Unapenda kujilaza kitandani kwa muda mrefu? Hizi ndizo athari za kiafya unazoweza kuzipata

Jamii Africa

Kulala kwa muda mrefu kunahusishwa na matatizo ya kuharibika kwa ngozi na kupata maumivu ya viungo hasa mgongo. Pia kujilaza kitandani muda mrefu huusishwa na matatizo ya msongo wa mawazo, mkazo (stress) na matatizo mengine ya kisaikolojia ambayo huweza kusababisha matatizo ya moyo.

Watu wengi duniani huwa hawanyanyuki kutoka kitandani mara tuu wanaposikia alamu zao bali hujigeuza geuza kwanza. Hali hii imekuwepo kwa muda mrefu tangu karne za zamani na sasa hivi hali imezidi kutokana na maendeleo ya teknolojia.

 

Je, tabia ya kujilaza kitandani kwa masaa mengi zaidi ukijinyoosha ni nzuri kiafya?

Mwaka 2014, Shirika la Marekani la sayansi ya anga (NASA) walifanya utafiti kuhusu asili ya mifupa na jinsi inavyoharibika pale binadamu anapokuwa kwenye anga. Utafiti huo ulifanywa na mwanasayansi Drew Iwanicki ambaye alijitolea kulala kitandani kwa siku 70 bila kunyanyuka kufanya chochote kile (isipokuwa pale alipojigeuza na kulala ubavu ili aweze kula).

Japokuwa utafiti huo ulimuwezesha kulipwa dola za Marekani18,000 lakini kulala kwa siku zote hizo haikuwa kazi rahisi. Mtu anapolala huku miguu ikiwa imeinuliwa kwa kiasi fulani husababisha damu nyingi kusambaa kwenye kichwa na uso kuvimba.

                              Drew Iwanicki alipokuwa amelala kwa ajili ya utafiti

 

Je, kuna madhara kulala kitandani siku nzima?
Jibu ni ndiyo. Kulala kwa muda mrefu huweza kudhoofisha afya yako. Kulala kifudifudi pekee sio tu huleta matatizo bali kulala kwa mtindo wowote ule kwa siku nzima huweza kukuletea matatizo ya kiafya. Kuna baadhi ya mazingira ambayo mtu hujikuta amelala kwa saa 6 mpaka 7 bila kujigeuza kwa namna yoyote au kujisogeza kidogo tu kwa kujikuna au kujiweka sawa.

Unapolala muda mrefu bila kujigeuza huweza kukusababishia vidonda vya tumbo vitokanavyo na shinikizo la damu au huweza kupata ugonjwa wa ngozi (bedsores) kwa sehemu ile unayoilalia muda mrefu kukosa mzunguko wa damu vizuri.

Ugonjwa huu wa ngozi upo katika hatua mbalimbali na unapofikia hatua ya 4 huweza kuharibu mifupa na hata kuweza kusababisha kifo, ndiyo maana wahudumu wa afya huwageuza wagonjwa waliopooza mwili mzima mara kwa mara.

 

Madhara ya kujilaza kwa muda mrefu
Hata kama ugonjwa huo wa ngozi (bedsores) usingekuwepo bado kujilaza kwa muda mrefu kuna madhara mengine ya kiafya. Utafiti uliotolewa mwaka 2004 na kuchapishwa kwenye jarida moja la mifupa, uti wa mgongo na maungio ya mifupa ulibaini kuwa watu waliokuwa na matatizo ya mgongo ambao walishauriwa na madaktari kulala kama njia mojawapo ya matibabu walijukuta wakiwa na maumivu makali zaidi ya mgongo kwa asilimia 32 zaidi ya yale ya mwanzo.

Utafiti mwingine uliochapishwa kwenye Jarida la Saikolojia mwaka 2008 ulihusisha panya ambao walilazwa kwenye mtindo ambao binadamu hulala na baada ya wiki 2 panya hao walianza kuonesha hali ya kupata msongo wa mawazo na mkazo (stress). Na baadaye walianza kupata matatizo ya kisaikolojia na athari kwenye moyo, hii yote ni kwasababu walilazwa kwa muda mrefu.

Madhara sio makubwa sana lakini…
kulala kwa muda mrefu sio vibaya ikiwa mtu atalala kwa kiwango kinachotakiwa. Inaweza kuwa jambo zuri hasa kwa wale ambao wamepata matatizo kwenye ubongo, kwasababu husaidia ubongo kuweza kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

Kwa faida yako mwenyewe usijilaze kitandani bila sababu yoyote ya msingi, ni vizuri kunyanyuka na kutembea ili uone dunia inavyokwenda na kusaidia viungo vya mwili kuwa imara kutekeleza majukumu muhimu ya kikazi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *