Wananchi vijijini walalamika kucheleweshewa huduma ya umeme.

Jamii Africa

Upatikanaji wa nishati ni nguzo muhimu kwa maendeleo na kupunguza umasikini katika jamii lakini kwa watanzania wengi bado imekuwa ni ndoto iliyokosa suluhisho la kudumu.

Inaelezwa kuwa asilimia 70 ya watanzania hawana nishati ya umeme kuwawezesha kuendesha shughuli za maendeleo licha ya Tanzania kuwa na vyanzo vingi vya nishati ya gesi asilia, makaa ya mawe, urani (uranium) na jadidifu (renewables) ambavyo bado havijatumika kikamilifu.

Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambayo kwa kushirikiana na serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini, imeeleza katika taarifa yake ya mwaka 2017 kuwa bado idadi kubwa ya watanzania hawajafikiwa na nishati ya umeme huku mahitaji ya nishati hiyo yakiongezeka kwa kasi.

“Asilimia 70 ya watanzania bado wanaishi bila umeme na mahitaji ya nishati hiyo yanaongezeka kwa kasi”, imeeleza taarifa hiyo iliyojikita kuelezea juhudi za pamoja za wadu wa maendeleo katika kukuza uchumi wa wananchi wa vijijini kwa kuwaunganishia nishati ya umeme katika shughuli zao za uzalishaji mali.

Kwa tafsiri ya kawaida ni kwamba watanzania 7 kati ya 10 hawana huduma ya umeme katika nyumba zao. Kwa muktadha huo umasikini unaowazunguka unaweza kusababishwa na ukosefu wa umeme.

Kwa mujibu wa AFDB, ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambao umefikia asilimia 6.8 unakabiliwa na changamoto ya ongezeko la mahitaji ya umeme ambayo yanachochewa na sera za uwekezaji na ujenzi wa viwanda.

“Hata hivyo, tukirejea kiwango kikubwa cha uchumi wa nchi, mahitaji ya umeme kwa Tanzania yanakua kwa 10% kila mwaka kwasababu ya uwekezaji katika sekta ya madini na viwanda pamoja na ongezeko la matumizi ya wateja waliounganishwa na wale wapya watakaounganishwa kwenye nyumba zao”, imeeleza taarifa hiyo.

Upatikanaji wa umeme kitaifa umeongezeka kwa asilimia 21 kutoka mwaka 2006 hadi 2016 lakini umebaki chini ya 30% ya kiwango kinachohitajika. Ukosefu wa umeme wa uhakika umeathiri zaidi wananchi wengi wa vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto za miundombinu ya kufikika kwa urahisi.

“Kwa wakazi wa vijijini upatikanaji wa umeme ni 11% tu- kiwango kinachowazuia kaya za vijijini kujihusisha na shughuli za kiuchumi na kunufaidika na huduma za elimu na afya”. Inabainisha ripoti hiyo.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati bungeni katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Waziri wa wakati huo, Prof. Sospeter Muhongo alinukuliwa kwa kusema, “Idadi ya wananchi waliounganishiwa umeme mjini imefikia asilimia 65.3 wakati waliounganishiwa umeme vijijini imefikia asilimia 16.9”.

Uzalishaji wa umeme sio changamoto pekee bali nchi inakabiliwa na matatizo ya mtandao wa usafirishaji na usambazaji kutokana na utendaji usioridhisha na uwekezaji mdogo wa rasilimali watu na fedha.  Pia ukame uliotokea katika kipindi cha mwaka 2012 na 2016 ulisababisha kupungua kwa uzalishaji wa umeme hasa katika mabwawa ya maji.

Hata hivyo, bado kuna fursa nyingi za uzalishaji umeme nchini ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano wa kuzalisha umeme wa maji (Megawati 4.7), makaa ya mawe (tani bilioni 1.9), gesi (trilioni 55 cubic feet) na nishati jadidifu ya upepo na jua. Zote zikitumiwa vizuri zinaweza kupunguza tatizo la umeme nchini hasa maeneo ya vijijini.

 

Mkakati wa muda mfupi…

Kutokana na Gridi ya taifa ya umeme kutowafikia wananchi wote hasa wale wa vijijini, mashirika mbalimbali yamejitokeza katika maeneo hayo kuhimiza wananchi kutumia umeme wa jua (solar power) ambao unaweza kutatua changamoto za kielemu kwa wanafunzi na uzalishaji.

Akielezea jinsi mradi wa solar ulivyobadilisha maisha yake kielimu, Asha Juma (11) mwanafunzi wa shule ya msingi Kiongozi iliyopo nje kidogo ya mji wa Babati mkoani Manyara amesema, “Tangu wazazi wangu waliponunua paneli ya solar (umeme wa solar), ninaweza kutumia taa kufanya kazi za nyumbani baada ya kwenda shuleni”.

Familia ya Asha ilijipatia betri lenye uwezo wa megawati 80 kutoka kampuni ya Mobisol inayoshirikiana na Benki ya AFDB kutatua changamoto ya umeme vijijini. Wanalipia huduma hiyo ya umeme kupitia simu ya mkononi ambapo wakimaliza malipo wanakabidhiwa vifaa vyote vya umeme wa jua.

Jambo la muhimu ni kuwa, familia ya Asha kama watanzania wengine hawalazimiki tena kutumia mafuta ya taa kupata mwanga kwasababu yanasababisha madhara ya kiafya. Mkakati huo unazidi kuenea kwenye shule, hospitali, vituo vya afya ili kuhakikisha wanapata umeme wakati serikali ikiendelea na mikakati ya muda mrefu kuzalisha umeme.

Serikali kupitia wizara ya madini imesema inaendelea na mipango ya kuhakikisha nishati ya umeme inayozalishwa inatumika vizuri ili kuwafikia wananchi wengi hasa wa vijijini, “Matumzi bora ya nishati ni suala linalotakiwa kupewa kipaumbele ili kupunguza upotevu wa nishati kuanzia uzalishaji, usafirishaji, usambazaji  hadi mtumiaji wa mwisho.

“Kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na TANESCO zikiwemo za kukarabati na kuwekeza katika njia za usafirishaji na usambazaji wa umeme, upotevu wa umeme umepungua kutoka ailimia 21 ya mwaka wa fedha wa 2015/2016 hadi asilimia 17 ya mwaka 2016/2017.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *