Hali ya uondoaji wa majitaka jijini Dar es Salaam bado kizungumkuti

Jamii Africa

DAR ES SALAAM ni miongoni mwa majiji makubwa barani Afrika ambayo hayajapangwa. Ama kwa lugha rahisi, ni jiji lililojengwa kiholela.

Jiji hilo lenye wakazi takriban milioni tano wanaoishi katika wilaya tano za Ilala, Kigamboni, Kinondoni, Temeke na Ubungo siyo tu kwamba linakabiliwa na miundombinu mibovu, bali hata mazingira yake ni machafu pia.

Ukiacha maeneo ya Ilala, Kinondoni, Masaki, Mikocheni, Oysterbay na Upanga ambayo ujenzi wa nyumba uko katika mfumo mzuri, maeneo mengi yaliyosalia yamejengwa kikolela kiasi kwamba ni vigumu kwa wakazi wa maeneo hayo kupata huduma muhimu za kijamii, hususan barabara.

FikraPevu inafahamu kwamba, kwa miaka zaidi ya mitano sasa jiji hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya msongamano wa magari barabarani, ambao kimsingi unasababishwa na ujenzi holela na kutokuwepo na mipango madhubuti ya ujenzi ambayo ingewezesha kuwepo hata barabarani za mitaa na kurahisisha usafiri kwa wakazi wake.

Lakini mbali ya changamoto ya msongamano wa magari, magonjwa ya milipuko kama kipindupindu yameweka makazi ya kudumu jijini Dar es Salaam ambapo kila mwaka ni lazima yalete madhara makubwa.

Hali hiyo inatokana na uchafu mwingi uliopo, ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mifumo mibovu na chakavu ya majitaka, huku maji ya mvua nayo yakikosa pa kutokea baada ya wakazi wa jiji hilo kuvamia mikondo ya kupitisha maji hayo, hivyo kusababisha mafuriko kila mara mvua zinaponyesha.

Uvamizi huo wa miaka nenda-rudi katika mabonde kama Mto Msimbazi, Mto Mzinga, Mto Kizinga na vijito vingine vidogo hasa vya Mwananyamala na Magomeni umeifanya Dar es Salaam kuwa kero na kuondoa sifa ya kuitwa jiji.

Mabomba na mitaro ya kupitisha majitaka yapo machache kulingana na uzalishwaji wa majitaka hayo ambayo yanatokana na ongezeko kubwa la watu.

Miundombinu mingi ya majitaka imejengwa miaka mingi iliyopita huku mingine ikiwa chakavu mno, ambapo kila wakati mvua zinaponyesha mingi huwa imeziba na kusababisha majitaka kufurika kila mahali, hususan maeneo ya Posta na Kariakoo.

Tatizo kubwa lililopo ni kuongezeka kwa watumiaji wapya huku kukiwa hakuna juhudi za dhati za kupanua ama kuifanyia marekebisho miundominu ya awali.

Jambo la hatari zaidi, kila wakati mvua zinaponyesha, wakazi wengine wasio waungwana, hufungulia mabomba ya vyoo vyao na hivyo vinyesi kuzagaa ovyo, hali inayohatarisha usalama wa afya za wakazi wa jiji hilo.

Kutokana na wananchi wengi wa Jiji la Dar es Salaam kujenga nyumba bila kufuata mipango miji, maeneo mengi yanaonekanakubanana, huku baadhi ya wakazi wakifikika kwa vichochoro vyenye upana chini ya mita mbili tu.

Ufinyu huo wa njia unasababisha magari ya kuondoa majitaka kushindwa kuwafikia wananchi wengi.

Kutokana na jiografia ya Jiji la Dar es Salaam yenye mabonde na miinuko, kipindi cha mvua maji mengi huelekea maeneo ya mabondeni ambako wananchi hutoboa mashimo ya majitaka na kufanya majitaka hayo kuchanganyika na maji ya mvua na mwishowe kuishia maeneo ya mabondeni na baharini.

Maeneo ya Tandale, Manzese, Magomeni, Buguruni, Tandika na Mbagala ambako wakazi wengi wamejenga kiholela bila kufuata taratibu za mipango miji, ndiyo huathirika zaidi na ‘mafuriko’ ya majitaka.  

FikraPevu inatambua kwamba, maeneo hayo ndiyo kwa kiasi kikubwa huongoza kwa idadi ya wagonjwa wa milipuko, hasa kipindupindu, kwani majitaka yaliyochanganyika na maji ya mvua huingia hadi kwenye makazi yao.

Kampuni ya Dawasco, ambayo inayohusika na suala la uondoaji wa majitaka, imeshindwa kudhibiti utumiaji sahihi wa mitaro, makorongo, na mito katika jiji katika kusafirisha majitaka.

Mito mingi hutumika na wakazi kama njia za kutoa maji taka majumbani kutokana na ufinyu wa njia unaozuia magari ya majitaka kuweza kuingia kwenye makazi yao kunyonya majitaka hayo.

Aidha, viwanda vingi vimejenga mabomba kutoka katika maeneo yao na kuyaelekeza katika mitaro na makorongo makubwa yaliyo karibu.

Mfano mzuri ni Mto Ubungo, Mto Msimbazi na Korongo la Tandale, ambayo daima hutirisha majitaka yanayotoa harufu kali na kuathiri afya za wananchi, hususan watoto wadogo, waishio jirani na makorongo hayo.

Wakulima wa mbogamboga jijini humo, wakitambua kwamba maji yanayopita kwenye mabonde kama ya Mto Msimbazi ni machafu na hayafai, wao hutatumia kwa ajili ya kumwagilia mboga zao, hali ambayo inazidi kuweka rehani maisha ya wakazi wengi wa jiji hilo wanaotumia mboga hizo.

Halmashauri za Manispaa pamoja na Jiji bado hazijafanya jitihada zozote kuhakikisha mifumo ya utiririshaji wa majitaka inaboreshwa.

Aidha, mamlaka husika zinatakiwa kuweka sheria kali za kudhibiti wakazi kuchepua mashimo yao ya majitaka kuelekea katika mito na mabonde ndani ya jiji hilo hasa nyakazi za mvua.

Tabia ya utupaji wa taka ngumu katika mitaro ya maji nayo inasababisha kuziba kwa mitaro hiyo na kufanya maji yatuame wakati wa mvua.

Taka kama chupa za plastiki, mifuko ya plastiki na mabaki ya bidhaa mbalimbali ni vizuizi vikubwa katika utiririshaji wa maji kwenye mitaro hiyo ambapo mvua zinaponyesha maji hayo hufurika na kusambaa hovyo.

Idara ya Mipango Miji nayo inapaswa kurejea upya michoro yake na kuhakikisha inasimamia sheria ili kuzuia ujenzi holela, ambao licha ya kuziba njia za watu na maji, lakini husababisha maafa ya mafuriko na wakati mwingine ajali za moto zinapotokea inakuwa vigumu kufanya uokoaji.

Wanamazingira pamoja na mamlaka zinazohusika nao wanapaswa kudhibiti suala la uchimbaji wa mchanga katika mito iliyo kando ya jiji, kwani husababisha maji kufurika katika kipindi cha mvua na kuleta maafa.

Mara nyingi uchimbaji huo wa mchanga huleta mmomonyoko wa udongo katika kingo zake na kusababisha matatizo kama vile kubomoka kwa madaraja na mafuriko pamoja na maji kuzua mikondo mipya ambayo huleta madhara kwa jamii.

Serikali inapaswa kujenga miundombinu mipya na kutengeneza ile ya awali ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Aidha, Serikali, kupitia Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), inapaswa kuvifungia viwanda vyote ambavyo vinatiririsha majitaka yenye kemikali katika makorongo na mito ya kupitisha maji ya mvua, kwani ni maji hayo ambayo baadhi ya wananchi wasio na uelewa, au pengine kwa makusudi, huyatumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Wananchi nao wanapaswa kupewa elimu ya kutosha na mamlaka husika  juu ya madhara yanayoweza kutokea iwapo majitaka yatatawanywa hovyo au kutumika katika kilimo.

Mamlaka hizo pia zipitie upya sheria zinatakiwa kuhakikisha zinadhibiti utupwaji hovyo wa taka katika njia za majitaka na maji ya mvuasambamba na wale wanaozibua vyoo vyao nyakati za mvua au wanaojenga pembezoni mwa njia za kupitisha maji ya mvua. Wahusika wanatakiwa kuwajibishwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *