Kamati ya Bunge yawahoji DC, OCD sakata la uchomaji nyumba Missenyi

Jamii Africa

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imewahoji watu mbalimbali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Issa Njiku, ambaye anatajwa kuamuru kuteketezwa kwa nyumba zaidi ya thelathini kwa moto katika kijiji cha Bubare kama shinikizo la kuwahamisha wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Neema Mgaya Hamid, amekiri kuhojiwa kwa kiongozi huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa katika mzozo na wananchi wakimtuhumu kufumbia macho vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na wawekezaji.

Kamati hiyo ya Bunge pia imewahoji baadhi ya viongozi wa polisi ngazi ya wilaya ambao inadaiwa walipewa amri na mkuu wa wilaya ya kuendesha zoezi la uteketezaji wa nyumba katika kitongoji cha Kazizi huku yakiwepo madai ya polisi kutumika kuwabambikizia wananchi kesi kama njia ya vitisho vya kuwataka kuhama.

Awali Fikra Pevu iliandika habari juu ya ‘Kitendawili cha uchomaji wa nyumba 36‘ na nakala kusambazwa kwa viongozi na mamlaka mbalimbali wakiwemo wabunge ili ufuatiliaji ufanyike.

Akiongeza na Fikra Pevu Makamu Mwenyekiti huyo alikiri kuhojiwa kwa viongozi hao wa dola huku akikataa kuweka bayana kilichozungumzwa na kukwepa kuzungumzia tuhuma za kiongozi huyo kuhusishwa na uchomaji wa nyumba za wananchi.

“Hata kama kamati imemhoji DC siwezi kukwambia kilichozungumzwa,wananchi wamezungumza mambo mengi sana sio kazi yetu kupeleka taarifa kwenye vyombo vya habari,tumeishamaliza kilichobaki ni kuishauri serikali kile tulichobaini,”alisema Neema Mgaya Hamid, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM.

Tume hiyo imewahoji viongozi hao baada ya kupokea maoni na malalamiko kutoka kwa wananchi wa  vijiji vya Bubare na Kakunyu ambao wameendelea kuharibiwa mali na makazi yao wakilazimishwa kuwapisha wawekezaji.

Katika mkutano wa wabunge hao na wananchi wa kijiji cha Bubare mwishoni mwa wiki wananchi walilalamikia vitendo vya ukatili vinavyoendelea ikiwemo ulishaji wa mifugo katika mashamba yao na hata kupotea kwa baadhi ya wananchi katika mazingira yenye utata.

mukasa

Picha Faustin Mukasa mwanafunzi wa kidato cha tatu toka Shule ya Sekondari – Kakunyu akionyesha kovu lililotokana na kupigwa risasi na askari wa mwekezaji.

Mmoja wa wananchi hao Julius Kajungu alisema kuwa, pamoja na kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya imeendelea kuvifumbia macho.

Baadhi ya matukio yanayotia shaka ni pamoja na uongozi wa dola wilayani Misenyi kutojishughulisha na tukio la kuuwawa kwa mwanakijiji Silvester John aliyedaiwa kuuliwa na walinzi wa mwekezaji mmoja wa kitalu namba 15 wilayani humo mwaka jana.

Pia mwananchi mwingine katika mkutano huo Plaxseda Faustin alilalamikia kung’olewa kwa ekari tatu za mazao yake na kuwa hata baada ya kupeleka malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya hakupewa msaada wowote.

mwanamke akiwa nje ya nyumba inayodaiwa kuteketezwa kwa moto na mkuu wa wilaya.jpg

Mwanamke akiwa nje ya nyumba inayodaiwa kuteketezwa kwa moto na mkuu wa Wilaya

Katika mkutano huo mwananchi Daud Kateshumba alieleza kusikitishwa na viongozi wa wilaya kuwakingia kifua wawekezaji hata wanapofanya vitendo vya kikatili na kueleza jinsi walivyoathirika na uchomaji wa nyumba za wananchi bila kupewa msaada wowote na viongozi wa wilaya.

Wabunge wengine walioambatana  na Makamu Mwenyekiti ni Dokta Titus Mlengeya Kamani (Busega), Seleman Said Jafo (Kisarawe) Waride Bakari Jabu na Asaa Othman Hamad kutoka Zanzibar ambao pia walitembelea kijiji chenye mgogoro katika ranchi ya Kagoma wilayani Muleba.

Imeandikwa na Phinias Bashaya, mwandishi wa Fikra Pevu – Kagera

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *