Jitihada zaidi zinahitajika kukomesha vifo vinavyotokana na uzazi Tanzania

Jamii Africa

MIAKA 27 iliyopita Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 18 barani Afrika katika orodha ya nchi 20 zilizokuwa zikiongoza kwa idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi.

Lakini hivi sasa FikraPevu inaandika bila shaka kwamba, Tanzania imejitahidi kupunguza idadi hiyo kwa takriban theluthi mbili kutoka vifo 997 mwaka 1990 hadi 398 mwaka 2015 kati ya vizazi hai 100,000, japokuwa inaendelea kushika nafasi ya tatu kwa Afrika Mashariki.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba, Kenya, ambayo pamoja na Uganda zilikuwa ikiongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya vifo (vifo 687 kati ya vizazi hai 100,000), hivi sasa inashika nafasi ya nne kwenye kanda hiyo ambapo sasa inarekodi vifo 510 kati ya vizazi hai 100,000.

Ingawa mafanikio hayo hayawezi kulinganishwa na Rwanda, inayoongoza kwa idadi ndogo ya vifo 290 kutoka vifo 1,300 mwaka 1990, lakini walau yanatia moyo kwamba kuna jitihada kubwa zilizofanyika kuhakikisha usalama wa afya ya akinamama wajawazito na watoto wanaozaliwa.

FikraPevu inaona kwamba, licha ya rekodi za Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonyesha matumaini hayo, lakini bado kuna kazi ngumu ya kutokomeza vifo hivyo walau kufikia kwenye tarakimu mbili kama siyo tarakimu moja kama ilivyo kwa Libya.

Libya ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo kwa kiasi kikubwa imeweza kufikia kwenye tarakimu moja ya vifo kwa kurekodi vifo 9 tu kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 39 mwaka 1990.

Kufikia walau tarakimu mbili kama ilivyo kwa Misri, Cape Verde, Mauritius na Tunisia ni kazi ngumu, lakini inawezekana ikiwa Serikali itatenga bajeti ya kutosha katika sekta ya afya na kuboresha huduma kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa.

FikraPevu inatambua kwamba Rwanda imefanikiwa kupunguza vifo hivyo kwa sababu kuu mbili, kwanza kwa kuboresha huduma za afya lakini pili imepata unafuu kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na Tanzania, ambayo mwaka 1990 ilikuwa na watu milioni 23.1 na sasa ina watu milioni 50.

Kwa Tanzania ambayo inaendelea ‘kuogelea katika kilindi cha amani’ kuliko nchi nyingi za Afrika, suala la kudumisha huduma za afya ni la msingi kinyume chake inaweza kujikuta kama Afrika Kusini ambayo badala ya kupunguza vifo vya uzazi, imejikuta idadi ikipanda.

FikraPevu inafahamu kwamba, mwaka 1990 Afrika Kusini ilikuwa na idadi ya vifo 108 kwa kila vizazi hai 100,000, lakini kufikia mwaka 2015 nchi hiyo ilirekodi vifo 138.

Uchunguzi wa FikraPevu umeonesha kwamba, mataifa kama Sierra Leone, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Sudan Kusini, Somalia, Nigeria, Liberia, Burundi, Gambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Guinea na Ivory Coast bado yanaidadi kubwa ya vifo kutokana na kukumbwa na migogoro ya kisiasa ambayo imesababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Jitihada za wadau

Daktari akimpima mama mjamzito.

Pamoja na kwamba serikali inajitahidi kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya ya uzazi, bado juhudi hizo hazijawakomboa wanawake wengi hasa wa vijijini, ndiyo maana wadau wengine nao wamekuwa wakishiriki kuhamasisha jamii na serikali katika kuhakikisha idadi ya vifo inapungua.

FikraPevu inajua kwamba, tarehe 15 Machi ya kila mwaka, Muungano wa Utepe Mweupe (White Ribbon) hufanya maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe Duniani katika kuunga mkono juhudi za mataifa mbalimbali duniani kupunguza vifo hivyo wa wanawake.

Maadhimisho hayo huambatana na shughuli mbalimbali za kijamii, kama vile kutoa ushauri wa afya ya uzazi na upimaji wa magonjwa mbalimbali.

Mwaka huu maadhimisho hayo yalifanyika Machi 10 ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, ambapo yalitanguliwa na shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Machi 5 hadi 9, huku yakiwa na kauli mbiu ya ‘Vifo vitokanavyo na uzazi havikubaliki, Wajibika’.

Utepe mweupe wasimamia

FikraPevu inatambua kwamba, Utepe Mweupe duniani ni alama ya uwakilishi ya kuwakumbuka akina mama waliofariki kutokana na matatizo ya mimba, uchungu na uzazi.

Mratibu wa taifa asasi ya Utepe Mweupe, Rose Mlay, aliiambia FikraPevu kwamba, lengo la asasi hiyo ni kushawishi kuimarika kwa huduma za afya kwa mama na mtoto.

“Asasi hii ambayo ilianzishwa mwaka 2004 pia inahakikisha kuwa tatizo la vifo vya uzazi linapunguzwa na hatimaye kumalizwa kabisa, hasa kutokana na sababu ambazo zinaepukika,” alisema Mlay.

Aliiambia FikraPevu kuwa lengo la asasi hii pia kuifanya Tanzania kuwa taifa ambalo haki ya mama na mtoto kuwa salama wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua linazingatiwa.

Jitihada zaidi

Mama Mlay alisema kwamba, jitihada zaidi zinahitajika kutokomeza vifo vya mama na mtoto ambavyo vinaepukika.

“Vifo hivyo vina madhara makubwa kijamii na kiuchumi kwani wanaokufa ni nguvu kazi ya taifa, na vifo hivyo huacha watoto yatima ambao wanaleta changamoto kubwa kwa jamii katika malezi” Mama Mlay aliiambia FikraPevu.

Sababu za vifo hivyo ni pamoja na uduni wa huduma za afya, utaratibu wa kujifungulia nyumbani, gharama zinazoambatana na huduma hizo, kifafa cha mimba na mapigo ya moyo kuwa juu.

NHIF wapigiwa chapuo

Katika maadhimisho ya mwaka 2016, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwasihi wanawake kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuondokana na ukosefu wa fedha wakati wa kujifungua kwani huduma hiyo hutolewa kwa utaratibu maalum unaowawezesha kutibiwa bila kulipa fedha taslimu.

Aidha, aliwataka wananchi kuachana na mila potofu hasa ukeketaji ambao unasababisha tatizo la kutoka damu nyingi na hatimaye kusababisha vifo wakati wa kujifungua.

Hata hivyo, uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, vikwazo vingine vya kufikiwa uzazi salama nchini ni pamoja na vituo vingi vya afya kukosa huduma za awali na za dharura, kama upasuaji na damu salama, umeme wa uhakika, hasa vijijini na upungufu wa watumishi wa afya wenye ujuzi na stadi, upungufu wa vifaa tiba na dawa muhimu.

Changamoto zaidi zabainika

Aidha, changamoto nyingine ni pamoja na kuwanyima watoto wa kike elimu, kuwaozesha watoto katika umri mdogo, kuwanyima wanawake fursa ya kumiliki uchumi, hivyo kuwafanya kushindwa kufikia huduma bora za afya hususani wakati wa kujifungua na kuishia kuhudumiwa na wakunga wa jadi ambao hawawezi kuhimili matatizo makubwa ya uzazi pindi yanapojitokeza.

Ofisa Mawasiliano wa asasi hiyo, Anna Sawaki, alisema asasi hiyo inafanya kazi kwa karibu na kundi la wabunge 22 wakiongozwa na Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, kwa kushawishi watunga sera waongeze Bajeti ya Wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na kutoa ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

“Katika kuhakikisha tunafanikisha suala hilo, Muungano wa Utepe mweupe umekuwa ukitafuta ushawishi ngazi ya halmashauri mpaka serikali kuu kwa nafasi zao kuhakikisha bajeti ya huduma za uzazi za dharura zinapewa kipaumbele katika ngazi za halmashauri na bajeti ya afya kwa ujumla” aliiambia FikraPevu.

Mikakati inayofanywa na Muungano wa Utepe Mweupe ni pamoja na kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kuhakikisha kampeni hii inawafikia walengwa.

Mashirika zaidi yasaidia

Baadhi ya Mashirika, taasisi na asasi zinazoshirikiana na Muungano wa Utepe mweupe ni pamoja na AfriCare, TAMA, UMATI, Plan International, Thamini Uhai, Benjamin Mkapa Foundation na Save the Children.

Asasi hii inashirikiana na nchi wanachama kutoka Uingereza, India, Malawi, Nepal, Nigeria, Sweden, Uganda, Yemen, Zimbabwe, India na Afghanistan.

Taarifa ambazo FikraPevu imezipata zinasema kwamba, asasi ya AfriCare ambayo itajenga chumba cha upasuaji mkoani Rukwa na asasi ya Benjamin Mkapa inaendelea kutoa mafunzo ya huduma za afya huku asasi nyingine zikisaidia kuimarisha miundombinu kama umeme na maji.

Aidha, Muungano wa Utepe Mweupe pia wamefanya kampeni mbalimbali za kuongeza watumishi wa afya katika vituo vya kutoa huduma, kuboresha huduma katika mikoa ya pembezoni na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Faida zaidi zaonekana

FikraPevu inafahamu kwamba, kampeni hiyo imefanikiwa katika Mkoa wa Rukwa, ambapo idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kwa asilimia 65 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 30 mwaka 2010.

Baadhi ya wananchi wameipongeza asasi hiyo na kushauri elimu ya uzazi itolewe kwa msukumo zaidi hasa kwa wanawake wa vijijini.

Vilevile wameshauri Wizara ya Afya kufuatilia kwa karibu hospitali za binafsi ambazo nyingine huajiri watumishi wasio na utaalamu wa kutosha jambo ambalo ni kikwazo kwa wajawazito kipindi cha kujifungua.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *