NYUMBA ya Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi Mtapemba kwenye Halmashauri ya Nsimbo, takriban kilometa 15 tu kutoka wilayani Mpanda, haina choo.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, ili kupata huduma, mwalimu mkuu huyo na familia yake wanalazimika kuomba msaada kwa majirani, jambo ambalo limeelezwa kwamba ni aibu na fedheha kubwa.
Aidha, mbali ya nyumba hiyo pekee shuleni hapo kukosa choo, miundombinu mingine ni mibovu ambapo walimu wengine 15 wanaofundisha shuleni hapo hawana nyumba za kuishi na badala yake wamepanga mitaani huku nyingi kati ya nyumba hizo zikikosa hadhi ya kuishi mfanyakazi wa serikali na hivyo wengine kuishi kijiji jirani, wakilazimika kusafiri mwendo mrefu kufika kazini.
FikraPevu imeelezwa kwamba, shule hiyo ilianzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita wakati Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa Operesheni Vijiji.
“Hii nyumba anayoishi Mwalimu Mkuu ni majanga tu. Haina choo! Kwa hiyo mwalimu analazimika kuomba msaada kwa majirani kujisitiri. Ni aibu kwa kweli,” anasema mmoja wa walimu wa shule hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Majimoto wakielekea kuchota maji katika chemchemi ya ‘Majimoto’.
Hata hivyo, zipo nyumba (mapagala) zilizokuwa zimejengwa kwa ajili ya walimu jirani na shule hiyo ambazo ni chakavu kiasi cha kuonekana kuhatarisha maisha kwa yeyote atakayejaribu kuzitumia, zikiwa zimejengwa kwa udongo.
Mwalimu mmoja aliyejitosa kuishi katika moja ya nyumba hizo aliiambia FikraPevu kwamba, nyakati za masika huwa hakuna kulala kwani nyumba hiyo inavuja.
“Ni sawa na kukaa chini ya mwembe. Hapo utafurahia kivuli tu lakini mvua ikija, hapafai,” anasema mwalimu huyo.
Diwani wa Mtapemba, Eliezer Fyula, anakiri kulifahamu tatizo la uhaba wa nyumba shuleni hapo, akidai kuwa lipo kwa muda mrefu sasa.
“Hapa tuna bahati kwa kuwa tuna walimu 16, lakini ni bahati mbaya kwamba nyumba zilizoandaliwa kwa ajili yao ni tano tu, nazo ni chakavu kama unavyoziona.
“Ni moja tu ndiyo imejengwa kwa matofali ya kuchoma, nyingine ni matofali ya udongo tu. Wenyewe wanaita biskuti. Zipo katika hali mbaya sana,” Diwani Fyula aliieleza FikraPevu.
Anasema tatizo hilo linachagizwa na Halmashauri ya Nsimbo kutotenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu licha ya yeye kuishauri mara kwa mara.
Kwa upande mwingine, katika Kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, changamoto ya uhaba wa maji ni kubwa na husababisha hata wanafunzi kushindwa kuendelea na ratiba ya masomo kama ilivyopangwa, badala yake huenda kutafuta maji kwenye mabwawa na chemchemi.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Majimoto wakichota maji kwenye chemchemi ya ‘Majimoto’.
Katika Shule ya Msingi Majimoto, FikraPevu iliwashuhudia watoto wakitoka madarasani kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi, hasa ya chooni, kwani shule haina kisima wala bomba la maji.
Wakizungumza na FikraPevu, wanafunzi hao waliokuwa wakichota maji katika chemchemi maarufu inayotoa maji ya moto, walilalamikia hali hiyo kwamba inawaathiri kitaaluma.
“Shuleni hakuna huduma yoyote ya maji na kama kusingekuwepo chemchemi hapa karibu, sijui tungepata wapoi maji. Kila mara huwa tunakatisha masomo kuja kuchota maji,” anasema mtoto mmoja wa darasa la tatu.
FikraPevu imeelezwa kwamba, ni kawaida kwa kila mwanafunzi anayesoma shuleni hapo kuwa na guduria la lita tano kwa ajili ya kuchotea maji kwenye chemchemi hiyo.
FikraPevu inafahamu kwamba, jina la kijiji cha Majimoto, linatokana na kuwepo kwa chemchem hiyo inayotoa maji ya moto kiasi cha kulazimika kuyapoozesha kabla ya kuyatumia. Maji hayo hutiririka kwa mwaka mzima.
Hata hivyo, maji hayo yanayotokana na nguvu za asili (volcano), hayafai kwa kunywa.
Pamoja na kufahamu kwamba maji ya chemchemi hiyo hayafai kwa kunywa, FikraPevu iliwashuhudia watoto kadhaa wakiyanywa baada ya kupoa, wakisema hawana sehemu nyingine ya kupata maji ya kunywa.
“Tumeshazowea kwa sababu imekuwa kawaida kabisa kuja kuchota maji hapa. Tutafanyaje na chooni hakuna maji? Ni lazima kila siku kuja hapa kuchota maji,” mwanafunzi mmojawapo.
Kwa ujumla maji ni tatizo kubwa kijijini hapo na wananchi husafiri kwa takriban kilometa sita kufuata maji katika Kijiji cha Mamba.