Rais John Magufuli ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia upya mfumo wa utozaji kodi ili kuwawezesha watu kulipa kodi inayoendana na mapato halisi ya biashara zao.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo mjini Dodoma leo wakati akizindua ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway) kutoka Morogoro hadi Makutupora-Dodoma ambapo amesema kulipa kodi kwa baadhi ya wananchi imekuwa kero kwasababu baadhi ya wafanyakazi wa TRA wanajihusisha na vitendo vya kuwaibia wananchi kwa kuwatoza kodi kubwa kuliko viwango wanavyostahili kulipa.
“Kuna watu TRA sio watu wazuri, na saa nyingine wanapokwenda kule wanaipaka matope serikali kwa kusema hii ndio dhana ya ‘Hapa Kazi Tu’ kumbe wao ndio wanatafuta kazi ya kuliibia taifa. Kulipa kodi isiwe kero, iwe ni heshima kwamba mwananchi anaenda kulipa kodi kwa maslahi ya nchi yake”, amesema Rais.
Ameongeza kuwa TRA wanapaswa kupitia upya mfumo wa utozaji kodi ili wananchi wahamasike kulipa kodi kulingana na miradi wanayomiliki na kuhakikisha wanawaelimisha wananchi juu ya njia sahihi na faida za kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
“Lakini niwaombe pia TRA muangalie kodi zenu mnazozitoza, inawezekana zingine ni kubwa kuliko miradi wanayotekeleza wananchi. Badala ya kuwa motisha kwa walipa kodi inakuwa kero kwa walipa kodi”, amesema Rais na kuongeza kuwa,
“Na badala yake wanapokwepa kulipa kodi wakati wangeelimishwa vizuri wangeweza kulipa kodi, kwahiyo TRA mjipange vizuri. Kamishna wa TRA, Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu mkalisimamie hili”.
Amegusia kodi ya majengo ambayo imekuwa ikitozwa nchi nzima katika nyumba za kuishi na majengo ya biashara ambapo imekuwa ikitofautiana kutoka eneo moja hadi lingine na kuibua maswali mengi yasiyo na majibu kwa wananchi kwasababu fedha inayotozwa haiendani na thamani ya jengo husika.
“Tulizungumzia kuhusu kodi za nyumba, mmeenda ninyi kutoza mpaka laki sita mpaka milioni kutoza nyumba, wakati tuliwaambia mpige flat rate (kiwango sawa) ambayo itakuwa motisha kwa watanzania wengi wawe wanalipia majengo yao”, amesisitiza Rais.
Awali kodi ya majengo ilikuwa inakusanywa na Halmashauri za Wilaya lakini ili kuongeza ufanisi TRA ilikabidhiwa jukumu hilo tangu Julai mosi, mwaka 2016 kwa mujibu wa mabadiliko ya Sheria ya Majengo sura namba mbili ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura namba 290 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania sura ya 339.
Kodi ya majengo ni tozo inayotozwa kwa mujibu wa sheria kwenye majengo au nyumba ambazo zinakaliwa au kumilikiwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi na sheria nyinginezo za nchi.
Pia majengo hayo au nyumba hizo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa kuwa zimefanyiwa uthamini, ikiwa ni pamoja na wamiliki wake kutambuliwa kwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Katika suala zima la ulipaji wa kodi za majengo, tozo hizo hutofautiana kutokana na sheria ndogo zilizotungwa na mamlaka za Serikali za Mitaa husika na kwa upande wa maeneo ndani ya jiji moja tozo hutofautiana, pia tozo za ndani ya manispaa moja na mji mmoja hutofautiana.
Malalamiko ya Sekta binafsi
Kauli ya Rais Magufuli kuhusu TRA kupitia kodi wanazotoza kwenye miradi inayotekelezwa na wananchi huenda ikajibu malalamiko ya muda mrefu ya sekta binafsi juu ya utekelezaji wa Sheria ya Kodi ambapo imekuwa sio rafiki kwa upatikanaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa nchini.
Mwaka jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alinukuliwa na vyombo vya habari akisema serikali inafanya vizuri katika kuweka mazingira mazuri ya biashara lakini kero yao kubwa ni jinsia TRA inavyokusanya kodi ambazo zinaathiri uzalishaji na biashara zao.
“Serikali kwa juhudi zake imeendelea kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, kama kurekebisha njia za usafirishaji ikiwemo reli na viwanja vya ndege, lakini suala la kodi limekuwa ni tatizo, malalamiko mengi ya sekta binafsi yanatoka kwa namna ambavyo TRA wanakusanya kodi, ni kero kubwa, imekuwa kwa mwezi mmoja taasisi binafsi inaweza ikatembelewa na timu ya TRA tatu na zote zikaja na makadirio tofauti”, alinukuliwa Simbeye.
Inaelezwa kuwa mfumo mpya wa kodi katika serikali ya awamu ya tano umechangia kwa sehemu kufungwa kwa biashara mbalimbali ambapo mwaka jana, Uongozi wa Mlimani City aliamua kulifunga Duka la Nakumatt lilipo jijini Dar es Salaam kutokana na kutotimiza majukumu yake kama mlipakodi wa jengo hilo hivyo kurudisha nyuma upatikanaji wa Mapato.
Athari za ongezeko la kodi pia zinajidhihirisha katika sekta ya usafirishaji na ughavi ambapo mizigo iliyokuwa inapitia katika bandari ya Dar es salaam kwenda nchi za Zambia, Congo DRC na Rwanda imepungua. Pia usafiri wa malori kutoka na kuingia nchini umepungua kutokana na mabadiliko ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli ameimarisha ulipaji wa kodi ambapo hatua muhimu iliyofikiwa ni matumizi ya mashine za EFD katika maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa yanadhaniwa kukwepa kodi na kuikosesha serikali mapato. Mkakati huo umeenda sambamba na ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali.
Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julai, Agosti na Septemba), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya jumla ya Sh.3.65 trilioni ambalo ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka 2016. Na inatarajia kufikia lengo lake la kukusanya Sh.17 trilioni kwa mwaka.
Ujenzi wa Reli ya kisasa kuongeza wigo wa biashara na mapato ya serikali
Maoni ya Wananchi
Baadhi ya wachangiaji katika mtandao wa Jamii Forums wamesema kuwa mlolongo wa kodi zinazotozwa na TRA umeathiri pia maisha ya kwaida ya wananchi wa kipato cha chini.
Mchangiaji mmoja anayejulikana kwa jina la Jidu La Mabambasi ameandika “ Bila kumung'unya maneno hali ni mbaya. Mimi niko sekta binafsi na nimejiajiri na nimeajiri. Kutokana na mapato kuporomoka changamoto ya kulipa mishahara ni kubwa. Na ili usipate kero za kushindwa kulipa kodi za kuajiri kama PAYEE, NSSF, SDL, Workers Compensation na mafao mengine, inabidi kuwaachisha kazi wafanyakazi mara moja”, amesema na kuongeza kuwa,
“Kero ya TRA ni tatizo lingine sababu wao wanafanya kukomoa ili kufikisha lengo la makusanyo ofisini kwao. TRA haiwezi kukwepa lawama za kufunga biashara nyingi hapa mjini”.
Naye Eric Cartman katika ukurasa wa JamiiForums ameshauri kuwa wafanyabiashara watunze kumbukumbu za mapato na matumizi ili watozwe kodi stahiki, “Kuhusu kodi ya wafanya biashara ni ‘corporate tax’, na nyingine ni ya VAT, sasa ili suala la kodi ni vizuri wakawa wanaweka takwimu zao vizuri za mapato na matumizi. Wengi hawapendi kuweka matumizi na mapato yao halali hivyo kuwapa nafasi TRA kuwakadiria au kuwapa data zaidi juu ya mapato yao”.