Kenyatta asisitiza kuendeleza ushirikiano EAC

Islam Mbaraka

Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesisitiza kuendeleza ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwani amesema ni moja ya nguzo muhimu katika kipindi cha utawala wake.

''Lengo letu kuu katika kuimarisha biashara na uwekezaji utakuwa ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,'' Rais Kenyatta alinukuliwa akisema alipokutana na Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera aliyekwenda kumtembelea ofisini kwake mjini Nairobi Juzi.

Aliongeza kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya biashara kupewe kipaumbele kadiri mtangamano wa EAC unavyozidi kuimarika na kupanuka, Shirikia Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.

''Kuondolewa kwa vikwazo vya kazi na kusafiri kwa raia ndani ya nchi wanachama kutasaidia zaidi kukua kwa biashara na kubadilishana mawazo,'' alisema Rais Kenyatta.

''Tunaweza kufanya vizuri zaidi tukiwa katika kanda kuliko nchi mojamoja,'' aliongeza Rais.

Naye Katibu Mkuu wa EAC, Dk Sezibera alimpongza Rais kwa kushinda uchaguzi wa rais hivi karibuni na kuwashukuru pia wananchi wa Kenya kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi walivyoendesha uchaguzi huo.

Dk Sezibera pia alimpatia Rais huyo maelezo mafupi kuhusu kikao maalum kijacho cha wakuu wa nchi za EAC kitakachofanyika, Arusha, Tanzania, Aprili 28, mwaka huu, ambacho kitakuwa cha kwanza kwake kushiriki kama Rais wa Kenya.

LC/NI – EANA

1 Comment
  • Unajuavingozi wetu ni watu wa ajabu hawa fikirii vitu vingine kwanza jiulize Tangia wa anze jumuia hiyo umesha sikia makubaliano yaliyo patikana kila siku wa na kaa  wana kula hela halafu kipi kina fanyika kama kweli wange kuwa wana kaa nakuamua maendeleo ya wana nchi wange sha pitisha hakuna kiongozi mzalendo nchi zetu siasa ime tawala kenya wana jitahidi ona shilingi yao ina vyo panda  nihayo nina mengi ya msingi

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *