WILAYA ya Mpwapwa ni moja ya Wilaya saba zinazounda mkoa wa Dodoma. Inapakana na Wilaya za Chamwino, Kongwa, Kilolo mkoani Iringa na Kilosa Mkoani Morogoro.
Ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 7,379 imegawanyika katika tarafa nne, kata 30, vijiji 84 na vitongoji 490.
Miongoni mwa vivutio vilivyo katika Wilaya ya Mpwapwa ni josho la kwanza kujengwa Afrika Mashariki na Wajerumani mwaka 1905 ambalo limeendelea kutumika hata sasa.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri) Dk.Daniel Komwihangilo anasema taasisi hiyo ilianzishwa na Wajerumani mwaka 1905 wakati huo ikiwa kama kliniki ya kutibu magonjwa ya mifugo.
“Wajerumani hawakuacha kumbukumbu nyingi isipokuwa majengo kadhaa na josho la kwanza hapa Afrika Mashariki na kati ambalo lilijengwa mwaka 1905 na hadi sasa bado linatumika.” Anasema
Pia tangu wakati huo Taasisi hiyo imekuwa kitovu cha utafiti wa mifugo kitaifa na kimataifa ambapo mwaka 2005 taasisi hiyo iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.
Anasema kujengwa kwa josho hilo kunatokana na Wajerumani wakati wa utawala wao katika Wilaya ya Mpwapwa walikuwa wakiona kama Wilaya hiyo kama eneo la kuwekeza kijamii na kiuchumi.
Lakini katika kuhakikisha wanapata nyama nzuri na salama walianzisha kituo cha utafiti wa mifugo na kujenga josho.
Lakini unapoliona josho hilo utagundua lilijengwa kwa ujuzi wa hali ya juu ambapo hufanya ng’ombe asitumie nguvu wakati anaingia ili awe anateleza.
Kwa jinsi josho hilo lilivyojengwa baada ya ng’ombe kupita kwenye maji yenye dawa kuna sehemu ya kumkaushia ng’ombe.
Hata unapoangalia majosho mengine yaliyojengwa miaka ya 1980 lakini ubora wake kwa sasa ukiuangalia haulingani na josho hilo lililojengwa na Wajerumani.
Kwa mujibu wa Dk. Komwihangilo anasema tangu wakati huo Taasisi hiyo imekuwa kitovu cha utafiti wa mifugo Kitaifa na kimataifa ambapo mwaka 2005 taasisi hiyo iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.
Kwa mujibu wa watafiti wa taasisi hiyo kudumu kwa muda mrefu kwa josho hilo kumechangiwa na ujenzi imara kwani licha ya kujengwa miaka mingi lakini josho hilo bado lina ubora wa hali ya juu kulinganishwa na majosho mengine yaliyojengwa miaka ya hivi karibuni.
Hiyo inatokana na ukweli kuwa teknolojia waliyoitumia ilikuwa nzuri licha ya kujengwa kwa matofali ya kuchoma lakini uimara wake uko pale pale ikiwa ni zaidi ya miaka 109 tangu kujengwa kwake.
Unapoongea na wenyeji wa maeneo hayo wanasema ujenzi waliokuwa wakifanya Wajerumani haulingani na ujenzi unaoendelea sasa kwani awali walitumia utaalam zaidi kulingana na hali ya mazingira ya maeneo husika.
Frank Anania mkazi wa Mpwapwa anasema kuwa majosho mengi yanayojengwa sasa hayana ubora kutokana na kujengwa chini ya viwango hali inayosababisha kuharibika baada ya muda mfupi.
Anasema hali hiyo inachangiwa na urasimu na ubabaishaji kwenye miradi mingi ya ujenzi kunakosababishwa na watu wasio na sifa kupewa kazi ya ujenzi au kazi za kusimamia miradi.
Kwa upande mwingine, mkazi wa Mpwapwa, Barnabas Kisengi anasema Mpwapwa ni Mji wa siku nyingi lakini maendeleo hayaendi kwa kasi kwani hata barabara ya kuingilia ndiyo hiyo hiyo ya kutokea.
Anasema jambo la muhimu ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na ujenzi wa barabara katika Mji wa Mpwapwa na vitongoji vyake ili kurahisisha mawasiliano.
Anasema hata ukiangalia uchumi wa wilaya hiyo haukui kwa kasi kubwa kutokana na ukosefu wa babaraba wa uhakika ambapo wakati wa msimu wa mvua hali inakuwa mbaya zaidi kutokana na barabara nyingi kutopitika kwa urahisi.
Kisengi anasema wilaya hiyo bado ina tatizo la kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo vimesahaulika yakiwemo makaburi ya Wajerumani yaliyopo eneo la Kikombo Mpweapwa Mjini ambayo kwa miaka ya hivyi karibuni yalizungushia uzio.
“Makaburi hayo yalisahaulika miaka mingi sana na hata kukawa na hofu ya kupotea kwa kumbukumbu hiyo” anasema
Pia Kisengi anasema ni muhimu kama mali kale zikapewa umuhimu wa kipekee ili kuongeza kipato cha halmashauri kwani vituo hivyo vikiboreshwa vitakuwa chanzo kikubwa cha utalii.
Anataka kisima ambacho kilitumiwa na watumwa kunywa maji na hata mti uliotumika kunyongea watumwa vinaweza kuwa vivutio tosha kwa wageni na watafiti kufika katika Wilaya hiyo.
“Pia kuna njia ambayo watumwa walikuwa wakipita eneo la Vighawe ambapo njia hizo zinaweza kupotea kama hakutakuwa na jitihada za kuhifadhi” anasema