Kama zitakaza buti, harufu ya utajiri inazinukia Simba,Yanga

Jamii Africa

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga na Simba, wako kwenye kampeni za Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kuanzia Jumamosi hii Februari 18, 2012.

Kikosi cha Simba
Kombe la Shirikisho

Timu hizo mbili, ambazo hata hivyo maandalizi yake yamekuwa ya kusuasua, zinaweza kuogelea kwenye utajiri mkubwa ikiwa zitafanikiwa kufuzu kwa hatua ya makundi katika michuano hiyo.

Yanga inapambana na Zamalek ya Misri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mchezo wa kwanza wa raundi ya awali unafanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Cairo, na matokeo mazuri ya Dar es Salaam yanaweza kuiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye raundi ya kwanza.

Klabu hiyo bingwa ya Tanzania inatakiwa kufanya kazi ya ziada, japokuwa ni sawa na kuupandisha Mlima Kilimanjaro ukikimbia, ingawa katika soka lolote linaweza kutokea kama tulivyoshuhudia Zambia ikiwakosoa walioibeza kwa kutwaa ubingwa wa Afrika hivi karibuni.

Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika
Kikosi cha Yanga

Ikivuka raundi hiyo ya awali, Yanga itakumbana na mojawapo ya timu kutoka Afrika Magharibi – Missile ya Gabon ama Africa Sport ya Ivory Coast, ingawa mtihani utakuwa bado unaendelea kwa sababu katika raundi ya pili, endapo itafika huko, itabidi ipambane na mshindi katika mechi baina ya Ports Authority ya Sierra Leone au Horoya ya Guinea na Maghreb Association Sportive (MAS) ya mjini Fez, Morocco.

Kwa kuzingatia rekodi mbovu ya Yanga dhidi ya timu za Maghreb, pamoja na maandalizi ya kungaunga, wengi wanasubiri miujiza itende kazi ili timu hiyo iweze kufuzu kwanza kwa kuitoa Zamalek baada ya kushindwa kufurukuta mbele yake katika Kombe la Washindi mwaka 2000 ilipolazimisha sare tasa jijini Dar es Salaam na kubandikwa mabao 4-0 huko Cairo.

Lakini ikiwa itafanikiwa kuingia kwa mara ya pili kwenye hatua ya makundi, Yanga itavuna utajiri mkubwa wa Dola 400,000 (karibu Sh628 milioni za Tanzania) hata kama itashika mkia kwenye kundi lake.

Mshindi wa tatu katika hatua ya makundi ataondoka na kitita cha Dola 500,000 (takriban Sh785 milioni) wakati ambapo timu zitakazovuka kucheza nusu fainali kila moja italamba Dola 700,000 (takriban Sh1 bilioni).

Bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Dola 1.5 milioni (karibu Sh2.3 bilioni) huku mshindi wa pili akipata Dola milioni moja (Sh1.5 bilioni).

Hizi ni fedha nyingi, lakini haziwezi kuja kirahisi rahisi kwa sababu zinahitaji uwekezaji wa kutosha katika maandalizi ya timu pamoja na kuwa na mipango endelevu.

Itakumbukwa kwamba, mwaka 1998 wakati Yanga ilipofuzu kwa hatua ya makundi ilipata karibu Dola 40,000, lakini fedha hizo zikaishia mikononi mwa wajanja wachache na pamoja na Kamati ya Muda ya Tarimba Ghullam Abbas kupiga kelele, mpaka leo haijulikani ni nani hasa aliyefaidika nazo.

Tamaa ya baadhi ya viongozi wa soka ndiyo inayokwamisha maendeleo ya timu hasa linapokuja suala la fedha, kwani huwakatisha moyo wachezaji wanaojituma uwanjani.

Kwa upande mwingine, Simba wao wako kwenye Kombe la Shirikisho ambako wanaanza kampeni zao dhidi ya Kiyovu ya Rwanda. Timu hiyo kutoka Kigali siyo ya kuibeza kwa sababu inafanya maandalizi kwa makini na hivi karibuni rais Paul Kagame wa nchi hiyo aliipatia takriban Dola 30,000 kwa maandalizi ya kuikabili Simba.

Simba na Yanga uwanjani

Timu hizo zimewahi kupambana katika Kombe la Kagame mwaka 2004 wakati mashindano yalipofanyika mjini Kigali ambapo zilikuwa Kundi B pamoja na Gendarmarie ya Djibouti, SC Villa ya Uganda, na Muzinga ya Burundi.

Mechi baina ya timu hizo ilifanyika Mei 3, lakini ilizua utata baada ya timu hizo kupanga matokeo ili zote zifuzu kwa nusu fainali. Simba ilikuwa na pointi nne na Kiyovu ilikuwa imekwishafuzu ikiwa na pointi saba.

Villa ilikuwa na pointi moja baada ya kutoka sare na Kiyovu na kufungwa na Simba, na siku hiyo iliichabanga Gendarmarie ya Djibouti kwa mabao 7-0 hivyo kufikisha pointi nne, lakini tayari ilikuwa imechelewa kwa sababu Simba ilipanga ipate pointi moja ili ifikishe tano na kusubiri mechi yao ya mwisho dhidi ya vibonde Gendarmarie ambayo walikuwa na uhakika wa kuibuka na ushindi na kuipiku Villa.

Endapo siku hiyo Simba ingefungwa na Villa ikashinda dhidi ya Gendarmarie, nafasi ilikuwa finyu kwao kucheza nusu fainali kwa sababu ingelazimika kupata ushindi wa mabao mengi katika mechi yao ya mwisho. Lakini kwa ‘bahati’ Simba na Kiyovu zikatoka sare ya bila kufungana.

Wakati wa mapumziko, timu hizo ziliingia katika chumba kimoja na wachezaji wa timu zote mbili walikuwa wakipiga soga kana kwamba wote wanacheza timu moja.

Kitendo hicho kililalamikiwa na makocha na viongozi wa timu za Villa na Muzinga, lakini hakuna kilichofanyika. Simba ikashinda mechi yake ya mwisho kwa kuifunga Gendarmarie mabao 5-0 na Villa nayo ikaifunga Muzinga mabao 2-0, hivyo ikautema ubingwa baada ya kushika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi saba, moja nyuma ya Simba.

Safari hii kila mmoja anakufa kwa namna yake – Simba inahitaji kurejesha heshima yake kwa kufika mbali huku Kiyovu nayo, inayochagizwa na hamasa ya Rais Kagame mpenda michezo, ikitaka kufanya maajabu katika kandanda la kimataifa.

Endapo itaitoa Kiyovu katika hatua hii, Simba itakumbana na Entente Sportive Setifienne au ES Setif kutoka Algeria, ambayo imefuzu moja kwa moja hatua hiyo.

Kwa rekodi za Simba, haitakuwa na mashaka na timu za Maghreb kwani imekwishapambana nazo mara kadhaa na kupata matokeo yanayoridhisha.

Hata hivyo, kibarua kitakuwa kigumu kwa sababu itapaswa kuvuka raundi ya kwanza na kuingia raundi ya pili, ambako inaweza kupambana na ama Ferroviario de Maputo ya Msumbiji au Gor Mahia ya Kenya, au El Ahly Shandy ya Sudan.

Ikifanikiwa kuingia hatua ya makundi ina uhakika wa kuvuta kitita cha kuanzia Dola 150,000 (takriban Sh235 milioni) ikishika nafasi ya nne kwenye kundi lake au Dola 625,000 (karibu Sh982 milioni) ikitwaa ubingwa.

Mshindi wa tatu kwenye kundi atapata Dola 239,000 (karibu Shs375 milioni) wakati mshindi wa pili wa mashindano atanyakua Dola 432,000 (karibu Sh679 milioni).

Kazi ni kwao, na itategemea nani aliyenoa vyema kisu chake ili ale nyama.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *