Serikali inapoteza bilioni 793 za walimu ‘watoro’

Jamii Africa

 Utafiti wa taasisi ya Twaweza unaeleza serikali inapoteza bilioni 793 kila mwaka  za mishahara ya walimu wa shule za msingi  ambao hawatimizi majukumu yao ya kufundisha wanafunzi na kuhudhuria shuleni.

Akitoa matokeo ya utafiti huo uliobeba dhima ya ‘Kuwalipa walimu bahshishi kwa matokeo ya kujifunza’, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema  katika uchunguzi walioufanya katika wilaya 10 za Tanzania wamebaini kuwa serikali inapoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na baadhi ya walimu kutowajibika ipasavyo katika ufundishaji.

“ Tunapoteza kila mwaka bilioni 793 ya mishahara ya walimu ambao hawaingia shule au darasani.  Ukilinganisha kiasi hiki na shilingi bilioni 306 zilizopotea mwaka 2014 katika kashfa ya IPTL Escrow na kuzua mtafuruku mkubwa nchini, upotevu wa fedha kupitia mishahara ya walimu wa shule za msingi ni mara mbili ya hasara iliyotokana na kashfa hiyo ya Escrow. Na kiasi hiki hupotea kila mwaka”, amesema Eyakuze.

Amesema  mazingira yasiyoridhisha ya kujifunzia na kufundishia katika shule za msingi, yamekuwa kikwazo kwa walimu kuhudhuria shuleni . Hali hiyo inatajwa kuathiri wanafunzi kuelimika na kupata stadi muhimu za maisha.

“Mahudhurio ya walimu darasani ni changamoto nyingine . Mwaka 2015 asilimia 31 sawa na Mwalimu  1 kati  3 hayuko shuleni  lakini imepungua kidogo hadi asimilia 27 mwaka 2016.  Hapo tena mwaka 2016 mwalimu 1 kati ya watatu  yuko shuleni lakini hayupo darasani anafanya mambo mengine ya kiutendaji halafu asilimia 41 wako darasani”, amesema Eyakuze.

Imebainishwa kuwa walimu wakipewa motisha ya fedha au ujuzi, mahudhurio yao shuleni yawaweza kuongezeka na kuwafaidisha wanafunzi kwa kupata  matokeo mazuri katika masomo yao.

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika utolewaji wa matokeo ya utafiti wa KIUFUNZA jijini Dar es Salaam leo

 

Motisha kwa walimu

Katika utafiti wa Twaweza ulifanyika chini ya mradi wa ‘KIUFUNZA’ ambao unachochea kiu ya kujifunza katika shule za msingi kwa kutoa matisha ya fedha kwa walimu, unaeleza kuwa kuna uhusiano wa karibu katika ya motisha na ufanisi wa mwalimu katika ufundishaji.

“Tumetumia njia mbalimbali za kuwamotisha walimu kwa kutumia malipo ya fedha baada ya matokeo ya kujifunza kudhihirika; mfumo ambao unahusisha malipo kwa walimu na stadi ambazo watoto wao wamejifunza”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya KIUFUNZA.

Mradi huo wa majaribio ulifanyika katika wilaya 10 za Tanzania Bara mwaka 2015-2016, ambapo shule zilizochaguliwa ziliingizwa katika mpango huo wa miaka 2 na kuwaahidi walimu ambao watajitolea kufundisha wanafunzi kupata stadi muhimu za kuandika na kusoma wangepata motisha ya fedha kulingana na matokeo ya ufundishaji.

“Mwaka 2015-16 tumepata matokeo chanya kwenye matokeo ya wanafunzi katika shule ambazo Twaweza ilitoa malipo haya. Hii tuna maanisha kuwa tuna uthibitisho kuwa motisha ya fedha inaweza kuwahamasisha walimu kuboresha utendaji wao na kuwasaidia wanafunzi wao kujifunza”, inaeleza ripoti hiyo.

Mradi huo wakati unaanza katika shule husika ulibaini kuwa asilimia 30 ya wanafunzi ambao wanahudhuria shuleni hawajifunzi stadi muhimu, lakini walipoanza kutekeleza mradi huo waligundua mafanikio kwa mwanafunzi mmoja mmoja hata kwa wale ambao walikuwa hawapati maarifa ya msingi.

Mwalimu Joseph Mbando, ambaye ni mmoja wa watafiti katika mradi huo anasema  walilenga wanafunzi wa darasa la I, II na III katika masomo ya Kiswahili na Hisabati ambapo motisha hiyo ilitolewa kwa mwalimu mmoja mmoja sio kwa uongozi wa shule kama inavyofanywa na serikali kupitia ruzuku inazozitoa.

“Pale ambapo bahshishi na ruzuku vilichanganywa, matokeo ya kujifunza katika madarasa ya I, II na III, yalikuwa ni mazuri: tulibaini kuwa viwango vya ufaulu wa Kiswahili na Hesabu viliongezeka kwa asilimia 20 katika kipindi cha mwaka mmoja”, anaeleza Mwalimu Mbando katika ripoti hiyo.

Licha ya Twaweza kutekeleza mradi huo, serikali inatoa ruzuku kwa shule zote nchini ili kugharamia mahitaji ya wanafunzi na walimu waliopo shuleni lakini ruzuku hiyo haiwalengi walimu wanaoonyesha juhudi za kuwasaidia wanafunzi.

Mwalimu Joseph Mbando kutoka Twaweza akiongea katika utolewaji wa matokeo ya utafiti wa KIUFUNZA

 

Walimu wanena

Mwalimu Sada Ally kutoka shule ya msingi Mpakani iliyopo Manispaa ya Ubungo anasema  motisha hiyo ya KIUFUNZA imechochea walimu wengi kufundisha kwa bidii kwasababu waliahidiwa kupata kiasi Fulani cha fedha ambacho kimewasaidia katika shughuli za kiuchumi.

Ameongezeka kuwa matokeo ya wanafunzi katika shule yake yamekuwa mazuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo motisha ilikuwa haitolewi.

Naye Mratibu Msaidizi wa KIUFUNZA Wilaya ya Kinondoni/Ubungo amesema mradi huo umekuwa ni chachu ya walimu kufundisha licha ya mazingira yasiyoridhisha yaliyopo katika shule za msingi nchini Ameiomba serikali itoe ushirikiano kwa taasisi za kiraia zinazojitolea kuinua ubora wa elimu.  

 

Wadau wa elimu watoa maoni yao

Mshauri wa Elimu kutoka Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Beatrice Omari amesema  utafiti huo ni mwanzo mzuri katika kutatua changamoto za elimu lakini ungekuwa na nguvu kama ungeongelea motisha zingine na kutambua juhudi za serikali za kuinua kiwango cha elimu nchini ikiwemo ruzuku kwa wanafunzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Tathmini ya Mitihani cha Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Alfred Mdima amesema utafiti huo haujaelezea kwa kiasi gani motisha ilipunguza asilimia 30 ya wanafunzi ambao hawajifunzi wakiwa shuleni.

Hata hivyo, ripoti hiyo inatoa hitimisho la jumla kwamba motisha kwa walimu imeboresha kujifunza katika maeneo mbalimbali lakini pia aina ya muundo na taratibu za utekelezaji yana umuhimu mkubwa sana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *