Wajawazito Tanzania wakimbilia kujifungulia Malawi

Gordon Kalulunga

SERA ya Afya ya mwaka 2007 haifahamiki wilayani Ileje katika mkoa wa Mbeya. Ni katika sera hii ambamo inatamkwa kwamba wajawazito nchini watapewa huduma za afya bure.

Kama sera inafahamika, basi haitekelezwi. Baadhi ya wajawazito katika wilaya ya Ileje wanaacha zahanati, vituo vya afya na hospitali wilayani mwao na kuvuka mpaka hadi nchini Malawi kufuata kinachoitwa “huduma bora.”

Kwa mfano, wajawazito kutoka kata za Bupigu, Itumba na Isongole wanafahamika kwa kwenda nchini Malawi kwa wingi ili waweze kujifungulia huko na kupata huduma nyingine za afya.

Lakini kutoka Isongole hadi hospitali maarufu ya Chitipa nchini Malawi ni umbali wa kilometa 45; wakati umbali wa kwenda hospitali ya serikali ya Ileje ni kilomita tatu tu.

Mwanamke mkazi wa kijiji cha Ikumbilo, kata ya Chitete wilayani Ileje, aliyejitambulisha kuwa anaishi na virusi vya ukimwi (VVU) anasema aliwahi kujifungulia hospitali ya Chitipa na mpaka sasa anapata matibabu yake huko.

Kuna nini katika hospitali ya Chitipa nchini Malawi hadi wajawazito wakimbilie huko? Jibu analo Neema Mbughi mkazi wa kijiji na kata ya Bupigu.

“Pale hospitali ya Chitipa hubebi chochote wakati unakwenda kujifungua. Hatuendi na madishi, karatasi za nailoni (ambako mjamzito huhala wakati wa kujifungua) wala glovu. Kila kitu ni bure, hata chakula ambacho kimepikwa kama kimetoka nyumbani,” anaeleza Neema.

Wilaya ya Ileje ina hospitali kubwa mbili – hospitali ya serikali mjini Ileje na ile ya misheni ya Isoko. Hizi ndizo hospitali ambazo zinategemewa kwa huduma ya uzazi.

Wanawake wapatao 27 waliohojiwa, pamoja na kutofautiana katika mambo mengine, wengi waliafikiana kuwa katika hospitali ya Chitipa, wauguzi wanatumia “lugha nzuri” inayompa matumaini mjamzito.

Sababu nyingine walizotaja ni kutotozwa fedha yoyote ikiwa gharama kwa kujifungulia hapo; kupewa dawa zinazohusiana na uzazi bila kulipia na kupewa chakula bure.

Hivi wanapitaje mpakani penye idara ya uhamiaji? Jibu unalopewa ni kwamba hawapiti mpakani kwenye ofisi za serikali. Wanapita kwenye njia zisizorasimi ambako wanaita “njia za panya.”

Wakifika hospitalini Chitipa wanajieleza kuwa wanatoka vijiji vya ndani ya Malawi – wengine wakitaja hata ndugu zao na viongozi katika maeneo hayo kuthibitisha kuwa wanatoka humohumo.

’Neema anasema wanalazimika kusema kuwa wanatoka Malawi “…ili tuweze kupata huduma za kliniki, mahali bora na bure pa kujifungulia na matibabu mengine.”

Siyo wajawazito peke yao wanaoingia Malawi kwa matibabu. Wananchi wengine huenda hospitali za Chitipa na Kameme kupata matibabu; tena bila kutozwa fedha zozote.

Henry Kayuni, mkazi wa Bupigu anasema licha ya kufuata matibabu na mahitaji mengine kama mafuta ya taa, mbegu za mahindi, sukari na mbolea, baadhi yao wanapeleka pia watoto wao shuleni.

Anasimulia kwamba kujieleza kuwa unatoka Malawi kunasaidia “…hata kusomesha watoto nchini humo mpaka Darasa la VIII. Baada ya hapo wanakuwa tayari wamejua vema Kiingereza; ndipo wanahamishiwa Tanzania na kuwaombea nafasi Kidato cha II.”

Lida Kibona wa kijiji cha Itumba, anasema yeye alianza kupata matibabu bure katika hospitali ya Chitipa hata kabla hajapata ujauzito na kwamba manesi na madaktari “wanasikiliza na kujali sana wagonjwa.”

Kuna kichocheo kingine kwa wananchi wa Tanzania kutibiwa Chitipa. Katika mahojiano nao Novemba mwaka jana walieleza, mmoja baada ya mwingine, kuwa ikitokea “bahati mbaya” mama au mtoto akafariki na wakati huo umejitambulisha kuwa unatoka Tanzania, basi inasafirishwa hadi mpakani bila gharama yeyote.

Katika hospitali za mkoani Mbeya karatasi la kutandika wakati wa kujifugua linauzwa kwa Sh. 3,000, paketi ya glovu Sh. 2000, beseni Sh. 3,000 na kama mjamzito amelazwa, basi hujitegemea pia kwa chakula.

Jane Kabuje mkazi wa kata ya Isongole anasema kuwa yeye ni mmoja wa wanawake wanaopata huduma za afya Chitipa nchini Malawi ingawa hospitali ya wilaya ya Ileje ipo jirani na kata yake.

Mkazi wa Bupigu wilayani Ileje, Amos Shimwela anasema tatizo linalowakumba wakazi wa vijiji vya mpakani hadi kuamua “kujitambulisha” kama raia wa Malawi, ni kutokana na kutopata huduma za afya nchini ambazo alisema ni ghali wakati nchini Malawi ni bure.

Naye mkazi wa kijiji cha Bulambya, Joseph Kapange anasema bora kujitambulisha kuwa ni raia wa nchi nyingine ili upate huduma, kuliko kung’ang’ania utokako ambako hupati huduma muhimu kwa afya yako.

Anasema wakati matibabu katika hospitali ya Chitipa na huduma kwa wajawazito ni bure, nchini Tanzania bado wanatozwa fedha na wengi wanashindwa hata kulipa Sh. 500 ili kupewa kadi ya kumwona daktari.

Hata wanaomudu kulipa kiasi hicho cha fedha, bado wanalazimika kununua dawa katika maduka nje ya hospitali.

Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Minga, anasema baadhi ya wanaume wamekuwa wakipeleka wake zao wajawazito katika hospitali ya Chitipa miezi mitatu kabla ya kujifungua.

Amesema hii ni kwa tahadhari kwa vile wanaishi mbali na hospitali hiyo; na kwamba hawataki kusubiri hadi wajawazito wazidiwe, “…kwani usafiri wa barabara siyo wa uhakika.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *