‘Hatuna daktari kwa miaka saba’

Kulwa Magwa

ZAHANATI ya kijiji cha Magalata, wilayani Kishapu, imekuwa ikitoa huduma kwa miaka saba chini ya wauguzi wasaidizi wawili ambao kitaaluma hawapaswi kutibu wagonjwa.

Akizungumza katika kijiji hicho, hivi karibuni, muuguzi wa zahanati hiyo, Zuhura Suleiman, alisema wamekuwa wakitoa huduma zote kama madaktari licha ya kwamba hawajasomea taaluma hiyo.

Zuhura-Suleiman

Zuhura Suleiman

Zuhura ambaye alihamishiwa kwenye zahanati hiyo, mwaka 1997, alisema alifanya kazi na daktari aliyekuwepo hadi mwaka 2006 ambapo tabibu huyo alihamishiwa sehemu nyingine.

Alisema tangu wakati huo wamekuwa wakifanya kazi zote wakiwa wawili, na kwamba wamezizowea na huzitekeleza kama madaktari waliosomea taaluma hiyo.

Muuguzi huyo alifafanua kwamba, wamezowea kutibu wagonjwa wenye matatizo mbalimbali, kuzalisha wajawazito na pia kuhudumia wajawazito na watoto wadogo.

Wodi-Kishapu

Wodi ya wagonjwa ya zahanati ya Magalata, wilayani Kishapu

“Hata hivyo tunachofanya ni kusikiliza tu historia za wagonjwa ndipo tunawatibu kwa kuwapa dawa, lakini hatuwapimi wagonjwa kwa kuwa hatujui,” alisema Zuhura.

Alisema siku yao ya kazi huanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri ambapo hutibu wagonjwa kati ya 20 hadi 25, na wakati mwingine huwa wengi zaidi hasa wakati wa mvua.

“Wakati wa mvua kuna magonjwa mengi kama kuhara, malaria na mengineyo na ukifika wakati huo huwa tunatibu watu hadi 30 na zaidi, “anasema.

Akizungumzia matatizo ya kazi wanayokumbana nayo, Zuhura anasema kuwa ni pamoja na uhaba mikasi, glovu na pamba – vinavyotumika wakati wa kujifungulia.

vifaa-magalata

Baadhi ya vifaa ya kupimia wagonjwa vya zahanati hiyo

“Dawa za chanjo zipo za kutosha, mipira ya kujifungulia nayo tunayo ila vitendanishi vya VVU huwa vinapungua kipindi fulani na kimsingi huwa tunazalisha wajawazito sita hadi wanane kwa wiki na wakati mwingine kwa mwezi,” anasema muuguzi huyo.

Hata hivyo, Zuhura anasema kila siku wanapokea wajawazito hadi wanane wanaoanza kliniki, wakiwemo wanaotoka vijiji vya jirani.

Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Japhet Makelele, anasema kuna upungufu mkubwa wa madaktari wilayani humo, suala ambalo linazifanya zahanati nyingi kuhudumiwa na wauguzi.

Kwa mujibu wa ikama ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya mwaka 1999, zahanati inapaswa kuwa na maofisa tatibu wawili, wauguzi wawili na mhudumu msaidizi wa afya mmoja.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *