Joto lazidi kupanda CHADEMA, CCM Uchaguzi Kirumba

Jamii Africa

JOTO la uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata ya Kirumba Jijini Mwanza, limezidi kupanda kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo mwanasiasa kijana wa CCM, Jackson Kabala Masamaki (38), anatajwa kung’ara zaidi ndani ya chama hicho.

Imeelezwa kwamba, Masamaki ambaye ni miongoni mwa wana CCM 11 waliochukuwa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea udiwani wa Kata hiyo, anatajwa kuwa ndiye pekee anayeweza kupambana na kutoa upinzani mkali dhidi ya mgombea yeyote wa Chadema.

Baadhi ya wanachama wa CCM katika kata hiyo ya Kirumba wameeleza leo kwamba, kimsingi CCM inatakiwa kumteua mtu mzuri na mwenye ushawishi mkubwa kwa wananchi, vinginevyo chama hicho kitapata pigo jingine kwa kushindwa kwenye uchaguzi na Chadema.

Wanachama hao wa CCM walimtaja moja kwa moja mwanasiasa huyo maarufu, anayefahamika kwa jina la ‘Jack Masamaki’ kuwa ndiye pekee anayeweza kuikomboa kata hiyo , iwapo chama kitampitisha kuwa mgombea katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi mwaka huu.

“Bila Masamaki kumsimamisha kuchuana na Chadema hapa Kirumba, CCM tutapata pigo jingine.  Chadema bado wanakubalika sana kwa wananchi, hivyo CCM isilogwe ikapeleka mtu wanaomtaka wao.

“Bila kupamba, Masamaki anakubalika kwa watu wa rika lote…na ana uwezo wa kuwasaidia wananchi, hivyo hii ni turufu pekee ambacho CCM inatakiwa ijivunie nayo. Wananchi wanahitaji mtu mwenye mtazamo wa kuwaletea maendeleo, hawahitaji machaguo ya vigogo wala longolongo.

“Kirumba inahitaji kuwa na mtu anayekubalika kwa wote. Ushawishi mkubwa alio nao kijana Masamaki ndiyo kiboko cha upinzani, la sivyo tutashuhudia ‘Peoples’ wakiitwaa tena kata yetu hii”, alisema mwanachama mmoja wa CCM ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba, unatokana na kufariki kwa aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Novatus Manoko (Chadema), ambaye alifariki mwaka jana.

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, takriban wanachama wake watatu wanaotajwa kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa umma tayari walishachukuwa na kurudisha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ya udiwani Kirumba.

Katibu wa Chadema mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi alimemwambia mwandishi wa habari hizi leo jijini hapa kwamba: “Moto wa Chadema upo pale pale. Wananchi wa Kirumba wasiwe na shaka, tunawapelekea mchakapakazi mwingine kama alivyokuwa marehemu Novatus Manoko”.

Alisema, kwa taarifa alizonazo wanachama wake watatu wenye ushawishi mkubwa wa kimaendeleo walishachukuwa na kurudisha fomu, na kwamba taratibu zote za kichama zitatumika kumsimamisha mgombea ambaye ni chaguo la wananchi wote wa kata hiyo.

“Sisi Chadema hatuna hofu na uchaguzi huu wa Kirumba. Tunaamini tutairudisha tena kata hii, maana mgombea atakayesimamishwa na chama changu ni yule anayestahili kwa watu wote”, alitamba Katibu huyo wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Mushumbusi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili katani humo, walisema wanachokisubiri ni kuona chama gani kimemsimamisha mgombea anayestahili kwao, na mwenye malengo na mtazamo mpana zaidi wa kuwaletea maendeleo makubwa ya kisekta.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *