Sababu 6 zinazothibitisha kwanini kukosolewa ni jambo zuri

Jamii Africa
People pointing at businessman, close-up (blue tone, grainy)

Mark Thomas anasema, kukosolewa kunaweza kuwa kitu kizuri bila kujali imetoka kwa mtu wa aina gani au anayefanya kazi gani.

Kukubali kukosolewa yaweza kuwa jambo gumu sana. Katika nafasi fulani katika ulimwengu huu unaotegemea mawazo na maoni, utakutana na mtu yeyote (anaweza kuwa mteja, hadhira au hata msomaji tuu) ambaye atataka kukwambia namna ya kufanya mambo yako kwa namna nzuri zaidi.

Yaweza kuwa vigumu kukabiliana na hali hiyo; ukizingatia kwamba hakuna mtu anayependa kuambiwa anakosea.

Sio wakati wote kukosolewa ni kubaya kwasababu wakati mwingine unaweza kutumia kukosolewa huko katika kujiboresha kitaaluma. Fahamu sababu sita zinazothibitisha kuwa kukosolewa ni jambo zuri:

Kukosolewa ni namna ya mawasiliano

Inapotokea mtu anakukosoa inamaanisha kwamba anataka kukupa mrejesho kuhusu huduma unayotoa na hii inaweza kuwa nafasi nzuri ya kujifunza kuhusu watu unaofanya nao kazi na jinsi ya kuwafanya wawe wateja wanaorizika na kazi yako.

Chukua muda kufikiria kile wanachokisema watu kabla hujajibu chochote, maana kwenye biashara au kufanya kazi na mtu ambaye yupo tayari kukosolewa na kufanyia kazi kile anachoambiwa humaanisha pande zote mbili zinaweza kufanya kazi kwa pamoja kufikia mafanikio mazuri. Uzalishaji unamaanisha kujua kile ambacho wateja wako wanataka.

 

Mrejesho hukusaidia kuboresha huduma zako

Unapodhani kwamba unachokifanya kipo sawa lakini hupati mrejesho wowote kutoka kwa watu, unakuwa na uhakika kiasi gani kama unachokifanya kina uzuri wowote? Haijalishi unajishughulisha na nini, kusikiliza na kufanyia kazi mrejesho unaoupata kutoka kwa wateja wako kutakusaidia kujua kipi ni kizuri na kipi kiboreshwe zaidi.

Tumia taarifa unazozipata kuboresha kile unachokifanya, inaweza kuwa vigumu kusikiliza kauli hizo zinazoumiza lakini itafanya unachokizalisha kiwe imara katika uzalishaji wake.

 

Hukufanya ufikirie kuhusu utendaji kazi wako

Kukosolewa kunakojenga huweza kukufanya uachane na utendaji mbovu na kuhamia kwenye mzuri. Jaribu kuwa na malengo na chukulia kile unachokizalisha kama vile sio cha kwako.

Hii inaweza kuwa ngumu hasa pale ambapo unahusika kwa kiwango kikubwa kwenye kile unachokifanya, lakini ukijaribu kufikiria zaidi unaweza kugundua namna ambavyo utaweza kuboresha namna ya utendaji kazi wako na kuzuia kushindwa kwa namna yoyote ile wakati wa kazi.

Jaribu kuangalia kama kuna taarifa yoyote ya ziada unayoihitaji? Je, kuna kitu umekisahau wakati ulipouanza huo mradi? Je, kazi inaweza kumalizika kwa muda uliopangwa awali?.

 

Kukosolewa kunakofaa kunaweza kukuletea manufaa

Fikiria pale inapotokea ukapata mteja ambaye yupo tayari kukwambia namna ya kumuhudumia vizuri; na wewe tuu ndio ukawa na taarifa hizi.

Hii hukuweka katika nafasi nzuri kwenye soko kuliko mtu mwingine yeyote na huweza kutumika siku za usoni ili kuboresha vitu na kuvipata kwa haraka. Jitahidi kutafuta taarifa hizi kutoka kwa wateja wako na kuwafanya wawe wazi kwako kuhusu kile wanachokitaka.

 

Tumia lugha nzuri, kusababisha suluhu

Lugha unayoitumia kujibu pale unapokosolewa ni ya muhimu sana. Jitahidi kuepusha ugomvi katika kujibu kwako. Badala yake badilisha kujibu kwako kuwa katika mazungumzo kuhusu namna ya kulikabili tatizo.

Hii itakufanya ubaki kwenye nafasi nzuri katika kazi yako na hautapoteza muda mwingi kuwaza kuhusu nini kifanyike ili kurekebisha mambo.

Yaweke maneno yako katika vitendo ili kuonesha kwamba unakubali kukosolewa, toa mrejesho wako kwa namna nzuri na fanikisha kukamilisha kazi yako.

 

Usichukulie kukosolewa kama shambulio binafsi

Inapotokea mtu hajaipenda kazi yako kwa mara ya kwanza usichukulie kwamba mtu huyo anakuchukia.

Hata pale unapokosolewa kwa kuonewa usiwe mwepesi kujibu kwa haraka na kwa hasira maana unaweza kuharibu uhusiano wako wa kazi na mtu huyo na inaweza kukuharibia sifa nzuri uliyonayo kwenye soko.

Kuna wakati kukosolewa kunaweza kuonekana kama shambulio binafsi, na wakati mwingine utakuwa sahihi kuwaza hivi. Tambua kwamba watu hukosea hivyo ni muhimu kukumbuka kutoruhusu maoni ya watu kukukasirisha.

Hata hivyo mtu makini anaweza kupokea kukosolewa kwa aina yoyote ile na akatoa mrejesho mzuri hata kama kukosolewa kwake kumekuwa ni shambulio binafsi kwake.

Watu wa aina hii wanaweza kutumia nafasi hiyo kwa manufaa yao, na kama itashindikana kabisa vunja mkataba wa kufanya kazi na mtu huyo kwa namna nzuri na kuacha sifa yako katika soko ikiwa bado ni nzuri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *