Israel yaadhimisha miaka 70 ya kujitawala. Tanzania yaendelea kuitambua Palestina

Jamii Africa

Leo Mei 14, Taifa la Israel linaadhimisha miaka 70 ya uhuru wake. Lakini sherehe hizo huenda zikachochea zaidi uhasama wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo limekuwa na migogoro isiyoisha.

Miaka 70 iliyopita (14 Mei 1948), Waziri Mkuu wa kwanza wa Israel, David Ben-Gurion alisaini azimio la uhuru wa nchi hiyo katikati ya vita vya Waarabu na Wayahudi ambayo ilikuwa inapigania ardhi ya Jerusalemu na ukanda wa gaza.

Israeli ina mengi ya kusherekea katika siku hii ya kuzaliwa ikizingatiwa kuwa imejiimarisha kwa silaha za kisasa na jeshi lenye nguvu duniani. Katika miongo 7 iliyopita imejenga uchumi imara, viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa, imeshinda tuzo ya Nobel kwa kuwa na kituo bora cha sayansi.

Pia inasifika duniani kwa huduma bora za afya na matumizi ya lugha ya kiebrania. Inajivunia utamaduni wake na kufuata mfumo wa demokrasia ya bunge.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati, wanaeleza kuwa sherehe hizo zitazidisha uhasama kati yake na Palestina ambazo zimekuwa na ugomvi wa kihistoria kugombania ardhi ya Jerusalem.

Kuchochewa kwa ugomvi huo kunatokana na hatua ya Israel kuhamishia makao  makuu ya serikali katika jiji la Jerusalemu kutoka Ter Aviv, wakati bado haijamaliza uhasama na Palestina ambayo ina miliki sehemu ya Mashariki ya jiji hilo.

Vita hivyo vilianza muda mfupi baada ya Israel kutangaza uhuru 1948, ambapo Wapalestina 700,000 wengi wao wakiwa ni Waarabu waliondolewa katika ardhi ya wayahudi. Na siku iliyofuata Mei 15, 1948 walitangaza kama siku ya “Nakba” (“catastrophe” au Janga) ambayo wanaikumbuka kila mwaka wakidai waliondolewa kimabavu kwenye ardhi yao

Vita hiyo ilianzishwa na Ligi ya Waarabu (Arab League) ambapo majeshi yake yaliivamia Israel saa chache baada ya kutangaza uhuru. Katibu Mkuu wa Ligi, Azzam Pasha alitangaza kuwa Wayahudi watamalizwa ‘kwa mauji ya kimbali’ lakini nchi hiyo changa ilishinda vita hiyo.

Hata hivyo, Israel haina mipaka inayojulikana kimataifa. Ushindi wake wa kijeshi katika vita ya siku 6 dhidi vikosi vya Misri na Jordan mwaka 1967, vilisaidia kulitwaa eneo la Gaza, Kingo za Magharibi na Mashariki ya Jerusalem.

Moja la eneo la kitalii katika mji wa  Tel Aviv, Israel

Israel imeendelea kujenga makazi ya Wayahudi, licha ya shinikizo la kimataifa kuitaka usijitanue kwasababu ni kinyume na sheria za kimataifa. Nguvu hiyo imewapa mamlaka ya kuwatawala wapalestina ambao hawawezi kuchagua serikali yao wenyewe.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu amesema Israel imekuwa taifa kubwa ambalo litashinda ”giza” la maadui zake.

 

Kujitoa kwa Marekani katika Mkataba wa Nyuklia wa Iran

Jambo lingine linalochochea zaidi mgogoro wa Palestina na Israel ni mahusiano ya karibu ya rais wa Marekani, Donald Trump na Israel ambapo jumuiya za kimataifa zinalalamika kuwa  Trump anaonyesha dhahiri kuipendelea Israel ukilinganisha na mtangulizi wake Barack Obama ambaye alijaribu kusimama katikati kwenye mgogoro huo.

Tayari Trump ametangaza kujitoa kwa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia na Iran ambao uliasisiwa na Obama. Hatua hiyo inaiongezea nguvu Israel dhidi ya vikosi vya kijeshi vya Iran katika vita ya Syria ambayo viongozi wake wanashtumia kwa kutumia silaha za sumu za nyuklia.

Zaidi ni uamuzi wa Marekani kuzindua ubalozi wake katika jiji la Jerusalemu, siku ambayo Israel inaadhimisha miaka 70. Awali ubalozi huo ilikuwa katika jiji la Tel Aviv ikiwa ni ishara ya kuunga mkono Israel na jitihada zake za kujiimarisha katika ukanda wa gaza.

Lakini Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki  alitahadharisha kwamba hatua ya Trump “itaongeza uhasama katika kanda hiyo na hata maeneo mengine na kutoa changamoto zaidi katika juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo wa Israel na Wapalestina.”

Alisema Umoja wa Afrika unaendelea kuwaunga mkono Wapalestina na juhudi zao za “haki za kuwa na taifa huru ambalo litakuwa na Jerusalem Mashariki kama mji wake mkuu.”

Tayari maandamano makubwa yameaandaliwa katika wa ukanda wa Gaza yakiongozwa na Hamas kuonyesha hasira zao dhidi ya Trump kuhamishia ubalozi katika jiji la Jerusalem akijua bado eneo hilo liko kwenye mzozo.

Hamas wametishia kuwa siku ya leo na kesho jumanne wataandamana na kuvunja fensi za mpaka wa Gaza. Lakini jeshi la Israel limejipanga kukabiliana na waandamanaji ili kuepusha umwagaji wa damu. Hatua hiyo itatoa ujumbe kwa jumuiya za kimataifa kuwa bado mzozo huo haujatatuliwa.

 

 Nafasi ya Tanzania kwenye mgogoro huo

Tanzania ambayo kwa muda mrefu, tangu utawala wa Mwalimu Julius Nyerere imekuwa ikipinga Palestina kuporwa ardhi yake kama inavyodaiwa na  baadhi ya watu. Kutokana na msimamo huo mahusiano ya Israel na Tanzania yamekuwa ya kusuasua.

Tangu wakati huo Tanzania haikuwa na ubalozi nchini Israel, na Israel nayo haikufungua ubalozi nchini, lakini ilikuwa inatumia ubalozi wa Nairobi nchini Kenya.

Mei mwaka huu wakati Israel inaadhimisha miaka 70 ya kujitawala imetuma ujumbe muhimu kwa nchi za Afrika Mashariki. Ujumbe huo ni kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania katika mji wa Tel Aviv, ambao unafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kidiplomasia.

Ufunguzi wa ubalozi huo ni muendelezo wa juhudi za kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili ambazo zilitiwa nguvu na ziara ya mawaziri wawili wa Israel nchini Tanzania mwezi Machi.

Waziri wa Ulinzi Avigdor Liberman alizuru Tanzania tarehe 20 hadi 22 Machi 2018 naye mwenzake wa Sheria Ayelet Shaked akafanya ziara ya kukazi tarehe 23 na 24 Aprili 2018.

Taarifa zilizopo, zinaeleza kuwa Israel nayo inategemea kufungua Ubalozi wake nchini ili kuongeza uungwaji mkono katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya, Uganda na Rwanda kuwa na mahusiano ya karibu na nchi hiyo.

Uhusiano wa Tanzania na Israel unajikita zaidi kwenye teknolojia ya ulinzi, ambapo nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sayansi ya ujasusi kupitia shirika la Mossad ambalo linaaminika duniani kote kwa shughuli hizo.

Swali linabaki, Je Tanzania italegeza msimamo wake wa kuitambua Palestina kama mamlaka yenye haki ya kukalia ardhi ya ukanda wa Gaza na Jerusalemu Mashariki ambayo Israel inadai ni eneo lake ililoahidiwa na Mungu?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *