Misungwi ‘wampuuza’ Waziri Magufuli!

Jamii Africa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, imemtunishia ‘misuri’ Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli, baada ya uongozi huo kupuuza na kukataa kutekeleza agizo lililotolewa na Waziri huyo, juu ya Kivuko cha Serikali cha Mv. Kigongo.

Uongozi wa halmashauri hiyo umesema, kamwe hautatekeleza agizo la Waziri Magufuli alilolitoa kwa kuitaka halmashauri hiyo ikome mara moja kukusanya ushuru katika kivuko hicho cha Kigongo Ferri, kinachosafirisha abiria ndani ya Ziwa Victoria kutoka Misungwi kwenda Wilayani Sengerema mkoani hapa.

Waziri John Pombe Magufuli

Kauli hiyo ya kupuuza agizo la Waziri Magufuli, imetolewa hii leo na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, Benard Porcarp, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya hospitalini iliyofanyika katika hospitali ya wilaya hiyo.

Desemba 16 mwaka huu, Waziri Magufuli alipokuwa akizindua Kivuko cha Mv. Kome II Jimbo la Buchosa wilayani Sengerema, aliagiza halmashauri ya wilaya ya Misungwi kuacha mara moja kutoza ushuru kwenye kivuko cha Mv. Kigongo, kwa kile alichodai kwamba kivuko hicho ni cha Serikali kuu.

Waziri Magufuli ambaye alitoa agizo hilo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Mariam Seif Lugailla aliitaka halmashauri hiyo kukoma kukusanya ushuru kivukoni hapo, la sivyo Misungwi wajenge kivuko chao cha kukusanya ushuru huo, na si hicho kilichojengwa na Serikali kuu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa halmashauri ya Misungwi, Waziri Magufuli hana mamlaka yoyote ya kuzuia ukusanywaji wa ushuru katika kivuko hicho, na kwamba kamwe agizo hilo hawatalitekeleza, badala yake wataendelea kutoza ushuru huo kwa ajili ya mapato ya halmashauri.

“Waziri Magufuli hana mamlaka hayo ya kutuzuia sisi tusikusanye mapato hapo Kigongo Ferri. Tulimshangaa sana alipotoa agizo lake hilo kwetu.

“Yeye anasimamia sheria, halafu anakuwa wa kwanza kuvunja sheria. Sisi siyo mbumbumbu, ndiyo maana nasema Misungwi tutaendelea kukusanya ushuru Kigongo Ferri, bila kuogopa agizo la Magufuli”, alisema mwenyekiti Porcarp kwa kujiamini mbele ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Xavier Tilweselekwa.

Alisema, halmashauri hiyo inatumia sheria GN 198 ya mwaka 2002 katika kukusanya ushuru kivukoni hapo, ndiyo maana wana jeuri ya kukataa agizo la kiongozi yeyote.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *