hao hasa kijiji cha Ikumbilo, walikiri kutumia kinga (kondomu) kufanya ngono na wapenzi wao wapya.

Wanasema kuwa kondomu hizo walitumia mara ya kwanza na mara ya pili baada ya kukubaliana na wenzi wao hao na ilipofika mara ya tatu na nne na kuendelea hawakutumia kinga yeyote kabla ya kupima afya zao.

Kwa upande wa baadhi ya wasichana nao wanakiri kuwa mara nyingi kuhusu kutumia kondomu unakuwa ni uamuzi wa wanaume wao na wanasema kondomu za kike hazitumiki kutokana na uvaaji wake kuchukua muda mwingi na wanapokosea kuvaa vizuri wanapoanza kufanya tendo la ndoa wanaumia.

Hata hivyo kwa upande wa watu wanaoishi na VVU, Dr.Moke Magoma ambaye ni bingwa ya magonjwa ya wanawake kutoka shirika la kimataifa la Evidence for action (E4A) anasema kuwa watu wanaotumia dawa za kurefusha maisha ARV wanakuwa na asilimia ndogo ya kuwaambukiza wena wao.

‘’Ni vema kupima afya na mtu anapogundulika kuwa ameathirika na akaanza kutumia dawa huwa katika nafasi ndogo ya kumwambukiza mtu mwingine pia mwili wake kutodhoofu’’ anasema Dr. Magoma.

Kama zilivyo nchi nyingi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara, Tanzania ina idadi kubwa ya vijana wadogo.

Moja ya tatu ya watanzania wote wana umri kati ya miaka 10 na 24, umri ambao vijana wengi huanza vitendo vya kujamiana. Takribani asilimia 7 ya vijana kati ya umri miaka 15-19 zimepungua katika miaka ya hivi karibuni.

Hii inaonekana wazi pale mtu anapochukulia uwiano wa watu wanaokiri kujihusisha na wapenzi wengi-idadi ya vijana kati ya umri wa miaka 15 na 19 wanaokiri kuwa na wapenzi wawili au zaidi imepunguza kwa nusu kati ya mwaka 2004 na 2008.

Hata hivyo, matumizi ya kondomu bado yapo chini kwa vijana katika umri huo. Chini ya moja ya tatu ya vijana wanakiri kutumia kondomu wanapokutana na wenzi wao kujamiana kwa mara ya kwanza. Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwa na elimu endelevu kuhusu ngono kwa kundi hili.

Wanawake katika Tanzania wameathirika zaidi na maambukizo ya VVU na UKIMWI. Katika mwaka wa 2008, wanawake wenye maambukizo walikuwa ni asilimia 60 ya watu wote wenye maambukizo ya VVU nchini.

Wanawake huwahi kuambukizwa, jambo linalosababishwa na wanawake kuwa na wapenzi waliowazidi umri au kutokana na kuwahi kuolewa kabla ya viungo vyao vya uzazi kupevuka.

Sababu nyingine ya wanawake kuwa na maambukizo makubwa ni kutokana na kuwa vigumu kwao kujadiliana kuhusu mambo ya ngono na kujamiana kutokana na kukosekana kwa usawa wa kijinsia.

Mfano mmoja ambao umekuwa kawaida kwa wanawake walio wengi ni kule kuwa na wapenzi wazee ambao huwapa zawadi nyingi kama vile fedha na zawadi nyingine za kijamii ili wakibali kufanya ngono nao.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749. Barua pepe; [email protected]

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *