Kashfa Mpya: Mganga Mkuu ashindwa kuagiza kuondolewa vipimo vibovu vya VVU nchini!

Jamii Africa

Mganga Mkuu wa Tanzania (Chief Medical Officer) Dr. Deo  Mutasiwa  (pichani) amedaiwa na wadau mbalimbali wa masuala ya afya nchini kwa kushindwa kutoa maagizo ya kuondolewa kwa vifaa vya kupimia virusi vya Ukimwi (HIV) kufuatia taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa vifaa hivyo vina kasoro kubwa na hivyo vinapaswa kuondolewa kwenye matumizi ya binadamu mara moja.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika Dr. Mtasiwa alipokea barua toka Shirika hilo ikimtaarifu juu ya mapungufu hayo makubwa ya vifaa vya SD Bioline HIV-1/2 3.0 vinavyotengenezwa huko Korea ya Kusini na kampuni ya Standard Diagnostic ya Jiji la Kyonggi-do.  Hata hivyo tangu kupokea taarifa hiyo toka WHO pamoja na taarifa toka kampuni ya Standard Diagnostic yenye kuthibitisha maamuzi ya WHO Dr. Mtasiwa hajachukua hatua yoyote ya kutahadharisha wanunuzi na watumiaji wa vifaa hivyo ambavyo vingi vinamuda wa matumizi unaoishia mwaka 2012 na 2013. Maisha ya vifaa hivyo ni miezi 24 (sawa na miaka miwili) kabla havijaondolewa kwa kupita muda wake wa matumizi.

Kutokana na kinachodaiwa kuwa ni uamuzi huo wa Dr. Mtasiwa ambaye anatajwa na vyanzo mbalimbali kuwa na “ushawishi mkubwa pale Wizarani” hata kuzidi baadhi ya watendaji wa juu maisha ya wananchi wa Tanzania yako hatarini  kwani matumizi ya vifaa hivyo ambavyo WHO imesema inauwezekano wa kuwa na uharibu wa asilimia 50 majibu yanayotolewa kupitia vifaa hivyo yaweza kuwa na makosa makubwa.

Shirika la Afya Duniani lilitoa taarifa kuwa kufuatia uchunguzi wake vifaa hivyo vilionekana kuwa na mapungufu yasiyokubalika katika kundi la vifaa vyenye namba 023419 na 023418B ambavo vina tarehe ya kutumiwa mpaka August 30, 2013 na Augusti 2, 2013. Shirika jingine la kusimamia Ugavi wa Vifaa vya Tiba la The Partnership for Supply Chain Management (PSCM) nalo limegundua mapungufu hayo katika vifaa vinavyotoka fungu lenye namba 023424B ambalo lina tarehe ya mwisho wa matumizi ya Augusti 18,2013. Vile vile PSCM wameona tatizo kwenye fungu jingine la vifaa vyenye namba 023425.

Kutokana na hilo taarifa ya WHO imetangaza kuwa “Vifaa vya SD Bioline HIV-1/2 3.0 vitaondolewa katika orodha ya WHO na hivyo havitaweza kuagizwa Who au taasiso yoyote ya Umoja wa Mataifa hadi itakapotolewa taarifa nyingine”.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo kampuni ya Standard Diagnostic iliipa uzito wa juu kabisa kwani tarehe 21 Novemba, 2005 siku karibu tano tangu taarifa ya WHO itoke ilitoa tangazo lake kwa waagizaji na taasisi zote za afya ambazo zinatumia vifaa hivyo kuviondoa mara moja na kutoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo. “Lengo la barua na ushauri wa taarifa hii  ni kukutaarifu kwamba Standard Diagnostics imeagiza kuondolewa kwa hiari (voluntary recall) ya vifaa vya SD Bioline HIV ½ 3.0” Shirika hilo limetaja kuwa vifaa ambavyo vinatakiwa kuondolewa mara moja kutoka matumizi ni vile vya fungu la 023418, 023418B, 023419, 023424, 023424B na 023425B. Agizo la SD linasema kuwa “tafadhali ondoa mara moja vifaa vyote vyenye namba hizo”

Uamuzi huo wa SD umekuja kufuatia uchunguzi wake ambao nao umeonesha kuwa vifaa kwenye mafungu hayo vinakasoro ya kati ya asilimia 10-15 ya vifaa vyote. Hata hivyo, upungufu wa kila kifaa katika utendaji kazi wake kwenye kundi hilo ni kati ya asilimia 10 hadi 50. Pamoja na hilo SD imeagiza hatua kadhaa kuchukuliwa na wateja wake (hii ni pamoja na mawakala wake) pote duniani:

–          Kusitisha maramoja matumizi na mauzo wa vifaa hivyo kutoka

–          Kuacha kutumia vifaa hivyo mahali popote na taarifa ya kufanya hivyo itumwe kwa Fax kwenye shirika hilo. Vile vile, mawakala wa kampuni hiyo wanatakiwa kutoa taarifa kwa wateja wao (kama Wizara ya Afya ya Tanzania) kuhusiana na uamuzi huo.

–          Baada ya kupata majibu toka kwa wateja madalali wote wahakikishe kuwa vifaa vyote vilivyotakiwa kuondolewa sokoni viwe vimeondolewa katika muda uliowekwa.

–          Mawakala wa kampuni hiyo watoe taarifa ndani ya siku kumi kuwa wamepokea taarifa hiyo toka SD wakielezea kiasi cha vifaa walivyonavyo au walivyokwisha uza.

Barua hiyo ya SD ilisainiwa na Meneja wa Usimamizi wa Ubora wa Standard Diagnostics Bw. Young-ah Chae. Barua ya Bw. Chae ilikuwa imeambatanishwa na fomu zote muhimu kwa mawakala kuweza kukamilisha zoezi hilo.

Uchunguzi wa FikraPevu na mtandao wa JamiiForums.com ambao ulikuwa unafuatilia kwa muda wiki zote hizi tangu agizo la WHO kutolewa umeonesha kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hadi hivi sasa bado imeachilia vifaa hivyo kuendelea kutumika nchini huku wakala mkubwa wa kampuni ya Standard Diagnostics nchini akitumia ushawishi wake mkubwa wa kisiasa na fedha kuhakikisha kuwa Wizara ya Afya haiagizi kuondolewa kwa vifaa hivyo nchini.

Tanzania imejikuta ikihusishwa na vifaa hivyo ambavyo vimekuwa vikitumika nchini kwa muda mrefu sasa tena kwa maelfu yake baada ya kutajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo ziliingiza nchini vifaa hivyo kati ya mwaka 2010 na 2011. Tanzania ilianza kuingiza vifaa vya SD Bioline baada ya kusitisha matumizi ya vifaa vya kupimia vya Cappilus HIV Test ambavyo vilikuwa vinaingizwa kutoka Ireland.

Katika kile kilichotajwa kuwa ni kashfa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baadhi ya watendaji walihisiwa kuhusika na sakata hilo ili kushawishi Serikali ya Marekani kufadhili uingizwa wa vifaa vya SD Bioline kutoka Korea ya Kusini. Mwezi Oktoba 2007 Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa imefadhili uingizwaji wa vifaa milioni 3 vya SD Bioline kwa ajili ya kusaidia katika harakati za kupima maambukizi ya HIV katika kuitikia wito wa Rais Kikwete wa watu kujitokeza kupima hali zao za HIV.  Marekani iliagiza vifaa hivyo moja kwa moja kutoka Korea ya Kusini kwa Gharama ya dola milioni 2.4.

Hata hivyo baadaye kampuni ya SD Bioline ya nchini “ilishinda” tenda ya kuingiza vifaa hivyo katika kile ambacho uchunguzi wetu umeonesha kuwa ni “kubebwa” kwa hali ya juu kwa wakala wa kampuni hiyo ambaye jina lake
(limehifadhiwa). Wakala huyo raia wa Korea ya Kusini ambaye hadi hivi sasa hajaanzisha utaratibu wa kuviondoa vifaa hivyo sokoni wala kuisukuma Serikali ya Tanzania kutekeleza wito wa WHO. “Huyu bwana anadai kuwa yeye ni mfadhili mkubwa wa CCM na hata serikali ya Tanzania ‘iko mfukoni’” kimesema chanzo chetu cha kuaminika.

Kwa mujibu wa chanzo hicho ofisi za Wakala wa SD Bioline ziko katika Jengo la Makao Makuu ya CCM jijini Dar-es-Salaam ambapo pia anazo ofisi zake nyingine za kampuni yake binafsi ya SD Green Limited ambayo kwa mujibu wa uchunguzi wetu wa awali unaonesha inamiradi ambayo inafanya na Chama cha Mapinduzi. Pamoja na uhusiano wa karibu na CCM Mkorea huyo (ambaye ametajwa kwa jina moja la “James” vile vile anatajwa kuwa na ushirika au uhusiano wa karibu na viongozi wa juu wa Wizara akiwemo Daktari Mkuu Bw. Deo Mtasiwa ambaye tetesi zinatajwa kuwa anaweza kuteuliwa kushika wadhifa mkubwa siku za karibuni kama “zawadi” yake ya ushirika huu.

Matokeo ya kuendelea kutumiwa kwa vipimo hivi ambavyo tayari vimeoneshwa na Shirika la Afya Duniani pamoja na watengenezaji wake kuwa vina kasoro kubwa na vinatakiwa kuondolewa vinaweka maisha ya Watanzania matatani. Uwezakano wa watu ambao hawana virusi vya UKIMWI kujikuta wanaambiwa wanavyo au wasio navyo kuwa wanavyo kwa kutumia vifaa vibofu (ambavyo vimeaminika huko nyuma kwa ujumla wake) una madhara kwa afya za maelfu ya watumiaji wa vifaa hivyo.

“Inakuwaje kama mtu ambaye ameambiwa kuwa hana VVU akaenda na kuamini kuwa hana na kwenda kuingia katika ngono bila kinga akijiamini kumbe vipimo vilivyotumika vina kasoro?” amehoji mpashaji wetu habari ambaye alizungumza kwa hisia kali. “Unajua ufisadi una madhara mengi lakini hakuna madhara zaidi kama yale ya kugusa moja kwa moja maisha ya watu” alisema mtoa habari huyo.

Mmoja wa wananchi ambao aliwahi kupimwa kwa kutumia kifaa hicho kwenye moja ya taasisi zenye kupima VVU Jijini Dar ameshtushwa na uwezekano kuwa vifaa vilivyotumika kumpimia mapema mwaka huu unaoisha vyaweza kuwa na makosa. “Kwa kweli hili si jambo zuri maana sasa inabidi tuambiwe kama sisi tuliotumia vifaa hivyo tujipime tena au la na itakuwaje kwa wale ambao waliambiwa hawana VVU kumbe wanavyo au kinyume chake?” alihoji akiwa na sauti ya wasiwasi.

Juhudi za Fikrapevu na JamiiForums kuwapata wasemaji wa Wizara akiwemo Katibu Mkuu Bi. Blandina Nyoni pamoja na Mganga Mkuu Dr. Deo Mtasiwa zimeshindikana ili kuweza kupata maelezo yao ni kwanini hadi hivi sasa Tanzania haijaitisha kuondolewa kwa vifaa hivyo nchini au kuwaambia watumiaji na wauzaji kufanya nini kama vifaa hivyo vikiondolewa. FP na JF vitaendelewa kuwatafuta watendaji hawa ili waweze kutolea maelezo ni kwanini hadi hivi sasa Wizara ya Afya imekuwa kimya kwenye jambo nyeti kama hili.

Hata hivyo, dalili zote za uchunguzi huu zinaonesha hali ya kuogopana ikiwa imetawala katika Wizara ya Afya huku baadhi ya watendaji wakiogopa kuchukua maamuzi magumu kwa kuhofia kuwa wanaweza kujitangazia maadui wenye nguvu na wengine kuhofia kuwa kwa kujitokeza hadharani kupinga kucheleweshaji wa kuondolewa kwa vifaa hivi vibovu kutakuwa ndio mwisho wa ajira zao na hivyo wameamua kukaa kimya ili kutetea vitumbua vyao visiingie mchanga.

Barua ya WHO

Na. M. M. Mwanakijiji na Timu

3 Comments
    • sasa kama ilifika kipindi Tanzania waliachia vifaa vibovu kuingia,viongozi husika kazi yao ni nini?unajua siajabu kuna watu walipima kutumia vifaa hivyo na kupewa majibu yasiyo yao,unadhan what nex kama mtu aliambiwa ameathirika wakati hajaathirika?or akaambiwa hajathirika wakati ameathirika,viongozi wet tunapaswa kuwa makini kwenye Afya za Watu,tusiingize politics kaika mambo ya muhm kama afya za watu jamani

  • Uliyekwishafanya checkup just go and do it again kwenye vituo zaidi ya viwili. Kila kitu kinachoendelea kwenye nchi hii si kigeni, hilo pia ni moja ya maelfu ya udhaifu na madudu yanayofanywa na watendaji wa serikali kwenye idara mbalimbali.

    Mimi sishangai kwakuwa sielewi ni eneo lipi linalofanya vizuri miongoni mwa idara zote za serikali, karibu kila eneo malalamiko.Ni vyema wananchi pindi wapatapo habari kama hizi wakachukuwa hatua za haraka kabla madhara zaidi hayajajitokeza kwao maana wao kila kukicha yanapojitokeza mambo kama haya ndiyo wanaokuwa victims namba moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *