MATOKEO ya kidato cha nne yalitangazwa mwezi Januari 31 2016, huku shule kumi bora zilizofanya vizuri kitaifa zote zikiwa za binafsi.
Watahiniwa kumi bora wote nao walitoka shule za binafsi. Asilimia kubwa ya shule zilizoshika mkia zilikuwa ni shule za serikali.
Hali hii inaonesha kuwa kuna tatizo kubwa katika utoaji elimu bora kwa shule za serikali.
FikraPevu inaweza kueleza kinagaubaga kwamba kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mitihani yao, ni “zawadi” iliyoanza kutengenezwa siku za mwanzo wanafunzi hao walipojiunga na shule za sekondari – kidato cha kwanza.
Matatizo lukuki yanayoikabili sekta hii ya elimu yamechangia kwa kiasi kikubwa shule za serikali kufanya vibaya katika matokeo hayo ya kidato cha nne.
Sababu hizo 10 ni hizi zifuatazo:
Mosi, madai ya walimu dhidi ya serikali ambayo yamelimbikizwa miaka nenda rudi. Theluthi ya watumishi katika kada hii ambao ni walimu wanaidai serikali malimbikizo yao, ambayo ni nyongeza za mishahara, posho, pesa za likizo, pesa za kujikimu na pesa za uhamisho.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba ameiambia FikraPevu kuwa walimu wote wanaidai serikali Zaidi ya Sh. 800 bilioni ambazo bado hazijalipwa.
Hata hivyo, serikali imekuwa ikidai kuwa imeshalipa madeni ya walimu na kwamba yale yanayodaiwa, mengi, ni yale yenye utata.
Ni ukweli kwamba madai haya ya walimu, yanasababisha morali ya walimu kushuka na kusababisha ufundishaji kuwa mbovu na usioridhisha. Walimu wengi wanajikuta wakishughulika na shughuli za pembeni kama vile kuendesha bodaboda, ili tu kuweza kumudu hali ya kimaisha.
Pili, kumekuwepo na ahadi lukuki kwa walimu kama vile nyumba bora za kuishi, ambayo haijatekelezwa kwa kiasi kikubwa.
Hali hii inasababisha walimu wanaoishi mbali na maeneo ya shule kufika kazini wakiwa wamechoka, hivyo kupunguza kasi ya kufundisha kwa ubora.
Tatu, uhaba wa walimu wa sayansi, maabara na wataalamu wa maabara, umesababisha kushindwa mitihani kwa wanafunzi wa shule za serikali.
Asilimia 90 ya shule za kata hazina maabara na zile zilizobahatika kuwa na maabara hazina vifaa vinavyohitajika.
Kuna baadhi ya wanafunzi wa shule za serikali wamefanya mitihani ya mbadala wa vitendo (alternative to practical) kwa kukosa vyumba vya maabara. Wataalamu wa maabara pia ni wachache kulingana na uhitaji.
Shule ya Sekondari Kiboriloni iliyopo Manispaa ya Moshi Mjini, Kilimanjaro haina mwalimu wa fizikia kwa kidato cha kwanza, badala yake kuna mwalimu anayefika kila siku ya ijumaa na kufundisha kutoka shule nyingine.
Wanafunzi hawa wa kidato cha kwanza wanajikuta wakikosa kabisa msingi wa somo hili, hali inayosababisha matokeo mabovu ya kidato cha nne kwa somo husika.
Nne, mazingira mabovu ya kufundishia na kujifunzia yamesababisha pia shule za serikali kufanya vibaya katika mtihani huu wa kidato cha nne.
Uhaba wa vifaa rahisishi vya walimu hasa wa sayansi, vilikuwa ni vichache mno, ubovu wa madarasa, baadhi ya shule wanafunzi walikuwa wanakaa chini, kulikuwa pia na upungufu wa vyumba vya madarasa, upungufu wa matundu ya vyoo.
Tano, sababu nyingine ni uhaba wa maji shuleni, uhaba wa maktaba na vitabu, ukosefu wa umeme kwa shughuli za maabara pamoja na ukosefu wa ofisi za walimu zinazokidhi mahitaji.
Sita, motisha kidogo wanayopata walimu, hasa wale waliofanikiwa kufaulisha wanafunzi wengi, inachangia walimu kupunguza jitihada walizokuwa wakiziweka kuhakikisha ufaulu unaongezeka.
Mfano shule ya sekondari ya serikali ya Kisimiri, iliyopo mkoani Arusha, iliongoza katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2015. Walimu wao walipongezwa ikaishia hapo.
Hawakupewa zawadi, hawakutangazwa majina yao kama mashujaa waliokomboa elimu. Hii iliwafanya wakate tamaa.
Kivipi wataendeleza jitihada zao kama serikali haikutambua mchango wao? Kulikuwa na utaratibu wa shule kuwapa zawadi wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya ndani, huku wale kumi bora wakitajwa na kusimama mbele ya shule wakipongezwa.
Hali hii ilisaidia sana kuleta jitihada na mashindano miongoni mwa wanafunzi na ilichangia kuongeza ufaulu. Sasa hivi mfumo huu haupo tena.
Saba, siasa kuingilia elimu imechangia anguko la ufaulu kwa shule za sekondari za serikali nchini. Wanasiasa wamekuwa na “mchezo” wa kuitumia elimu kama daraja la kisiasa.
Wanasiasa wanakaa ofisini na kubadili mitaala, huku wakiwaachia walimu kazi za kuifundisha bila mafunzo yeyote.
Wanasiasa na viongozi wengine, hasa wakuu wa wilaya wamekuwa wakiwaonea walimu, kwa kuwaingilia majukumu yao, kuwaadhibu na kadhalika.
Imewahi kutokea Mkurugenzi wa Wilaya ya Misungwi, Mwanza, kumwamuru mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Shilala, Hamis Sengo, kudeki darasa zima, mbele ya wanafunzi wake.
Haiwezekani kabisa mwalimu huyu akabaki na morari aliyokuwa nayo mwanzo, kuendelea kufundisha kwa moyo.
Hatua za namna hii zinasababisha walimu wengi kukata tamaa na kujikuta wakifanya kazi kwa uoga hali inayochangia matokeo mabovu.
Kuruhusu wanafunzi wenye alama za chini kuingia kidato cha kwanza imesababisha pia matokeo mabovu kwa shule za serikali.
Shule zote za binafsi zina utaratibu wa kuwa na mitihani ya uchujaji na viwango vya juu vya alama zinazomwezesha mwanafunzi kuingia kidato cha kwanza.
Kwa shule za serikali, Serikali ilishusha kiwango cha alama zinazoruhususiwa ili mwanafunzi aweze kujiunga kidato cha kwanza.
Nane, msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ni sababu inayochangia ubovu wa matokeo ya kidato cha nne. Asilimia 99 ya wanafunzi wa shule za sekondari za serikali, wamesoma shule za msingi za serikali, ambazo hazifundishi “kwa nguvu” somo hilo. Masomo mengine hufundishwa kwa Kiswahili.
Hii inamaanisha wanafunzi wengi wa shule za serikali wana msingi dhaifu wa Kiingereza. Leo hii mwanafunzi wa kidato cha nne anashindwa hata kuandika insha ya zaidi ya maneno 100 kwa lugha hiyo ya kigeni.
Katika mitihani, wanafunzi wengi wanajua vitu vingi kwa Kiswahili, lakini hawayajui kiingereza, hii inafanya wasijue swali linauliza nini.
Laiti kungekuwa na msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza, wengi wangefaulu kwani mambo mengi ya shule ya msingi hujirudia sekondari kwa lugha nyingine.
Tisa, shule za kutwa ni chanzo cha ubovu wa matokeo hayo. Shule nyingi za serikali hasa za za kata ni za kutwa.
Wanafunzi hujikuta muda mwingi wakiwa nyumbani tofauti na wale wa bweni. Wale wanaorudi nyumbani hushiriki katika shughuli zinazoathiri taalauma kama vile kucheza kamari, kuangalia luninga, kunywa pombe, kushiriki mapenzi na kuvuta bangi.
Wanafunzi wa shule za kutwa hasa za mijini, wamekuwa wakiteseka na umbali uliopo kati ya shule na majumbani mwao.
Wengi wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita tano huku wale wa Jiji la Dar es Salaam, lililoshika nafasi ya mwisho kitaifa, wamekuwa wakitumia muda mwingi “wakigombea au kuwa vituoni” wakisubiri daladala, hivyo kujikuta wakichelewa kuanza masomo na kukosa baadhi ya vipindi. Hali hii inaathiri taaluma na kusababisha matokeo mabovu kwa shule hizi.
Kumi, ukata unaozikabili shule za serikali umechangia kwa kiasi kikubwa matokeo mabovu kwa shule hizo.
Kutokana na ukata, shule zimeshindwa kuandaa mitihani ya kutosha ya majaribio ukilinganisha na shule binafsi ambazo huwa na mitihani kila mwisho wa wiki.
Ukata huu husababisha pia wanafunzi kushindwa kupata chakula kizuri shuleni, kukosa baadhi ya vifaa vya kufundishia na mahitaji mengine muhimu.
Serikali inatakiwa kujitathmini upya katika suala hili la elimu. Katika awamu hii ambayo Rais Dk. John Magufuli, makamu wake, Samia Suluhu Hassan na waziri mkuu, Kassim Majaliwa- wote waliwahi kuwa walimu, serikali inategemewa ifanye vizuri kwenye sekta ya elimu.
Elimu ya Tanzania inahitaji mabadiliko kufikia malengo na kusaidia nchi kuwa na wataalamu wa kutosha kuinua uchumi.
Serikali inatakiwa kukabiliana na changamoto hizo ili kurudisha hadhi na ubora wa shule zake na kuhakikisha shule binafsi nazo hazibweteki ili kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza wanafaulu na baadaye kuwa na msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi na watu wake.