Ukuaji wa huduma za miamala ya fedha kwa njia ya mtandao (mobile money) umetenegeneza fursa mpya kwa wafanyabiashara kutangaza na kuuza bidhaa na huduma zao. Moja ya fursa ambayo inavuma kama upepo wa dhoruba nchini ni ukuaji wa sekta ya ubashiri katika mchezo wa mpira wa miguu.
Kwa lugha nyepesi inatambulika kama ‘kubeti’ au ‘sport betting’. Kilichofanya sekta hiyo ikue ni ongezeko la matumizi ya intaneti hasa kwa vijana wengi wa Afrika. Wateja wa sekta hiyo wanaweza kupata huduma za kubashiri matokeo ya mpira wa miguu kwa njia ya mtandao popote walipo.
Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Ghana, Nigeria na Congo DRC zinashuhudia ukuaji mkubwa wa ubashiri katika michezo na aina zingine za kamari zinazochezwa kwa kutumia simu za mkononi za kawaida au zile zenye uwezo wa kupata intaneti.
‘Sport betting’ hufanyika kwa mtu kubashiri matokeo ya mechi ya mpira inayochezwa siku husika, ikiwa atabashiri/ atatabiri na timu fulani ikashinda dhidi ya nyingine hupata kiasi fulani cha fedha.
Ubashiri huo ambao hufanyika hasa kwenye ligi za mpira wa Ulaya na Ligi ya ndani (Vodacom Premier League), imekuwa ni sehemu yenye mzunguko mkubwa wa pesa. Asilimia kubwa ya ubashiri huo hufanyika kwa kutumia simu ambapo tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa majukwaa ya simu yanaibukia kuwa njia ya haraka ya kucheza kamali za mitandaoni.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani, Victor Odundo Owuor anaeleza katika moja ya makala zake kuwa ukijumuisha sekta ya kamali ya Kenya, Nigeria na Afrika Kusini inaweza kufikia Dola za Marekani bilioni 37 kwa mwaka 2018 pekee.
Anasema kuwa Kenya pekee inakadiriwa kuwa watu milioni 2 wanajihusisha moja kwa moja kwenye ubashiri wa matokeo ya mechi za mpira kwa njia ya simu. Wanaoshiriki zaidi ni vijana wasio na ajira ambao wanaamini kuwa ubashiri ni njia ya haraka kupata fedha na kuondokana na umasikini.
Kwa mukta huo, ni rahisi kuwaona vijana wakigombania fursa ya kubashiri matokeo ya ligi za mpira kwasababu sh. 1000 inaweza kuzalisha sh. 5000 na zaidi.
Inaelezwa kuwa nchini Nigeria, watu milioni 60 walio katika umri wa miaka kati ya 18 na 40 hutumia karibu Dola 5 (zaidi ya Tsh.100,00 ) kwenye ubashiri kila siku. Wengi wao hawana ajira na wanaishi kwenye umasikini wa kiwango cha juu. Fedha wanayoipata hutumia kujikimu kwa maisha ya kila siku.
Athari za ubashiri wa mpira wa miguu
Utafiti uliofanywa nchini Kenya umeonyesha kuwa watu ambao wanajihusisha zaidi kwenye ubashiri wa matokeo ya mpira wa miguu mtandaoni, wanafanya hivyo licha ya kufahamu kuwa kuna hatari mbele yao.
Hatari mojawapo ni kwamba vijana hao hukopa fedha ili wakabashiri matokeo ya mpira wa ligi. Hali hiyo huwaingiza katika mzunguko mkubwa madeni. Kadiri deni linapokuwa kubwa humuweka kijana kwenye wakati mgumu na kufanya maamuzi yanayoweza kugharimu uhai wake.
Licha ya kuwepo sheria zinazosimamia michezo ya bahati nasibu, lakini ubashiri umetawala akili za vijana na kuwafanya kuwa walevi (addictive). Wataalamu wa saikolojia wanahofia kuwa siku zijazo ubashiri utakuwa miongoni mwa sababu kubwa za magonjwa ya akili miongoni mwa vijana wengi wa Tanzania.
Mtafiti Owuor, anaeleza kuwa licha ubashiri au kamari kuwa na athari hasi kwa vijana lakini ni miongoni mwa sekta inayochochea ukuaji wa biashara ya fedha za mtandaoni.
Anaeleza kuwa miamala inayofanyika mtandaoni ndio njia pekee ya kuzinusuru benki ambazo zinakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji na madeni ya mikopo.
Upande wa pili, michezo ya ubashiri na bahati nasibu zinazofanyika kwa njia ya simu zinaongeza mapato kwa serikali kupitia kodi inayokatwa kwenye miamala ya simu.
Hata hivyo, serikali za Afrika ikiwemo Tanzania zimeshauriwa kutathmini na kuwasaidia vijana ambao hawana ajira ili kuwaepusha na madhara hasi ya ubashiri wa mtandaoni wa mpira wa miguu.