Katavi: Muuguzi alazimika kufanya kazi ya daktari wilayani Mlele

Jamii Africa

OPERESHENI ya uhakiki wa vyeti feki vya elimu na taaluma nimesababisha mhudumu wa afya katika Zahanati ya Majimoto, Kata ya Majimoto wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi kufanya kazi ya udaktari.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, zahanati hiyo ni moja kati ya zahanati nyingi mkoani Katavi ambazo watumishi kadhaa wamezolewa na zoezi la uhakiki wa vyeti feki, hivyo kuongeza ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya.

Akinamama wakiwa wanasubiria huduma katika Zahanati ya Majimoto.

Zahanati hiyo iliyofunguliwa miezi kadhaa iliyopita ikilenga kuhudumia kaya 6,000 za Majimoto zinazohusisha wakulima na wafugaji wanaoishi Mpimbwe inakabiwa na uhaba wa madaktari na wauguzi kiasi kwamba kwa sasa mhudumu ndiye anafanya shughuli za kuwatibu wagonjwa zinazotakiwa kufanywa na mganga mfawidhi wa zahanati.

“Pamoja  na Kata hii kuwa na idadi kubwa ya watu, watumishi wa afya tulioajiriwa tupo wawili tu; Mganga wa Zahanati na mhudumu. Wahudumu wengine wawili waliopo hapa ni wa kujitolea,” Maria Leonard, mhudumu anayefanya kazi ya udaktari, aliieleza FikraPevu.

Maria anasema hulazimika kufanya kazi ambazo kitaaluma si za kwake, bali zilipaswa kufanywa na mganga wa zahanati, hasa pale inapokuwapo dharura au mganga akiwa amesafiri nje ya Kata.

“Huwa ni usumbufu sana nyakati za asubuhi kwani idadi ya wagonjwa huwa kubwa wakati wahudumu ni wachache. Sijui itakuwaje mmoja wao akidaiwa kuwa na cheti feki,” anasema Maria.

Hofu hiyo imewakumba pia wananchi wa kawaida ambao wanasema ikitokea hata watumishi wa kujitolea kwenye zahanati hiyo wakakumbwa na zoezi hilo hali itakuwa mbaya zaidi.

“Hii ikitokea basi hali itakuwa mbaya zaidi. Tunachofanya kwa sasa ni kuomba Mungu isitokee hali hiyo. Hata kwa sasa watu hatupati huduma za afya kwa wakati sasa wahudumu wakipungua sio hatari hii?” anasema na kuhoji mwananchi mmoja wa Majimoto.

FikraPevu ilishuhudia baadhi ya watu wenye wagonjwa hasa wenye uwezo wa kifedha wakienda kupatiwa matibabu katika zahanati ya mtu binafsi au wakienda kununua dawa moja kwa moja kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi.

Mbali na uhaba wa watumishi, Maria anasema changamoto nyingine inayowakabili kama watoa huduma ni uhaba wa vyumba vya kutolea huduma.

“Kwa hakika vyumba ni vichache sana kulinganisha na idadi ya wagonjwa wetu. Hebu fikiria, chumba maalumu cha kujifungulia kipo kimoja tu!

“Chumba chenyewe kipo hapa hapa katika jengo linalotumika kwa ajili ya kutoa huduma nyingine za tiba. Hakuna faragha! Hii haipendezi pale wengine wanapokuwa wakihudumiwa wakati huo huo huduma ya kujifungua ikiendelea,” Maria ameieleza FikraPevu.

 

Wilaya ya Tanganyika pia

Hali ya uhaba wa watumishi imeielemea pia Wilaya mpya ya Tanganyika mkoani humo ambayo iko katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, hata kabla ya kuwa wilaya, hali ya kijiografia ya eneo la Tanganyika kwa miaka mingi imekuwa ikisababisha kukumbwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali.

Ukiacha viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani, wenyeviti wa mitaa na vitongoji, wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba wa walimu, wauguzi, madaktari, maaskari na hata mahakimu.

FikraPevu imeambiwa kwamba, Serikali mkoani Katavi imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kukabiliana na uhaba huo ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu na wauguzi waliokuwa tayari kwenda kufanya kazi maeneo hayo.

Lakini sasa, mtikisiko uliosababishwa na msako wa wafanyakazi wa Serikali wanaodaiwa kughushi vyeti vya elimu pamoja na vile vya taaluma umeiathiri wilaya hiyo, hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika na kusababisha kudorora kwa huduma za afya.

Akizungumza na FikraPevu, Diwani wa Ikola, Karema mwambao wa Ziwa Tanganyika, Philemon Moro, anasema moja kati ya zahanati zilizoathirika ni ile ya Isengule katika Tarafa ya Karema.

“Wauguzi tuliokuwa nao pale kwa sasa hawapo kazini baada ya kudaiwa kuwa na vyeti vya kughushi. Kwa kweli tumeathirika na tunaiomba Serikali kutuma haraka wataalam wengine, vinginevyo hali itakuwa mbaya,” anasema Moro.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, aghalabu, maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika hukumbwa na magonjwa ya mlipuko, huku kukiwa na kesi nyingi za magonjwa ya malaria na homa za matumbo ambayo huhitaji uangalizi na ushauri wa kitabibu, mambo yanayokosekana kwa sasa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *