Hogo la nini?

KWA Wordson Pakyindi (30), mkazi wa Kijiji cha Kyimo wilayani Rungwe, kuvunjika mguu kutokana na ajali ya pikipiki aliyoipata Desemba 17, 2013 kulimaanisha mwanzo mpya wa maisha ya ulemavu.

Alitambua kwamba, asingeweza kupatiwa tiba na zaidi huenda angeambiwa akatwe mguu kutokana na kuvunjika vibaya, kama inavyotokea kwa wahanga wengi wa ajali za pikipiki zilizongezeka hivi sasa nchini.

“Nilijua ndio mwisho wa kutembea kwa miguu yangu miwili, kwa sababu kuna watu wengi waliopatwa na ajali za pikipiki ambao wameshindwa kupatiwa huduma ama kutokana na kutoweza kumudu gharama au kutokana na mlundikano wa majeruhi,” anasema kwa uso wenye tabasamu hafifu akiwa anaota jua nje ya nyumba ya mganga wa jadi, Anyimike Mabeja (56), mkazi wa Kitongoji cha Bwenda wilayani Ileje.

Akizimulia mkasa huo, Pakyindi anasema alikuwa anaendesha pikipiki akielekea kazini na alipofika katika eneo la  Igawilo-Uyole jijini Mbeya aligongwa na gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace na kusababisha kuvunjika mguu wa kushoto na paja kupasuka huku akiwa na jeraha kubwa ikiwa ni pamoja na kifundo cha goti kuhama katika sehemu yake.

“Baada ya ajali hiyo wasamaria wema walinibena ma kunipeleka katika Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako nilipatiwa huduma ya kwanza kwa kushonwa sehemu ya paja iliyokuwa na kidonda.

“Wakati napelekwa kwenye chumba cha kupigwa picha ya mionzi (X-Ray)nilifuatwa muuguzi aliyekuwa ananihudumia akaniambia kuwa ‘wenzio wanaokuja hapa huwa wanatoa fedha ndipo wanahudumiwa vizuri’ kauli ambayo iliniongezea maumivu,” anasema.

Anasema baada ya kupiga X-Ray alipelekwa wodini ambako madaktari walimwambia anatakiwa kuwekwa chuma bila ganzi kutokana shinikizo la damu kuwa chini (BP Kushuka).

“Nilikataa kuwa siwezi kuwekwa chuma bila ganzi kutokana na maumivu makali niliyokuwa nayapata wakati ule.

“Niliwaeleza ndugu zangu kuwa sipo tayari kuwekwa chuma bila ganzi na ndipo alipokuja kaka yangu na kuniambia kuwa huku kuna mganga ambaye angeweza kunitibu na nikapona, nilimkubalia kuja huku kwani nili kuwa siwezi kuinuka, kukaa wala kugeuka zaidi ya kulala,” anasema.

Pakyindi anasema waliondoka hospitalini hapo kwa kuwaeleza wauguzi kuwa wameamua kwenda hospitali ya Misheni Peramiho mkoani Ruvuma, wakaruhusiwa kutoka kesho yake.

“Nilipokuwa natoka rufaa hali yangu ilikuwa mbaya, huduma pekee niliyopata ni ya kushonwa kidonda ili kisiendelee kutoka damu, nilikuwa siwezi kutembea wala kutikisika nilikuwa nabebwa kama jiwe, lakini namshukuru Mungu mara baada ya kufika hapa hali yangu ni nzuri kwa sasa kama unavyoniona, naweza kuinuka peke yangu na kutembea kwa kutumia magongo,” anasema.

Anasema baada ya kufika hapo mganga huyo aliunganisha mfupa bila ya kuwekwa chuma na goti kulirudisha sehemu yake na kwa sasa kidonda kimepona kilichobaki ni goti ambalo limesababisha atumie msaada wa magongo kutembea.

“Namshukuru sana huyu mganga kwani ameokoa maisha yangu, ningeweza kupata ulemavu wa maisha, ameniambia kwamba muda si mrefu ninaweza kurudi nyumbani kuendelea na kazi zangu… najiona nimepona, ni hili goti ndiyo bado kidogo,” anasema.

Pakyindi ni mmoja wa majeruhi wengi wa ajali za pikipiki zinazotokea nchini ambao wamepoteza viungo vyao huku wananchi wengi wakipoteza maisha.

Pamoja na ukweli kwamba ajali za barabarani zimekuwa zikitokea muda mrefu zikisababishwa na magari, lakini hivi sasa ujio wa pikipiki, maarufu kama Boda Boda, ndio umesababisha wimbi kubwa la ajali hizo ambazo zimeacha wengi wakiwa na ulemavu wa maisha kutokana na wengi wao kukatwa viungo vyao baada ya kuonekana haviwezi kutibika tena.

Hali hii imesababisha kupungua kwa nguvu-kazi kwani wengi wa wanaopata ajali hizo ni vijana ambao ndio mhimili wa uchumi wa taifa pamoja na familia.

Licha ya kuwepo kwa hospitali na madaktari bingwa bado matumaini ya wananchi kupona yamekuwa madogo kutokana na kukithiri kwa madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa vinavyosababishwa hasa na uhaba wa watalaam hao, hivyo kuwa kikwazo kwa watu wa kawaida kupata tiba stahiki.

Hata hivyo, tumaini jipya linaweza kuwa limepatikana kutokana na kuibuka kwa mtaalam wa tiba mbadala ya kuunganisha mifupa na kutibu majeraha kwa kutumia dawa za miti shamba na wanyama.

Huyu ni Anyimike Malabeja (56)mkazi wa kitongoji cha Mtambo, Kijiji cha Bwenda, Kata ya Lubanda katika Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya, umbali wa kilometa 50 kutoka barabara kuu ya kutoka Mbeya kwenda Malawi, ambaye ndiye amemuokoa Pakyindi.

Mabeja ambaye ni mtoto wa sita katika familia ya Mzee Patisi Mabeja anasema kuwa alianza kutoa tiba hiyo baada ya kurithi kutoka kwa baba yake. Baba yake naye alirithi  kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa akitoa tiba hiyo wakati wa ukoloni kutokana na mazingira waliyokuwa wakiishi kutokuwa na hospitali na wataalam wa dawa za kisasa mara wanapokuwa wamepatwa na matatizo ya kuvunjika mifupa.

“Huu utaalam ni kutoka kwa mababu zetu, alianza kufanya babu yake baba akaja babu yangu, baadae akaja baba yangu ambaye ndiye aliyenirithisha… kwa sasa baba yangu ana umri wa zaidi ya miaka 90,” anasema.

Anasema baba yake alianza kutoa tiba hiyo mwaka 1982 ambapo watu wengi wa kutoka vijiji mbali mbali wamekuwa wakitibiwa na kupona, wakati huo yeye alikuwa anajifunza kwa karibu.

Dawa inayotumika

Mabeja anaeleza aina ya dawa inayotumika kuwa ni wanyama, mizizi inayoitwa ‘Mlumila’, na majani aina ya ‘Nalutete’ na ‘Nakisokoso kwa lugha ya Kindali.

Anasema kuwa shughuli za kuunganisha mifupa zinaendana na tiba ya kansa, hivyo wagonjwa pia hulazimika kutumia dawa ya kansa inayotokana na wanyama ambao ni Kapenka (Panya buku), Mbega weupe (jamii ya nyani) na mdudu anayependa kukaa kwenye matope (maarufu kwa Kindali kama Kabhwa kabhwa).

“Dawa hizi zinapatikana porini, kuna umbali mrefu ninalazimika kutembea kwa miguu kwa siku mbili hadi tatu kwenda na kurudi nyumbani kutokana na mazingira ya kijijini.

Jinsi anavyofanya kazi

“Nina utaalam wa kugundua tatizo hata bila kutumia picha kama wanavyofanya hospitalini, ninaweza kugundua ni aina gani ya mfupa uliovunjika na jinsi ya kupunguza mfupa na kuupanga vizuri,” anasema.

Anasema kuwa kuna mifupa ambayo inatoka nje na mingine ipo ndani kwa ndani ambapo huweza kutiba akitumia pia dawa ya ganzi ya hospitalini.

Anafafanua kuwa mara wagonjwa wamalizapo matibabu kwake  huwashauri kwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kujiridhisha kama wamepona. “Wengi wamefanya hivyo na wamepona kabisa,” anasema.

Anasema huwa anawapokea wagonjwa walioshindwa kupata tiba kwenye hospitali mbali mbali ikiwa ni pamoja na Rufaa Mbeya na wengine humchukua kwenda kutoa tiba majumbani kwa wagonjwa wenye hali mbaya zaidi.

Mganga huyo anasema enzi za mababu wagonjwa walikuwa wanatoa mbuzi mmoja kama gharama ya matibabu, lakini kwa sasa wanatoa Shs. 70,000 pekee ambayo ndiyo gharama ya mbuzi mmoja kwa wakati huu.

Hata hivyo, anasema anapata ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya Kijiji, Kata na Hospitali Teule ya Wilaya ya Ileje ya Isoko ambapo humsaidia kupata mipira ya kuvaa mkononi (glavu) wakati wa kutoa tiba na dawa ya ganzi.

Changamoto zinazomkabili ni pamoja ukosefu wa usafiri kwa ajili ya kwenda kutafuta dawa, ukosefu wa mawasiliano hapo kijijini kwake na hivyo kushindwa kuwasiliana na wagonjwa wake.

“Huku kwetu hakuna mawasiliano, hivyo nashindwa kabisa kuwasiliana na wagonjwa wangu kwani nimeweza kuwahudumia wagonjwa kutoka ndani ya mkoa na nje kama vile Morogoro na Iringa,” anasema mganga huyo anayetibu wagonjwa 20 kwa mwezi.

Kwa upande wake, Pakyindi ameiomba serikali kuwa karibu na mganga huyo ili kumuwezesha katika kutoa tiba.

“Serikali isiangalie waganga wale wanaojitangaza kwa mabango makubwa na kwenye vyombo vya habari, mganga wa ukweli hajitangazi bali anafuatwa, hivyo ni vema wakamtumia huyu kwa ajili ya kuokoa nguvu kazi kubwa ambayo imekuwa ikipotea kutokana na ajali na matukio mengine ya kijamii,” anasema.

Naye Abunuwasi Kalinga, mkazi wa Kijiji cha Bwenda, anasema mganga huyo amekuwa msaada mkubwa katika eneo hilo ambapo watu wengi wanaopata ajali katika shughuli mbali mbali wanatibiwa na kupona.

“Tumeshuhudia watu wengi ambao wamefika kwa mganga huyu na wamepona, kwa hapa kwetu kijijini vijana wengi wamehudumiwa na huyu mganga na wamepona bila hata ya kwenda hospitali,” anasema.

Abunuwasi anasema tatizo siyo serikali bali ni watoa huduma katika hospitali za umma ambao wanatanguliza maslahi binafsi badala ya kutoa huduma kwanza, hii husababisha watu maskini kupata ulemavu wa kudumu kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Ileje, Sylivia Siliwa, anasema wanamfahamu mganga huyo na wagonjwa wengi wamepona kupitia tiba yake, lakini bado hajajisajili na kutambulika kama waganga wengine wa tiba ya asili.

“Nimemsikia na halmshauri yetu inafahamu kuwepo kwake, lakini bado hajajisajili kwani anatakiwa kujisajili na kujiunga na umoja wa waganga wa tiba ya asili ili aweze kupata kibali na kutambulika kisheria,” anasema.

Anasema kinachotakiwa kwa sasa ni mganga huyo kuanza utaratibu wa kuhakikisha anajiunga na umoja huo ambao utamsaidia kutambulika kisheria na kupatiwa msaada wa aina yoyote ambao anauhitaji  kutoka halmashauri ili aendelee kutoa tiba yake vizuri na kwa watu wengi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *