Kutu ni moja ya tishio linalosababisha vifaa na mashine zenye asili ya chuma kushindwa kufanya kazi yake na hata kufa kabisa. Kama ilivyo kwa magonjwa ya kuambukiza, kutu husambaa kidogo kidogo na kuathiri kila atomiki inayopatikana kwenye chuma.
Madhara ya kutu kwa kiasi kikubwa hupunguza ufanisi wa kifaa husika na kumlazimisha mtumiaji kuingia gharama kubwa za matenegenezo. Lakini kinachosikitisha zaidi ni kuwa matokeo hayo sio kosa lako!
Kabla ya kwenda kwenye njia za kusafisha kutu, ni vizuri kuelewa kwanini vyuma vinapata kutu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kukirejesha chuma katika hali yake ya awali ili kiendelee kutumika.
Kwanini vyuma vinapata kutu?
Kutu ni matokeo ya kemikali haribifu kushambulia vyuma na mchakato huo hujulikana kama ulikaji wa chuma (corrosion). Ulikaji hutokea wakati chuma kinapotofautiana na mazingira kilipo; hasa hali ya hewa ya eneo husika ambapo hewa ya Oksijeni yenye asili ya majimaji hufunika chuma na kuunda tabaka jipya.
Hata hivyo, vyuma huathirika zaidi na hali hiyo kwasababu ndio hutumika zaidi kwenye shughuli za viwandani na nyumbani. Ulikaji ‘Corrosion’ unaotokea kwenye vyuma ndio hujulikana kama kutu.
Kutu ni matokeo ya mchanganyiko wa chuma, hewa ya Oksijeni na maji (mvuke/ukungu) ambao huunda tabaka lenye rangi nyekundu kahawia juu ya chuma ambayo ina kemikali za ‘hydrated iron oxide’ na ‘iron oxide-hydroxide’.
Baadhi ya tahadhari zinazoweza kuchukuliwa ili kukilinda kifaa chenye asili ya nyuma kukutana na hewa; ni kuhifadhi kwenye mifuko yenye mafuta ya silika, kupaka rangi au madini chuma/bati. Hii huzuia chuma kukutana na mazingira yanayokizunguka.
Lakini njia hizo sio za kudumu, kwasababu huruhusu hewa kukishambulia chuma kupitia mipasuko midogo. Katika mazingira kama haya, unahitaji njia rahisi kuondoa kutu na kukiacha chuma kufanya kazi yake. Jambo la muhimu ni kuwa njia hizi ambazo tunazijadili hapa chini zimehakikiwa kisayansi:
Magadi Soda
Njia hii inaweza kutumika nyumbani. Chukua unga wa magadi changanya na maji mpaka upate uji mzito. Jambo la kuzingatia ni kwamba mchanganyiko huo usiwe mlaini au mgumu sana. Paka au weka mchanganyiko wa magadi juu ya chuma chenye kutu halafu kiache kwa saa chache. Baada ya hapo ondoa kutu kwa brashi.
Changamoto ni kwamba tabaka gumu la kutu juu ya chuma haliwezi kuondolewa kirahisi kwa brashi na kama utalazimisha unaweza kuharibu chuma. Inashauriwa utumie msasa kuondoa kutu hiyo.
Siki na asidi ya matunda
Njia nyingine unayoweza kutumia nyumbani ni asidi hafifu, kama siki (vinegar) au asidi ya limau, ndimu na machungwa. Chukua Kifaa chenye kutu na weka kwenye chupa iliyo na siki kisha funika vizuri ili kutoruhusu hewa kuingia. Hakikisha chupa imetikiswa vizuri na iache angalau siku moja ili kuruhusu asidi kufanya kazi yake.
Asidi inafanya kazi ya kuyeyusha tabaka la kutu na kukirejesha chuma kwenye hali yake ya awali. Inashauriwa kutumia asidi hafifu kwasababu ukitumia asidi kali sio tu itayeyusha tabaka la kutu lakini itaondoa tabaka laini la chuma. Njia hii inaweza kutumika kusafisha misumali na skrubu (screws).
Kwa upande wa asidi ya matunda, paka chumvi kwenye chuma na kisha pitisha maji ya limao. Subiri kwa saa kadhaa kisha sugua chuma kuondoa kutu. ikiwa kutu itaendelea kuwepo kwenye chuma, rudia tena mchakato na kiache chuma kikiwa na mchakanyiko huo wa chumvi na asidi kwa saa 24. Baada ya hapo kwangua ili kuondoa kutu. Msisitizo ni kwamba unatakiwa kuwa makini ili usiharibu muonekano wa kifaa chako.
Kemikali ya WD-40 iliyoidhinishwa kuondoa kutu
Vifaa ambavyo viko wazi ndivyo mara nyingi vinapata kutu. Inashauriwa vifaa vyenye asili ya chuma kuhifadhiwa kwenye droo vikiwa vimefungwa kwenye mfuko maalumu wenye mafuta ya silka kama hatua ya kuchukua tahadhari. Hata hivyo kutu inaweza kupenya.
Kuliko kutumia asidi, unaweza kupulizia virainishi aina ya WD-40 na kusugua kwa msasa mlaini aina ya ‘Scotch-Brite pad’.
Kwa njia nyingine za kudhibiti kutu, tumia asidi yenye nguvu iliyoidhinishwa na mamlaka husika. Nyingine ni Evapo-Rust ambayo hurejesha muonekano wa chuma katika hali ya awali.
Kimbilio la mwisho? ‘Electrolysis’
‘Lysis’ ni neno la Kigiriki lenye maana ya kutenganisha na ‘electrlysis’ ni kutenganisha kwa kutumia umeme. Njia hii hutumika kuvunja tabaka la kutu na kuliondoa kwenye chuma kwa kutumia umeme wa betri.
Unahitaji ndoo kubwa iliyo na mchanganyiko wa maji na magadi soda ambao ni njia salama ya umeme kupita kwenye chuma. Chuma chenye kutu na kile ambacho hakina kitu vyote hutumbukizwa kwenye mchanganyiko huo.
Waya chanya wa betri (hasa wa gari) huunganishwa kwenye chuma kisicho na kutu na ule wa hasi huunganishwa kwenye chuma nyenye kutu ambacho kinatakiwa kushafishwa.
Washa betri ili kuruhusu waya hasi kwenda kwenye chuma chenye kutu ili kuondoa tabaka lisilotakiwa. Kiache chuma hicho ndani ya mchanganyiko huo kwa siku moja ili kuruhusu mchakato wa kuondoa kutu kufanyika. Baada ya hapo ondoa chuma kwenye maji hayo ya magadi.