KAMATI YA UKIMWI YAVUNJWA WAKATI IPO JAMII INAISHI KWA VIRUSI VYA UKIMWI MWADUI LOHUMBO.

Belinda Habibu

Na: Belinda Habibu.
Kamati ya ukimwi iliyoundwa mwaka 2008, imekufa kwasababu ya wanachama wengi kuhitaji posho ambayo haijulikani itatoka wapi.
Hii ni kauli ya afisa mtendaji wa kijiji cha Mwadui Lohumbo,wilayani Kishapu, mkoa wa Shinyanga,Musiba Atanasi aliyesema tulihamasishwa na dada mmoja alikuja sijui kutoka wapi vile hata nimesahau ,ndio tukaunda kamati hii ya watu 16.
Ameongeza kilichokwamisha isiendelee na kazi ya uhamasishaji,ni fikra za wajumbe kuwa tunapokutana basi kuna fungu la hela limeandaliwa na walivyoona halipo basi wakajitoa.
“Mimi,mwenyekiti wa kijiji tulikuwa miongoni mwa watu ndani ya kamati hii,na tusingeweza kuwa peke yetu”alisema afisa mtendaji huyo.
Wakati hilo linatokea katika kijiji hicho , kuna zaidi ya waathirika 44 waliojiunga katika vikundi viwili, kile cha Upendo na kingine kinaitwa Amani,na ushuhuda wa kuwepo watoto wawili waliothibitika wanatumia dawa katika kijiji hicho wanaosoma katika shule ya msingi ya Mwadui Lohumbo
Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Elisifa Michael alisema wanatoa elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na jinsi ya kujikinga na maambukizi,kwa kuwa wanaona wao jinsi walivyopata na jamii ilivyo kwa sasa kitabia.
“Sisi tunapewa mafunzo kule mwadui mgodini na wakati mwingine kutoka wilayani, tukirudi tunatoa elimu tuliyoipata kwa wengine, kwenye mkutano wa kijiji”aliongeza mwenyekiti huyo.
Aliongeza hatufanyi maramara kwa mara kutokana na hali ngumu tuliyonayo sisi tulioathirika na VVU,utakuta mara mwenzetu anaumwa,mara nyingine huna chakula inabidi ukafanye biashara ili upate hela kidogo.
Mjumbe wa kikundi hicho Halima Juma Nkwabi alisema changamoto zipo nyingi kama jinsi ya kujikinga,na elimu inahitajika sana, sisi tunatoa semina ila mapokeo ya watu inategemea na maamuzi yake na hata hivyo hatuwezi kuwafikia wote.
Frank Vitusi anasema elimu ya ukimwi hapa kijijini (Mwadui Lohumbo) haipo,kwa sababu hatujui hata matumizi ya kondom tunaangalia tu picha iliyowekwa juu ya boksi lake ndio tunatumia.
Alisema ndugu mwandishi,akina dada wa hapa kwetu,hawapendi mwanaume atumie kondomu,na kingine ni uwelewa wa matumizi ya mipira hii,lakini sisi wenyewe, tunajuana nani ana ugonjwa huu na nani hana,hivyo kama unajijali mazingira haya,inabidi utumie kondom lakini si wote wanafanya hivi.
Akizungumzia suala la kupewa ama kutolewa kwa elimu kuhusu VVU,Vitus aliongeza kusema,hapo kijijini wanapewa walioathirika wakienda hospitali,zahanati na katika mkutano wa kijiji hajawahi kuona ikitolewa.
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu Japhet Makelele alisema elimu inaendelea kutolewa na kuna kamati za afya za kuhamasisha masuala ya afya kwa kila kijiji,kikiwemo cha Mwadui Lohumbo.
Mratibu wa TASAF, wilaya ya Kishapu Rehema Edson,alisema hakuna kamati iliyokufa,kwa uzowefu wangu wa kazi vijijini, watu wake kutokana na hali ngumu ya maisha wanapomuona mgeni wanahisi kupata chochote ndio maana wamesema hivyo.
Katika moja ya kanuni za sera ya taifa ya kudhibiti ukimwi ya mwaka 2001,inasema kipengele C,kwamba msukumo na uongozi madhubuti wa siasa na serikali katika ngazi zote ni muhimu katika kushiriki kwa ukamilifu kwenye vita dhidi ya VVU/UKIMWI.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *