Serikali ya Tanzania imeshauriwa kutengeneza mifumo imara ya kitaasisi itakayosimamia utolewaji wa huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kupunguza vifo vya watoto hao ambavyo vinaongezeka kila mwaka.
Kauli hiyo ya wadau wa afya ni mkakati maalumu wa kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ikizingatiwa kuwa vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (pre-mature babies) vinashika nafasi ya pili baada ya vile vinavyotokana na maambukizi mbalimbali.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Kila mwaka duniani kote inakadiliwa watoto milioni 15 wanazaliwa kabla ya muda na idadi hiyo inaongezeka kila mwaka. Mwaka 2015 pekee nchini Tanzania watoto 236,000 walizaliwa kabla ya muda ambapo waliofariki walikuwa 9,400 ndani ya mwezi mmoja tangu kuzaliwa kwao.
Kutokana na ongezeko la vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakusudia kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kuanzisha vitengo maalumu katika hospitali zote nchini ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa na wahudumu waliopitia mafunzo maalumu ya kuwatunza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Ulisubisya Mpoki amesema wototo wanaozaliwa kabla ya wakati ni matokeo ya kutokuwa na huduma bora za mama na mtoto na uhaba wa watumishi wa afya wenye ujuzi wa kuwahudumia watoto hao pindi wanapozaliwa.
“Taarifa za kitakwimu tulizonazo kwa 2015 peke yake zinaonyesha Tanzania hapa tulipata watoto 236,000 ambao walizaliwa kabla ya kutimiza siku 37 za kukaa katika matumbo ya mama zao. Katika hao watoto 9,400 walifariki”, anaeleza Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa,
“Sababu ya kufariki kwao ni watu kutokuwa na ujuzi wa namna ya kuwahudumia lakini vilevile vifaa vya kutolea huduma na mahali maalumu panapoweza kukidhi mahitaji ya watoto hao ambao walitakiwa kuendelea kubaki katika matumbo ya mama zao lakini kwasababu moja au nyingine wakapata hayo matatizo”.
Serikali inaandaa mfumo rasmi wa kukabiliana na changamoto ya vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ikiwemo utolewaji wa elimu kwa wafanyakazi wa afya na akina mama juu ya njia sahihi za kuwatunza watoto hao ili wakue kama watoto wengine.
“Wataalamu wa sayansi kutoka katika vyuo vikuu walikuwa wanaliaangalia tatizo hili kwa kipindi kirefu, wakagundua kwamba ni lazima tuweke mifumo itakayosaidia kupunguza shida hiyo”, anaeleza Dkt. Mpoki ambapo wanashirikiana na Shirika la Misaada la Ujerumani (GIZ) kufanya tafiti, kutoa mafunzo na kujenga majengo yenye vifaa maalumu vya kuwatunza watoto hao ili kuwaepusha na vifo vinavyozuilika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Dkt. Ulisubisya Mpoki (Kushoto) akiwa na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dkt. Detlef Wachter mapema leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watoto Wanaozaliwa Kabla ya Wakati (Prematurity Day) zilizofanyika katika Hospitali ya Ocean Road.
Mtwara na Lindi wafanikiwa kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati
Wataalamu kutoka shirika la GIZ mwaka 2015 walifanya utafiti nchini na kugundua mikoa ya Lindi na Mtwara ina huduma duni za afya ya mama na mtoto ambapo ndio sababu kubwa ya vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. Kwa kushirikiana na Mamlaka za afya katika mikoa hiyo walianza kuchukua hatua muhimu ikiwemo kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga katika vituo vyote vya afya.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Wedson Sichalwe amesema walipata msaada wa kiufundi kutoka shirika la GIZ ambapo tangu mwaka 2015 wametoa mafunzo kwa wauguzi na akina mama, vifaa maalumu katika vituo vya afya na hospitali za Mtwara na Lindi.
“Ndani ya miaka 2, mikoa yote miwili imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa watoto wachanga na kupunguza vifo vya watoto hospitalini kwa 38% (kutoka vifo 32 kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa mpaka vifo 20)”, anaeleza Dkt. Sichalwe, “Hata hivyo, watoto wengi waliozaliwa kabla ya muda wanakuwa katika afya nzuri bila kuwa na ulemavu wa muda mrefu”.
Njia mbalimbali hutumika kumtunza mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati ikiwemo njia ya Kangaroo ambayo mtoto huwekwa kwenye ngozi ya mama yake ili kumuongezea joto na kuimarisha uhusiano. Pia kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa ili kumkinga na maambukizi ya magonjwa na kifo.
Kutokana na mradi huo wa kuboresha huduma za mtoto, hospitali zote 14 za Mkoa na Wilaya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara zina kitengo maalumu cha kutunza watoto wanaozaliwa, ambapo wafanyakazi 286 wamepewa mafunzo na kusimamiwa katika majukumu yao ya kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Pia wahudumu wa afya 990 kutoka vituo vya afya 35 na Zahanati 160 katika mikoa hiyo walipata mafunzo ya kuwahudumia watoto wanaozaliwa na wanaendelea kupata msaada wa kiufundi kila mara ili kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anakuwa salama.
Naye Meneja Programu wa Shirika la GIZ kwa nchi ya Tanzania, Dkt. Susanne Grimm amesema wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika sekta ya afya kuboresha huduma za mama na mtoto kwa kutoa msaada wa kiufundi kwa wataalamu wa afya nchini.
Msaada huo unajumuisha jinsi ya kutumia gesi ya oksijeni kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo kwenye mfumo wa upumuaji, itifaki ya kuzuia na kutibu tatizo la kushuka kwa sukari kwenye damu na watoto wenye matatizo ya anemia.
“Mchakati huo unahitaji wataalamu wa afya waliofunzwa, vifaa vya kisasa, usambazaji mzuri wa dawa na eneo maalumu la hospitali lililotengwa”, amesema Dkt. Grimm.
Mafanikio yaliyopatikana Mtwara na Lindi ni hatua ya kwanza kuelekea safari ndefu ya kupandana na vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda nchini Tanzania.
Mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati akiwa katika chupa maalumu
Watoto wanaozaliwa kabla muda (Premature babies)
Watoto hao ni wale wanaozaliwa kabla ya wakati kuanzia wiki 28 hadi 34, uzito wao huanzia gramu 500 hadi 1,500.
Sababu zinazosababisha watoto wengi wazaliwe kabla ya wakati ni pamoja na wajawazito kuwa na shinikizo la damu, kifafa cha mimba, upungufu wa damu, maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU). Pia magonjwa ya zinaa, mama kutokwa na damu kabla mimba haijakomaa, malaria, mimba za utotoni, utumiaji wa vilevi mfano pombe, sigara na dawa za kulevya pamoja na kufanya kazi ngumu wakati wa ujauzito.
Tafiti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) zinaeleza kuwa kila siku zaidi ya watoto wachanga 100 hufariki nchini Tanzania kutokana na maambukizi, matatizo yanayojitokeza wakati wa kuzaliwa kama vile kupumua kwa shida na matatizo yanayotokana na kuzaliwa kabla ya muda. Vifo vya watoto wachanga vinachangia hadi asilimia 40 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Novemba 17 kila mwaka Dunia huadhimisha Siku ya Watoto Wanaozaliwa kabla ya Wakati (Prematurity Day) ambapo Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la GIZ wamekutana na wadau mbalimbali jijini Dar es salaam kujadili hatua iliyofikiwa katika kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.