MVUA kubwa iliyonyesha jana mjini Musoma mkoani Mara, imesababisha maafa makubwa, ambapo karibu kaya 200 hazina makazi yake, huku miundombinu ya barabara katika Manispaa hiyo ikiharibiwa vibaya; JF imethibitishiwa.
Kutokana na hali hiyo, misaada mikubwa ya kibinadamu inahitajika kwa waathirika hao wa mvua, na kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, inatakiwa kuharakisha kupeleka msaada wa chakula pamoja na vitu vingine kwa wananchi hao ambao hadi sasa hawana pa kuishi.
Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kisurura alisema leo kwa njia ya simu kutoka Musoma kwamba, kila kata ya Manispaa hiyo imekubwa na maafa hayo, na kwamba baadhi ya madaraja, barabara zimeharibika vibaya sana, huku kaya hizo zikianguka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia saa 9 usiku hadi saa 4 asubuhi, na kuanza kunyesha tena majira ya mchana na kukatika jioni jana.
Kwa mujibu wa Meya huyo wa Musoma, hadi sasa uongozi wa Manispaa hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge wa Musoma mjini pamoja na Serikali ya Wilaya ya Musoma unafanya tathmini ili kubaini hasara iliyojitokeza, kaya na watu wangapi wanahitaji msaada wa haraka, ili kunusuru maisha yao yasiangamie.
“Kwa harakaharaka kaya 150 hazina makazi yake hapa Musoma. Na hii inatokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi. Tunaiomba Serikali ifanye haraka sana kuleta msaada kwa wananchi wetu hawa, maana hali ni mbaya sana.
“Kwa sasa tunafanya tahmini kubaini hasara yote kwa ujumla!. Ofisi yangu, ofisi ya mbunge wetu wa Musoma mjini na Serikali ya Wilaya ya Musoma tunahangaikia mambo haya kwa sasa, maana hata barabara zimechimbika vibaya sana. Yaani ni hasara tupu, baadhi ya madaraja yamesombwa na maji”, alisema Meya Kisurura.
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), alimwambia mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana jioni akiwa mjini Dodoma kwamba: “Serikali inatakiwa iwahishe misaada kwa wananchi wa Musoma, maana kaya nyingi hazina pa kuishi, na hata mimi (Nyerere), nitakuwa Musoma Jumatatu (kesho)”.
Aidha, Nyerere alitoa pole kwa wananchi wote wa jimbo lake hilo la Musoma mjini, huku akiwaombea kwa mwenyezi Mungu awaepushe na mambo mengine yasiyo mazuri kama hayo, na kwamba, mashirika, taasisi na makampuni hayana budi kuguswa na athari hiyo kwa kutoa misaada ya aina mbali mbali ili kuwasaidia wananchi hao.
Hata hivyo, mbunge huyo aliwaomba wananchi wa Musoma kuchukuwa tahadhari pale mvua inapoonekana kuanza kunyesha, na kwamba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, inapaswa kuhakikisha wananchi wote walioathirika na janga hilo la mvua wanapata misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vyakula vya kutosha na si vinginevyo.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa mvua kubwa na kusababisha athari kubwa namna hiyo katika Manispaa ya Musoma, ambapo miezi takriban sita au saba hivi mvua kubwa ilinyesha Musoma kisha kusababisha kaya nyingi kukosa makazi yake, huku miundombinu ya barabara ikiharibika zaidi.
Mwisho.
Na. Sitta Tumma