Ndani ya Manispaa ya Dodoma, mwalimu mmoja wa shule ya msingi anafundisha wanafunzi 151

Jamii Africa

KUSITISHWA kwa ajira za watumishi wa umma wakiwemo walimu kumeipa mzigo mzito Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambapo mwalimu mmoja anafundisha watoto 151, FikraPevu inaripoti.

Uchunguzi uliofanywa kwa takriban wiki mbili umeonyesha kwamba, uwiano huo upo katika Shule ya Msingi Mbabala iliyoko Kata ya Mbabala katika manispaa hiyo ambayo ina wanafunzi 753 na walimu watano tu.

Katika mwaka wa fedha 2015/16 Serikali ilikuwa imepanga kuajiri walimu 35,411 kwa shule za msingi na sekondari, lakini ajira zote zilisitishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, hali ambayo imeongeza ugumu kwa watendaji hao kutekeleza majukumu yao.

Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inabainisha uwiano sahihi wa mwalimu kwa wanafunzi (PTR) katika shule za msingi kuwa ni mwalimu mmoja kwa watoto 40 (1:40).

Hadi Desemba 2016, takwimu za Tamisemi zinaonyesha bado kulikuwa na uhaba wa walimu 47,151 wa shule za msingi, idadi inayozidi kidogo jumla ya walioajiriwa katika shule za msingi za umma na binafsi kwa miaka 10 iliyopita ambao ni 45,528.

Ingawa Manispaa ya Dodoma inaonyesha kuwa na uwiano wa jumla wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 ukiwa unalingana na uwiano wa kitaifa wa 1:40, lakini hali halisi kwa kila shule ni tofauti ambapo shule nyingi zinaonekana kuwa na walimu wachache kulinganisha na idadi ya wanafunzi na mahitaji kwa ujumla.

FikraPevu imebaini kwamba, Manispaa hiyo ina jumla ya shule za msingi 95 na walimu 1,817 tu wakati wanafunzi wapo 72,330.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, shule 67 katika manispaa hiyo zina uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi zaidi ya 50 ukiwa ni zaidi ya uwiano unaotakiwa.

Ukiacha Shule ya Msingi Dodoma Viziwi katika Kata ya Dodoma Makulu yenye wanafunzi 88 na walimu 14 (uwiano wa 1:6), shule pekee ya kawaida ambayo ina walimu wanaotosheleza ni Uhuru yenye wanafunzi 351 na walimu 24 ikiwa na uwiano wa 1:15 ikifuatiwa na Kaloleni katika Kata hiyo na Jenerali Msuguri katika Kata ya Ihumwa ambazo zina uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 16.

Shule ya Kaloleni ina wanafunzi 473 na walimu 30 wakati Jenerali Msuguri ina wanafunzi 684 na walimu 44.

Mbali ya Mbabala, shule nyingine zilizoelemewa na wanafunzi kutokana na uhaba wa walimu ni Nguji iliyoko Kata ya Nghonghona ambayo ina walimu wanne tu na wanafunzi 548, ukiwa ni uwiano wa 1:137 ikifuatiwa na Michese katika Kata ya Mkonze yenye walimu saba na wanafunzi 870 ukiwa ni uwiano wa 1:124.

Aidha, shule nyingine na uwiano wake kwenye mabano ni Chihanga yenye walimu wanne na wanafunzi 490 (1:123), Mlangwa yenye wanafunzi 1,071 na walimu tisa (1:119), Gawaye yenye wanafunzi 587 na walimu watano (1:117), Zepisa ina wanafunzi 692 na walimu sita (1:115), Nghambala ina wanafunzi 559 na walimu watano (1:112), Nkulabi yenye wanafunzi 784 na walimu saba (1:112), Mapinduzi yenye walimu wanne na wanafunzi 425 (1:106), sawa na Chololo yenye wanafunzi 742 na walimu saba.

Nyingine ni Kikombo yenye wanafunzi 1,095 na walimu 11 (1:100), Chahwa ina walimu wanne na wanafunzi 401 (1:100), Chigongwe yenye wanafunzi 685 na walimu saba (1:98), Nzasa ina wanafunzi 782 na walimu nane (1:98), Mbalawala yenye walimu saba na wanafunzi 672 (1:96) sawa na Iyumbu, Ipala ina walimu 10 na wanafunzi 902 (1:90), Msisi ina walimu watano na wanafunzi 439 (1:88) sawa na Mkoyo yenye wanafunzi 617 na walimu saba huku Hombolo Makulu ikiwa na wanafunzi 772 na walimu tisa hivyo kuwa na uwiano wa 1:86.

FikraPevu imebaini kwamba, tatizo la uhaba wa walimu limeukumba mkoa wote wa Dodoma japokuwa uwiano wa jumla unaonyesha kwamba mwalimu mmoja anafundisha watoto 46.

Mkoa huo una jumla ya shule 729 za msingi zenye wanafunzi 382,412 huku walimu wakiwa 8,324 tu, lakini shule 476 kati ya hizo mwalimu mmoja anafundisha watoto 50 na kuendelea.

 

Wilaya ya Kondoa

Uwiano wa walimu kwa wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa siyo mzuri ambapo wastani wa jumla ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 52.

Halmashauri hiyo yenye jumla ya shule 92 za msingi ina walimu 818 na wanafunzi 42,273 ambapo shule 68 kati ya hizo zina uwiano wa zaidi ya wanafunzi 50 kwa mwalimu mmoja.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, Shule ya Msingi Makafa katika Kata ya Salanka ndiyo pekee yenye uwiano mzuri zaidi wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20. Shule hiyo ina wanafunzi 160 na walimu nane.

Walimu katika Shule ya Mwisanga katika Kata ya Haubi ndio walioelemewa zaidi na wanafunzi ambapo mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 115. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 576 na walimu watano.

Shule nyingine zenye walimu wachache na uwiano ukiwa kwenye mabano ni Idindiri iliyo na wanafunzi 702 na walimu saba (1:100), Makirinya yenye wanafunzi 832 na walimu tisa (1:92), Ihari ina walimu 7 na wanafunzi 586 (1:84), Keikei ina wanafunzi 826 na walimu 10 (1:83), Mnenia ina walimu 8 na wanafunzi 654 (1:82) uwiano sawa na Kwadelo yenye wanafunzi 1,071 na walimu 13.

Nyingine ni Loo yenye walimu saba na wanafunzi 565 (1:81), Chungai ina wanafunzi 712 na walimu tisa (1:79), Dorasi ina walimu nane na wanafunzi 623 (1:78), Kwadelo B ina wanafunzi 228 na walimu watatu tu (1:76), Kinyasi ina wanafunzi 746 na walimu 10, Atta ina wanafunzi 527 na walimu saba na Bambare ina wanafnzi 597 na walimu nane ambapo zote tatu uwiano wake ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 75.

 

Halmashauri ya Mji Kondoa

Halmashauri ya Mji wa Kondoa ndiyo pekee katika Mkoa wa Dodoma ambayo walau ina uwiano mzuri, ambapo mwalimu mmoja kwa wastani anafundisha wanafunzi 28.

FikraPevu imebaini kwamba, halmashauri hiyo yenye jumla ya shule 26 na wanafunzi 11,191 ina walimu 397, huku Shule ya Msingi Kilimani yenye wanafunzi 331 na walimu 30 ikiwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 11.

Ni shule saba tu ambazo uwiano wa walimu kwa wanafunzi umevuka kiwango kinachotakiwa cha 1:40 huku Shule ya Mongoroma katika Kata ya Serya ikielemewa zaidi kwa kuwa na uwiano wa 1:79. Shule hiyo ina wanafunzi 714 na walimu tisa.

Shule nyingine zenye uwiano usiokidhi kiwango halisi ni Munguri yenye wanafunzi 325 na walimu watano (1:65), Mulua ina walimu nane na wanafunzi 453 (1:57) sawa na Iyoli yenye wanafunzi 510 na walimu tisa, Hachwi ina wanafunzi 307 na walimu sita (1:51), na Tampori ina walimu nane na wanafunzi 376 ikiwa na uwiano wa 1:47.

 

Wilaya ya Mpwapwa

Wilaya ya Mpwapwa ndiyo iliyoelemewa zaidi kutokana na kuwa na walimu wachache ikilinganishwa na wastani wa uwiano uliopo katika halmashauri nyingine.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, kati ya shule 116 zilizopo wilayani humo, 86 zina uwiano wa zaidi ya wanafunzi 40 kwa mwalimu mmoja, huku wastani wa uwiano kwa wilaya nzima ukiwa 1:50.

Wilaya hiyo ina walimu 1,243 na wanafunzi 61,371.

Shule ya Msingi Berege katika Kata ya Berege ndiyo iliyoelemewa zaidi, ambapo ina wanafunzi 950 na walimu sita pekee, ukiwa ni uwiano wa 1:158, ikifuatiwa na Lufu katika Kata ya Lufu ambayo ina wanafunzi 668 na walimu watano, huku uwiano ukiwa 1:134.

Shule hizo zinafuatiwa na Kinusi katika Kata ya Ipera yenye wanafunzi 655 na walimu sita (1:109), Mang’aliza ina walimu nane na wanafunzi 856 (1:107), Mlunduzi ina wanafunzi 499 na walimu watano (1:100), Wotta ina walimu sita na wanafunzi 575 (1:96), Mbori ina walimu saba na wanafunzi 637 (1:91).

Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kuwa, shule nyingine zilizo na uwiano usiokidhi wa walimu na wanafunzi ni Mima (1:90), Kimagai (1:89), Mlunga na Makose (1:86), Wangi (1:87), Msagali (1:82), Winza (1:82), Mtamba (1:81), Chinyika (1:80), Mlimo (1:80), Idodoma (1:79), Tambi (1:78), Godegode (1:77), Sazima (1:76), Kidabaga (1:76), Igoji Kusini, Galigali, na Chinyanghuku (1:75), Chilendu, Makulu, Iyenge, Kidenge, Iguluwi na Chitembo (1:74), Kimagai, Iwondo, Iramba na Chamanda (1:72), Igoji Kaskazini na Ipera (1:71), na Munguwi wastani wa 1:70.

Shule ya Msingi Igovu katika Kata ya Mpwapwa Mjini ndiyo pekee yenye uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 13, ambapo ina jumla ya walimu 33 na wanafunzi 441.

Shule hiyo inafuatiwa na Kiegea katika Kata ya Nghambi yenye uwiano wa 1:14 ambapo ina walimu 13 na wanafunzi 181, pamoja na Idilo katika Kata ya Mazae na Mazae yenyewe ambazo zina uwiano wa 1:17. Idilo ina wanafunzi 254 na walimu 15 wakati Mazae ina walimu 34 na wanafunzi 575.

 

Wilaya ya Kongwa

Uchunguzi unaonyesha kwamba, wastani wa jumla wa uwiano wa walimu kwa wanafunzi wilayani Kongwa siyo mbaya sana ambapo mwalimu mmoja anafundisha wastani wa wanafunzi 46.

Wilaya hiyo yenye jumla ya shule 106 ina walimu 1,335 na wanafunzi 61,181.

Mseta Bondeni katika Kata ya Chamkoroma ndiyo shule inayoongoza kwa uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 12, ambapo ina jumla ya walimu 12 na wanafunzi 148 tu.

Shule ya Msingi Ngomai yenye wanafunzi 1,273 na walimu 17 ndiyo inaonekana kuelemewa ambapo mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 75.

Shule hiyo inafuatiwa na Chang’ombe katika Kata ya Iduo ambayo ina walimu 11 na wanafunzi 811 na uwiano wa 1:74, Hogoro ina walimu 13 na wanafunzi 930 na uwiano wa 1:73 na Banyibanyi katika Kata ya Hogoro ina wanafunzi 775 na walimu 11 na uwiano wa 1:70.

 

Wilaya ya Chemba

Shule 63 kati ya 103 wilayani Chemba zinaonekana kuelemewa na wanafunzi ambapo wastani wa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi wilayani humo ni 1:51.

Takwimu ambazo FikraPevu imezipata zinaonyesha kwamba, wilaya hiyo ina jumla ya walimu 903 na wanafunzi 45,514.

Shule ya Msingi Kinkima katika Kata ya Churuku yenye wanafunzi 834 na walimu saba ndiyo imezidiwa ambapo uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ni 1:119 ikifuatiwa na Mlongia katika Kata ya Jangalo, ambayo ina wanafunzi 1,102 na walimu 10 hivyo kuwa na uwiano wa 1:110.

Shule hizo zinafuatiwa na Igunga katika Kata ya Goima ambayo ina walimu saba na wanafunzi 719 (1:103), Mrijo Chini yenye wanafunzi 1,434 na walimu 15 (1:96), Chemka ina walimu tisa na wanafunzi 823 (1:91), Hamai ina walimu tisa na wanafunzi 800 (1:89), Mtakuja ina walimu saba na wanafunzi 600 (1:86), Tandala yenye wanafunzi 1,107 na walimu 13 (1:85) uwiano sawa na Itolwa ambayo ina wanafunzi 1,099 na walimu 13.

 

Wilaya ya Chamwino

Wastani wa uwiano wa walimu kwa wanafunzi wilayani Chamwino ni 1:50, hali inayoonyesha kwamba kuna upungufu mkubwa pia wa watendaji hao katika sekta ya elimu.

Wilayani hiyo ina shule 119 za msingi na walimu 1,147, wakati idadi ya wanafunzi ni 56,776 huku shule 77 kati ya hizo zikiwa zimeelemewa na tatizo la uhaba wa walimu.

Shule ya Msingi Kambarage ndiyo pekee yenye uwiano mzuri wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20, ambapo ina jumla ya wanafunzi 479 na walimu 24.

Takwimu zinaonyesha kwamba, mwalimu mmoja katika Shule ya Msingi Huzi yenye wanafunzi 586 na walimu sita tu anafundisha watoto 98.

Shule hiyo inafuatiwa na Itiso ambayo ina walimu 10 na wanafunzi 958 hivyo kuwa na uwiano wa 1:96, wakati Shule ya Msingi Manda yenye wanafunzi 847 na walimu tisa ina uwiano wa 1:94.

Shule nyingi na uwiano wake kwenye mabano ni Mahama yenye wanafunzi 558 na walimu sita (1:93), Chita ina walimu sita na wanafunzi 559 (1:93), Gwandi ina wanafunzi 783 na walimu tisa (1:87), Nagulo Mwitikira ina waimu saba na wanafunzi 588 (1:84), Ikombo yenye walimu watano na wanafunzi 415 (1:83), Nghahelezi ina walimu 12 na wanafunzi 996 (1:83), na Umoja katika Kata ya Segala yenye wanafunzi 328 na walimu wanne (1:82).

Nyingine ni Msamalo yenye wanafunzi 564 na walimu saba (1:81), Makang’wa ina walimu 11 na wanafunzi 892 (1:81), Chinoje ina wanafunzi 390 na walimu watano (1:78), Izava ina walimu 10 na wanafunzi 754 (1:75), Igandu ina walimu 12 na wanafunzi 883 (1:74), Ikombolinga yenye wanafunzi 517 na walimu saba (1:74), Igamba ina walimu sita na wanafunzi 426 (1:71), Kawawa ina walimu saba na wanafunzi 491 (1:70), na Ndebwe ambayo ina walimu 10 na wanafunzi 703 na uwiano wa 1:70.

 

Wilaya ya Bahi

Katika Wilaya ya Bahi yenye shule za msingi 72, walimu 664 na wanafunzi 31,776, wastani wa uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 148.

Hata hivyo, wastani huo haujaondoa pengo la uhaba wa walimu, kwani shule 33 kati ya hizo zina uwiano wa zaidi ya wanafunzi 45 kwa kila mwalimu ukiacha Kigwe Viziwi yenye wanafunzi 101 na walimu 28 na uwiano wa 1:4.

Shule ya Mpinga yenye wanafunzi 1,013 na walimu 10 ina uwiano wa 1:101 wakati Nagulo Bahi ina uwiano wa 1:99 ambapo wanafunzi ni 594 na walimu sita.

Shule hizo zinafuatiwa na Mnkola yenye wanafunzi 502 na walimu sita (1:84), Mapinduzi ina walimu nane na wanafunzi 656 (1:82), Nguji ina wanafunzi 376 na walimu watano (1:76), Chimendeli ina wanafunzi 448 na walimu sita (1:75), Magaga ina walimu sita na wanafunzi 437 (1:73), Kusila ina walimu saba na wanafunzi 495 (1:71), na Bankolo yenye walimu sita na wanafunzi 422 ambayo uwiano wake ni 1:70.

Kwa ujumla, Mkoa wa Dodoma bado una upungufu mkubwa wa walimu na wachambuzi wa masuala ya elimu wanasema jitihada za makusudi zinahitajika ili kupunguza pengo hilo na kuongeza ufanisi.

<Mwisho/FP>

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *