MISSENYI ni kati ya wilaya nane za mkoa wa Kagera yenye ranchi mbili za taifa na sehemu imebinafsishwa kwa wawekezaji. Ni wilaya mpya iliyoanzishwa Julai 2007 ambayo asilimia 59 ya eneo lake inafaa kwa kilimo.
Katika ranchi za Missenyi na Mabale, imeibuka migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji na wananchi.Wanakabiliwa na vitisho ikiwemo kuharibu makazi yao kama shinikizo la kuwahamisha.
Wamezuiwa kuendelea na kilimo, na mashamba yao ni malisho ya mifugo ya wawekezaji.Wananchi wanadai mipaka ya vijiji haiheshimiwi na hata hawakuhusishwa wakati wa kugawa ardhi. Badala yake wananchi hawa walistahili kuwa na furaha kwani maeneo wanayoishi yalitumika kama uwanja wa mapambano wakati wa vita vya kumng’oa Nduli Idd Amin.
Serikali iliwahamisha kwa muda na baada ya vita walirudi. Wanamkumbuka Marehemu Edward Sokoine kuwa alitoa amri ya wao kurudi kutoka uhamishoni kwani ushindi ulikuwa umepatikana na mapambano yalikuwa yamekwisha.
Mkazi wa kijiji jilani cha Byeju Petro Muzora ni miongoni mwa wananchi waliotekwa na majeshi ya adui ambaye anasema alishuhudia wenzake sita wakiuwawa na yeye kufanikiwa kutoroka.
Kitendawili cha uchomaji wa nyumba 36
Mwandishi wa FikraPevu alipokelewa kama rafiki wa mashaka zikiwa ni wiki chache tangu kuchomwa moto nyumba 36 na wanaodaiwa ni viongozi wa serikali. Bado wanaomboleza tukio hilo la kikatili na hawana imani na mgeni yeyote.
Katika kitongoji cha Kazizi ni wanawake na watoto wanaojitokeza kutoa maelezo ya tukio hilo. Wanaume wamezikimbia familia kwa hofu ya kukamatwa na kufunguliwa kesi za kutungwa. Wanadai waume zao wamepotea, wameachiwa watoto na wanatakiwa kumpisha mwekezaji.
Beatha Anthony (44) ni mwanamke mjane aliyeachiwa watoto sita na anadai yeye na watoto wake walishuhudia uchomaji wa nyumba yao. Alisema Juni 17 alifika mkuu wa Wilaya akiwa na kikosi cha askari na kumwamuru atoe vitu vyake ndani.
Alimtambua kuwa ni mkuu wa wilaya kwani amefika mara nyingi na siku hiyo alifika na gari likiwa na bendera akiwa na askari. Baada ya kutoa vitu vyake nje nyumba ilichomwa moto na zoezi hilo kuendelea kwa nyumba nyingine.
Maelezo ni yale yake kutoka kwa Speransia Phaustin(40) aliyesema anamfahamu na kumjua kiongozi wake. Zoezi liliendeshwa mbele ya macho yake na kuwa vilio vyao pamoja na watoto havikuzuia kufanyika kwa zoezi hilo.
Mwamad Zaid anasema baada ya kuchoma nyumba ya Silvester Nyabenda walihamia kwake na kuwa ulitokea ubishi kati yake na Mkuu wa wilaya aliyemshurutisha kuondoa mali zake ndani ya nyumba. Uchomaji ulifanyika na kuwa mbali na kumfahamu pia alikuwepo mtendaji wa kijiji John Mbuga.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kazizi Cleophace Lubega anasema ukatili huu hauvumiliki na hivi karibuni amekamatwa na kuwekwa ndani katika kituo cha polisi Kyaka kwa amri ya mkuu wa wilaya kwa madai ya kukwamisha zoezi la kuwahamisha wavamizi.
Anasema wananchi wamekosa mtetezi na wale waliotakiwa kuwatetea wanamkumbatia mwekezaji. Shughuli za uzalishaji zimesimama ambapo hata wanafunzi wa familia zilizopoteza makazi hawaendi tena shuleni. Ujenzi wa shule ya msingi umesimama kutokana na mgogoro unaoendelea.
Abella Rwegasira(ii)na Johanes Joseph(i) ni miongoni mwa wanafunzi waliolazimika kuacha masomo. Baba zao wamekimbia baada ya nyumba kuchomwa moto na wamepata hifadhi kwa majilani ambao pia wanasubiri zamu yao.
Watoto hawa wanadai kushuhudia uchomaji moto wa makazi yao kama alivyo Leonard Ereneus(36) aliyedai tukio hilo lilifanyika tarehe Juni 17 majira ya saa nne asubuhi.Anadai alikuwepo na alimuona mkuu wa wilaya akisimamia uchomaji.
Mgogoro umeficha mauaji na ubakaji.
Niko kwa Silvester Emanuel(36) mwananchi aliyeuwawa May 13 na wanaodaiwa ni askari wa mwekezaji wa kitalu namba kumi na tano. Mmoja wa wananchi hao Julius Kajungu anasema baada ya mauaji nyumba yake ilichomwa.Familia yake haijulikani ilipo na kaburi liko nje ya mabaki ya nyumba iliyoteketezwa na wauaji.
Watuhumiwa walishikiliwa kwa siku tatu katika kituo cha polisi na baadaye kuachiwa.Tangu kuachiwa wananchi wameendelea kuwa na hofu kwani ni askari wale wale wanaoranda kijijini wakitoa amri na vitisho kwa wananchi.
Wanadai kuachiwa kwao inatokana na nguvu kubwa ya mwekezaji na mahusiano ya karibu aliyonayo na viongozi wa serikali. Hii ni kesi ya mauaji inayoweza kuwa katika rekodi ya kutumia muda mfupi zaidi wa kufanya uchunguzi kwa watuhumiwa.
“Walifika asubuhi na kumtaka marehemu aondoke,tulikuta amefungwa mikono na miguu watuhumiwa wanajulikana wananchi wameogopa na kukimbia tumekatazwa kuwa tunatoa taarifa za matukio haya” alilalamika Julius Kajungu.
Wanalalamikia ubakaji na mauaji na kuwa watuhumiwa pamoja na kufahamika hakuna jitihada zozote za kuwatetea. Wanawatuhumu viongozi wa wilaya kwa madai ya kuonyesha upendeleo kwa mwekezaji.
Familia za Mwesiga Didas na Cyprian zinadai huenda ndugu zao waliuwawa kwani walipelekwa sehemu isiyojulikana na askari wanaomlinda mwekezaji. Mzee Fransis Bandihe (84) ana makovu mengi mwilini akidai alipigwa na askari. Nyumba yake imechomwa moto.
Mwanamke Dionizia Diocles(58) anasimulia yaliyompata Juni 5, baada ya kutishiwa na hatimaye kubakwa na askari. Anasema askari alifika nyumbani kwake akimtafuta mme wake akiwa na silaha begani, baada ya kumkosa alimwamuru kuingia ndani na kumbaka. Analalamika kuporwa pia kuku wake wawili.
Mme wake amekimbia na kuachiwa watoto wawili. Baada ya tukio hilo anadai alipeleka malalamiko kwenye kambi ya mwekezaji wanapoishi askari. Alidhani kuwa ndipo atakapopata msaada.
“Nilienda kambini niliwakuta maaskari na walisema watanisaidia, walinipa elfu ishilini wakasema nisiende kusema kijijini. Niliona nihame naogopa wanaweza kurudi tena hakuna hatua zaidi zilizochukuliwa” anabainisha mwanamke huyo.
Madai yake yanathibitishwa na muhtasari wa mkutano wa June 10,ambapo mwanamke huyo alitoa malalamiko yake dhidi ya ubakaji aliofanyiwa na kuwaomba wananchi wajadili jinsi ya kumsaidia.
Ni miongoni mwa wanawake wenye ujuzi mdogo wa sheria na wanaogopa kuyaripotiwi kwa kuogopa milolongo mirefu ya kisheria.Hawana uwezo wa kupambana na kundi la watu wanaoendeleza ukatili huku wakilindwa na sheria.
Takwimu zilizopo zinaonyesha ubakaji ulioripotiwa umeongezeka kwa asilimia 48 kutoka matukio 497 mwaka 1991 hadi matukio 736 mwaka 1992. Tangu wakati huo mpaka leo hali inaweza kuwa mbaya zaidi na matukio ya aina hii yanaficha ukubwa wa tatizo.
Anasema mbakaji anamfahamu na haamini kama kuna hatua zozote za maana zinaweza kuchukuliwa.Mwenyekiti wa kijiji hicho Ereneus Lwamashonga anakiri kulifahamu tatizo hilo na kuwa alishauri malalamikaji akafanyiwe vipimo.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora mwaka 2009 kiwango kikubwa cha ukatili kinafanywa na maofisa wanaotekeleza sheria. Asilimia 97 ya askari polisi wanahusishwa na vitendo hivyo ikiwemo vipigo na mauaji. Utafiti unawataja askari polisi kuwa wahalifu wakubwa wakifuatiwa na sungusungu.
Ni zaidi ya habari mbaya kwa askari wenye dhamana ya kuwalinda raia na mali zao kuhusihwa na vitendo vya ukatili na ubakaji. Wananchi wanadai haya ndiyo maisha yao ya kila siku yaliyojaa hofu na mashaka .
Utetezi wa mkuu wa wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Issa Njiku anasema migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika eneo lake imemalizika na kuwa kuna tatizo kidogo katika kijiji cha Bubare linalopandikizwa na watu wachache.
Kwamba hausiki kwa vyovyote na uchomaji wa nyumba kama anavyolalamikiwa na wananchi na kuwa aliwaagiza viongozi wa kijiji hicho kuwahamisha wananchi walioko katika maeneo ya mwekezaji na huenda ndiyo wanahusika na ukatili huo.
“Hili limeundwa na watu wachache kwa nia ya kuleta vurugu,wananchi wanaendelea na shughuli zao na uamuzi wa kuondoka au kubaki utategemea tume iliyondwa ambayo majibu yake hayajatolewa” alibainisha Njiku
Anasema serikali imepeleka askari kwa ajili ya kuwalinda raia na mali zao wala sio kumlinda mwekezaji. Kwamba askari hao wanafanya kazi ya kulisaka kundi la wananchi linalofanya mauaji dhidi ya wananchi.
Mkuu wa wilaya anaeleza kuwa tuhuma za askari kufanya vitendo vya ubakaji ni maneno ya mitaani na kuwa maeneo yenye mgogoro ni mali ya serikali na Kanati (mwekezaji) ni mpangaji tu. Anakanusha madai ya wananchi kuvamiwa na kukabiliwa na vitisho vya askari.
“Hakuna mwananchi yeyote aliyebakwa, tumepeleka askari kuwalinda raia na kulisaka kundi la wauaji, hakuna mifugo ya mwananchi iliyeuwawa na kuleta malalamiko kwangu” alibainisha akijibu tuhuma za Francis Bandiho aliyedai alipeleka malalamiko ya kuuliwa kwa mifugo yake katika ofisi yake.
Alipoulizwa hatima ya wananchi waliochomewa nyumba na wanafunzi walioacha masomo Njiku alisema suala hilo waulizwe viongozi wa kijiji aliodai amewahi kukutana nao na kujadili mgogoro unaoendelea kufukuta.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Salewi anakiri kufahamu uchomaji wa nyumba za wananchi hao na kuwa zoezi hilo liliendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.
Naye mwekezaji wa kitalu namba kumi na tano Nestory Kulinda hataki kuzungumzia lolote kuhusu mgogoro unaoendelea katika eneo lake ambaye pamoja na kuwa na ahadi ya kukutana baada ya kukagua miradi yake iliyopo visiwani hakuwa tayari tena kupokea simu yangu.
Hata hivyo wabunge wa mkoa wa Kagera Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) Asumpter Mshama (Nkenge) wanasema uwekezaji katika ranchi za Missenyi umegubikwa na vitendo vya unyanyasaji kwa wananchi na kupendekeza hati zilizotolewa zifutwe na utaratibu kupitiwa upya.