KUWAPO kwa masoko yasiyotumika katika Halmashauri ya Iringa na Manispaa ya Iringa, pamoja na kujengwa kwa thamani kubwa ni ishara ya wazi kwamba yalijengwa kinyume na kipaumbele halisi cha wananchi wa wilaya hizo.
Miradi mingi ambayo huanzishwa kwa matakwa ya wananchi wenyewe huwa mkombozi kwa wananchi wanaozunguka miradi hiyo na hata baadhi ya miradi kufanikisha kuwakomboa wananchi hao na hali duni ya maisha.
Ukitazama sera za miradi yenye ushiriki wa wananchi kama TASAF na hata DADS wananchi wanapaswa kuchangia nguvu zao katika uanzishwaji wa miradi hiyo nah ii ndio siri kubwa ya mafanikio ya miradi hiyo katika utekelezaji na matumizi yake.
Katika utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika miradi ya ujenzi wa masoko kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Iringa vijijini imebainika kuwepo kwa baadhi ya masoko ambayo yalijengwa kati ya mwaka 2007 hadi 2009 hayatumiki.
Masoko haya kimsingi yamebaki kuwa makazi ya ndege na wanyama wa porini kutokana na kutotumika na wananchi wanaozunguka masoko hayo.
Sarah Sanga ni mkazi wa Tagamenda katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini anasema kuwa Halmashauri hiyo ilipata kuwajengea soko lililokamilika mwaka 2009 .
Soko hili kwa mujibu wa mwananchi huyo lilifanya shughuli zake kwa wiki mbili kabla ya kuondoka na kurudi katika eneo lao la mwanzo.
Anasema kuwa tatizo lililopelekea kutoendelea na biashara katika soko hilo ni kuwa mbali na makazi ya watu na hivyo kukosa wateja japo wananchi walishirikishwa katika ujenzi japo baadhi walikuwa wakipinga soko hilo kujengwa eneo hilo ambalo ndilo ardhi ilipatikana .
“Hili soko sisi tulipendekeza lijengwe eneo letu la biashara ambalo ni mita kama 800 kutoka eneo hilo ila wao walilazimisha kujengwa hapa ….lakini tunajengewa soko bila kupewa mitaji tutauza nini hapa sokoni wakati sisi biashara zetu ni za magengeni na si za kuweka sokoni kama wao walivyotujengea soko.”
Hata hivyo alisema ni vema eneo hilo la soko ili kuweza kuwavuta wateja zaidi na wafanyabiashara wakageuza majengo hayo ya soko kuwa klabu cha pombe za kienyeji ambayo ndio ina soko kubwa katika kijiji hicho.
Naye Lusajo Kalinga mkazi wa kijiji cha Muwimbi anasema kuwa wanashindwa kujua sababu ya serikali kujenga soko eneo la Ulete wakati wakijua mahitaji yao eneo hilo hayakuwa ni soko bali maji safi na salama ya bomba kwa kipindi hicho .
Hivyo alisema sababu ya kushindwa kuendelea kwa soko hilo ni kutokana na wananchi kutokuwa na tabia ya kuuza biashara zao kwenye jengo la soko huku kila mmoja akiuza kivyake mitaani na baadhi huuza bidhaa zao katika klabu cha pombe.
Zuwena Mussa mmoja kati ya wananchi wanaojishughulisha na biashara ndogo nje ya soko la Magari mabovu kata ya Miyomboni Kitanzini katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa anasema kuwa soko hilo linaendelea kuchakaa bila wafanyabiashara kutumia kutokana na wafanyabiashara kulipishwa ushuru wa Tsh 500 pale wanapoingia kufanya biashara katika soko hilo huku biashara zao utokaji wake ukiwa mdogo zaidi.
Mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Aman Mwamwindi akizungumzia matumizi ya masoko, alitolea mfano soko la Magari Mabovu ambalo limejengwa na Halmashauri kwa msaada wa SIP kupitia mradi wa Mazingira.Alisema upo mkakati wa kulifufua soko la samaki kwa kuwaondoa wauza samaki wote mitaani na kuwapeleka eneo hilo.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tagamenda Joel Mofuga anasema kuwa soko la Tagamenda kuchakaa kwake kunatokana na wakazi hao kugoma kufanyia biashara katika soko hilo na badala yake kuendelea kulipa ushuru wa Tsh 500 kwa mtu binafsi ambae anamiliki nyumba aliyoijenga kama sehemu ya matumizi ya klabu cha pombe za kienyeji ambalo ni eneo lililochangamka zaidi.
Mofuga anasema kuwa hivi sasa mkakati wa kijiji hicho katika soko hilo ni kupigania kuingiza umeme katika majengo hayo ili kubadili matumizi ya soko na kuweka shughuli kama za uungaji wa vyuma ,mashine za kukamua alizeti na shughuli nyingine rafiki na wananchi badala ya kuendelea kuliacha soko hilo likiendelea kuchakaa.
Hata hivyo anasema mradi ambao ungeweza kuwakomboa wananchi wa eneo hilo ambao wengi wao ni wakulima ulikuwa ni mradi wa bwawa la maji ambalo lingeweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji na kuwaongezea kipato zaidi wananchi wa eneo hilo.
Abel Mgimwa ambaye ni afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo anasema Halmashauri yake ina masoko matano ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa DADS na masoko matano mengine yamejengwa kwa ufadhili wa mradi wa DADPS .
Anataja masoko ambayo yamejengwa na DADS kuwa ni Muwimbi, Ifunda kibaoni , Ilolompya,Itunundu na Tungamalenga na kuwa kati ya masoko hayo ni masoko mawili ambayo hayatumiki kabisa likiwemo soko la Muwimbi na Ilolompya wakati mengine yanatumika vema.
Kwenye mradi wa DADPS masoko yaliyojengwa ni Tagamenda , Ng’enza,Ndiwili , Luganga na Kitayawa na kuwa masoko ambayo hayatumiki baada ya kujengwa ni Tagamenda na Ndiwili wakati yaliyobaki yanatumika japo si kwa asilimia kubwa .
Mgimwa ambae ndie alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi wa masoko hayo anasema kuwa ujenzi huo umeanza kati ya mwaka 2007 na kukamilika mwaka 2009 na kuwa ukiacha soko la Ifunda Kibaoni lililojengwa kwa Tsh milioni 38. 9 masoko mengine yote yamejengwa kwa zaidi ya Tsh milioni 64 fedha kutoka kwa wahisani.
Pia anasema kuwa si kweli kama wananchi hawakushirikishwa katika ujenzi huo kwani kabla ya kuanza ujenzi vikao vilifanyika na wao kuonyesha maeneo ya ujenzi ila baada ya kujengwa ndipo walipoanza kususa kufanya biashara katika masoko hayo .
Anasema kuwa lengo la kujenga masoko hayo ni kuwakomboa wananchi ambao wengi wao ni wakulima na masoko hayo yangewasaidia kuuza mazao yao bila kuibiwa na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakinunua mazao majumbani kwa bei wanayoitaka wao .
Ofisa huyo pamoja na kueleza umuhimu wa masoko hayo amesema hataki kuamini kama fedha za ujenzi wa masoko hayo zimepotea kwani tayari Halmashauri imeanza kuunda kamati za watumiaji wa masoko hayo ili kufufua masoko yaliyokufa.
Aidha alisema anashangaa kuachwa kutumika kwa masoko hayo kwani ni vyanzo vya mapato kwa Halmashauri za vijiji kwani asilimia 20 huenda Halmashauri na vijiji hupata asilimia 80 ya makusanyo hayo.
Mratibu mkuu wa miradi hiyo Ofisa kilimo wa mkoa wa Iringa Adam Swai ambae ni katibu tawala msaidizi katika uchumi na uzalishaji anasema kuwa jumla ya masoko 23 ndio ambayo yamejengwa katika mkoa wa Iringa kabla ya kutengana na Njombe.
Hata hivyo anasema lengo la masoko hayo ni kuwakomboa wakulima katika soko na kuwa na eneo moja la kuuzia mazao yao kwa vipimo stahiki ,wazalishaji mazao na kuuza kwa bei yenye faida .
Anasema japo baadhi ya masoko uendeshaji wake si mzuri na yapo ambayo yameanza kuchakaa bila kutumia kama lile ya Ruaha Mbuyuni ,Lukani ,Magulilwa na Kitwiru mjini Iringa ambayo yote yamejengwa kwa pesa za ASDP – DADPS ipo haja ya kuwa na mikakati ya kuyafanya masoko hayo kuanza kunufaisha wakulima.