Kadi alama ya lishe  kutokomeza utapiamlo, udumavu kwa watoto chini ya miaka 5

Jamii Africa

Serikali imeanza kutumia kadi alama ya lishe ili kuongeza uwajibikaji kwa watoa huduma itakayosaidia kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto nchini.

Muhtasari wa hali ya utapiamlo Tanzania ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa asilimia 34 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini wamedumaa. Kwa maeneo maeneo ya mjini ni asilimia 25 na vijijini ni asilimai 38.

Kutokana na viwango vikubwa vya utapiamlo na udumavu vinavyosababisha na lishe duni, vimeathiri ukuaji na uwezo wa watoto kijifunza shuleni, jambo ambalo lina matokeo hasi kwa nguvu kazi ya taifa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema  matumzi ya kadi alama ya lishe utasaidia kufuatilia ufanisi na uwajibikaji wa watoa huduma za lishe nchini ili kuhakikisha viashiria vyote vya utapimlo vinadhibitiwa  mapema na kuwawezesha watoto na watu wazima kuepukana na udumavu wa akili na mwili.

“Katika kufuatilia kiwango cha ufanisi katika utekelezaji wa afua za lishe nchini na kuhimiza uwajibikaji kwa watoa huduma, Wizara imeanza kutumia Kadi Alama ya Lishe (Nutrition Score Card). “ amesema Waziri Ummy.

Amesema Kadi hiyo itakuwa na viasharia 18 ambavyo vitatumika kupima utekelezaji wa lishe katika maeneo mbalimbali nchini. Viashiria hivyo vitatumika kama vigezo vya msingi ambavyo vinaonyesha mtoto aliyekidhi vigezo muhimu vya lishe ikiwemo kupata matone ya vitamin, madini, chakula bora na chanjo.

“Kadi Alama hii ina jumla ya viashiria 18 ambavyo vinatumika kufuatilia utekelezaji wa afua za lishe na matumizi ya kadi hii yamezingatia uzoefu uliopatikana katika matumizi ya kadi alama nyingine zilizopo nchini kama ile ya Malaria na ile ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto. “, amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema  ili kampeni hiyo ifanikiwe, serikali inatakiwa kuongeza bajeti kwa taasisi  ya Chakula na Lishe (TFNC) kuwezesha kutimiza majukumu yake ikizingatiwa kuwa taasisi hiyo inafanya kazi na sekta zaidi ya moja.

Amesema viwango vya udumavu vinavyotokana na lishe duni kwa watoto nchini siyo vya kuridhisha na serikali ifanye juhudi za makusudi kutatua changamoto hiyo kwa watoto.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mapitio ya bajeti ya Lishe iliyotolewa na Shirika la Watoto duniani (UNICEF-2015/2016) nchini Tanzania inaeleza kuwa bajeti iliyotengwa kwenye shughuli za lishe ya taifa imeongezeka hali iliyochochea ongezeko la matumizi mara mbili zaidi ukilinganisha na mwaka wa fedha wa 2011/2012 na 2014/2015.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa matumizi halisi katika sekta hiyo kwa mwaka 2011/2012 yalikuwa bilioni 10.5 na bajeti hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na hadi kufikia 2014/2015 ilikuwa bilioni 22.5. Licha ya ongezeko hilo bado bajeti hiyo haikidhi mahitaji yote ya lishe inayoelekezwa katika sekta mbalimbali ambazo zinahusika kuboresha afya za watoto.

Matumizi ya bajeti ya lishe yanaelekezwa katika maeneo matatu makuu ambayo ni kuhimiza ulaji wa chakula bora kwa watoto wachanga na watoto wadogo; kuzuia na kupambana na utapiamlo na kuboresha mazingira kuiwezesha serikali kutoa huduma bora za lishe nchini.

Shughuli zote hizo zinaratibiwa na sekta za afya na ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, jinsia na watoto; elimu; kilimo, usalama wa chakula; maji na usafi; mifugo na uvuvi; biashara na viwanda na taasisi za fedha.

 

Utapimlo na Udumavu

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa utapiamlo ni upungufu, ziada au kutokuwa na usawa katika kiwango cha chakula kinachompa mtu nguvu au virutubisho mwilini. Hali hii hutokea kwenye makundi mawili; kwanza kutokuwa na lishe ya kutosha ambako kunajumuisha kudumaa, kuwa  na uzito mdogo pamoja na kukosa virutubisho vya kutosha.

Pili ni kula vyakula vinavyoleta  unene uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha. Na hali hii huwapata zaidi watoto na watu wenye kipato kizuri waishio mjini.

Sababu kubwa ya watoto kupata utapiamlo ambao unasababisha udumavu wa akili na mwili ni kwamba familia nyingi hula vyakula vya wanga kwa wingi mfano ugali wa mahindi, unga wa mtama, muhogo, mchele na vyakula vya jamii ya maharage. Milo mingi hukosa mchanganyiko wa protini ya wanyama, mimea, mbogamboga na matunda.

Ripoti ya ya Shirika la Watoto Duniani  (UNICEF) inayoangalia  viwango vya ukosefu wa lishe kati ya mwaka 1992-2015 inaonyesha kuwa udumavu na utapiamlo sugu umepungua kutoka asilimia 50 hadi 34, huku utapiamlo uliokithiri ukipungua kutoka asilimia 7 hadi 5 na hali ya upungufu wa uzito ikipungua kutoka asilimia 24 hadi 14.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anaendelea kuwa kuwa, “Katika kupambana na utapiamlo nchini, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wa Lishe imetoa matone ya nyongeza ya vitamin A kwa watoto wa kati ya miezi sita na miaka mitano sambamba na dawa za minyoo kwa watoto wa umri kati ya mwaka mmoja na miaka mitano.”

Amebainisha kuwa wizara yake itaendelea  kutoa huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto kupitia; kuongeza idadi ya Hospitali zinazotoa matibabu ya utapiamlo na kuboresha miundombinu ya hospitali kwenye wodi  17 za kulaza watoto.

“Wizara yangu pia imeendelea kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa chakula dawa na vifaa vya kupimia hali ya Lishe pamoja na kujengea uwezo wa watoa huduma.” Amesema Waziri Ummy.

Naye, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali itakua na miradi mingi ya kutekeleza, miongoni mwa miradi hiyo ni kupambana na tatizo la utapiamlo hivyo ni vema kama nchi ikaangalia namna bora ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia katika utekelezaji wake.

“Kitaalamu mpaka mwanadamu anapofikisha siku 1000 ni kipindi muhimu sana kinachoamua maisha ya mwanadamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa na uwezo gani wa kufikiri, kutokana na hali hiyo mtu ambaye atakua na utapiamlo uwezo wake utakua ni mdogo zaidi kulinganisha na mtoto aliyepata lishe bora’” alifafanua Dkt. Mpango.

Katika kutekeleza mradi huo Serikali itafanya kazi na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe ili kuhakikisha kwamba Taifa linapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la utapiamlo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *