Hatari: Bodaboda zaongeza idadi ya wagonjwa wa kifafa Tanzania

Jamii Africa

ZAIDI ya Watanzania milioni moja wanaugua ugonjwa wa kifafa (epilepsy), FikraPevu inaripoti.

Ukiachilia mbali watoto, lakini watu wanaopata ajali za magari, bodaboda na kadhalika, wako hatarini kuugua ugonjwa wa kifafa ikiwa watakuwa wameumia kichwani na ubongo kuathirika.

Kwa kipindi cha takriban miaka 10 sasa, ajali za bodaboda zimeongezeka na kuwaacha watu wengi, hususan vijana, wakiwa na ulemavu wa kudumu.

Taarifa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaeleza kwamba, Tanzania inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifafa duniani huku vijiji vya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro yenye wakazi 265,203 vikiwa na idadi kubwa ya wagonjwa hao, ambapo katika watu 1,000 kuna wagonjwa 37.5 wa kifafa.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, ugonjwa wa kifafa ni mojawapo ya sababu zinazochangia vifo ambapo unakadiriwa kuchukua nafasi ya 7 hadi 15 kama kisababibishi cha vifo Tanzania.

“Wagonjwa wa kifafa katika Tanzania wako katika hatari ya kifo mara sita zaidi ukilinganisha na mwananchi wa kawaida kwenye jamii. Zaidi ya 60% ya vifo vinavyotokana na matatizo ya kifafa, husababishwa na athari za ugonjwa wa kifafa moja kwa moja,” zimesema taarifa kutoka Wizara ya Afya.

FikraPevu inatambua kwamba, wagonjwa wengi wa kifafa ni vijana, wakiwa na umri wa wastani wa miaka 15, na zaidi ya 24% ya wagonjwa wa kifafa wana ulemavu mwingine, wengi wao kutokana na kuangukia moto wakati mgonjwa anapopatwa na degedege.

Inaelezwa kwamba, ni 50% tu ya wagonjwa wa kifafa na ndugu zao ambao hutafuta ushauri miezi miwili baada ya dalili za kifafa kuanza huku 70% kati ya hao huenda kuwaona waganga wa jadi na wengine viongozi wa dini.

Aidha, ni 60% tu ya wagonjwa wa kifafa hufika kwenye vituo vya afya ndani mwaka mmoja baada ya dalili za kifafa kuanza, lakini kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ni asilimia 5-10 ndio huweza kupata matibabu sahihi.

Wakati wa maadhimisho ya siku ya kifafa duniani Februari 13, 2017, ilielezwa kwamba ingawa ugonjwa huo unatibika, lakini wananchi wengi wana mtazamo hasi.

“Zaidi ya 36% ya watu bado wanaamini kuwa ugonjwa wa kifafa unatokana na nguvu za giza au kulogwa… Kifafa kimefanywa kuwa ugonjwa wa siri na zaidi ya 58% ya idadi ya watu huamini unaleta ugonjwa sugu wa akili.

“Miongoni mwa jamii yetu bado inaaminika ni ugonjwa wa kuambukiza na 50% ya wagonjwa wa kifafa hupatwa na msongo wa mawazo na kukosa furaha,” zimeeleza taarifa kutoka Wizara ya Afya.

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, anasema mambo mengi yanayosababisha kifafa yanazuilika kuanzia kuumia ubongo wakati mama anapojifungua, magonjwa yanayosababishwa na vijidudu kama ‘parasite’ na ‘bacteria’.

Waziri Ummy anasema, ugonjwa huo umewanyima fursa Watanzania wengi, hasa watoto, kupata haki zao za msingi za kijamii kama elimu na hata kuoa ama kuolewa.

“Asilimia 45 ya watoto wenye umri wa kuanza shule wenye tatizo hili la kifafa hawapelekwi shule na 68% ya wanaokwenda shule mahudhurio yao  hayaridhishi ambapo ni 37% tu ndio humaliza elimu ya msingi,” anasema Waziri huyo wa Afya na kuongeza kwamba mara nyingi watoto hao wanazuiwa na ndugu na jamaa zao kucheza pamoja na wengine, hivyo hubakia kufichwa katika jamii.

Anaongeza: “Zaidi ya 55% ya watu wenye kifafa Tanzania hawana ajira. Watu pia huwakwepa kuwaoa ama kuolewa nao, na kama wakioa au kuolewa wengi wao huachika ndani ya muda mfupi tu.”

Hata hivyo, matibabu ya wagonjwa wa kifafa hutolewa bure kama ilivyo kwenye Sera ya Afya ya Taifa, kwani ni mojawapo ya magonjwa sugu yaliyoainishwa kwenye sera hiyo.

“Wizara ya Afya inagharamia matibabu haya kwa kutoa dawa 3 muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya, dawa hizi ni Phenobarbitone, Phenytoin na Carbamazepine. Hata hivyo, kuna kipindi huwa kunatokea changamoto za kukosekana kwa dawa hizi kwa baadhi ya maeneo, lakini inapobainika hushughulikiwa mara moja,” anasema.

Waziri Ummy anasema kwamba, Wizara yake kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa ugonjwa wa Kifafa Tanzania wanaendelea kufanya kazi pamoja katika kuimarisha afya za wagonjwa wa kifafa kwa kuwapatia elimu maalumu ya afya dhidi ya ugonjwa huo.

“Jamii inapaswa kutambua na kuelewa kuwa hospitali ndiyo sehemu sahihi ya kwenda pale wanapokuwa na dalili za ugonjwa huu. Kifafa ni ugonjwa au tatizo la mfumo wa fahamu linalosababishwa na magonjwa mengi na unatibika, hivyo tushirikiane pamoja kuhamasisha watu wenye matatizo haya wafike kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupatiwa matibabu husika,” anaongeza.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *