Hatimaye upande wa Jamhuri katika kesi inayoikabili JamiiForums imekamilisha kutoa ushahidi wake na kuipa nafasi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamua kama kuna kesi ya kujibu au la.
Katika kesi hiyo namba 457, JamiiForums inashitakiwa na kampuni ya CUSNA Investment na Oceanic Link ambayo ilidaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi.
Uamuzi huo umefikiwa leo mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa ambaye anasikiliza kesi hiyo. Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Nassoro Katuga kufunga ushahidi na kuiachia Mahakama jukumu la kupitia ushahidi walioutoa ili kubaini kama upande wa washatakiwa wana kesi ya kujibu.
Ikumbukwe kuwa kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwaka 2016 na mpaka leo upande wa Jamhuri ulifanikiwa kuwaleta mahakamani mashahidi wa tano kutoka Jeshi la Polisi, Wakala wa Kusajili Biashara na Leseni na Kampuni ya CUSNA Investment na Oceanic Link kutoa ushahidi wao.
Shahidi wa kwanza alikuwa Inspekta Monica Pambe kutokana Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandao. Mwingine ni ASP Fadhiri Bakari ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu wa fedha kanda maalumu ya Dar es Salaa ambaye alitoa ushahidi wake Desemba 5, 2017.
Wengine ni Msajili Msaidizi Mkuu wa Makampuni, Rehema Kitambi kutoka BRELA ambaye alitoa ushahidi wake juu ya kusajiliwa kwa kampuni ya JamiiForums. Shahidi wa nne alikuwa Jonas Wilson Mcharo kutoka CUSNA Investment and Oceanic Link ambapo aliwasilisha kielelezo kinachodaiwa kuwa ni andiko lenye maudhui ya kuichafua kampuni yao linalodaiwa kuwekwa kwenye mtandao wa JamiiForums lakini mahakama ilikataa kupokea kielelezo hicho kwasababu hakikudhi matakwa ya kisheria.
Shahidi wa tano na wa mwisho alikuwa ni Loy Mhando, Naibu Msajili wa Alama na Huduma kutoka BRELA ambapo leo upande wa Jamhuri umeamua kufunga ushahidi wao ili kutoa nafasi kwa Mahakama kutoa uamuzi kama kuna kesi ya kujibu au la.
Baada ya Wakili Katuga kumaliza kutoa maelezo yake na kufunga ushahidi, Hakimu Mwambapa uliugeukia upande wa utetezi ambao ulikuwa ukiongozwa na Wakili Jeremiah Mtobesya ambaye aliiomba Mahakama iwapatie muda wa kupitia ushahidi ili kutoa utetezi wao kabla ya mahakama hiyo haijatoa uamuzi wa kesi.
Hakimu Mwambapa alikubali ombi hilo la upande wa utetezi ambapo aliwataka hadi Aprili 9 mwaka huo wawe wamewasilisha ombi lao la kujitetea dhidi ya ushahidi uliotolewa na Jamhuri. Kwa upande mwingine, Jamhuri wametakiwa hadi kwa Aprili 23, 2018 kujibu hoja za upande wa utetezi (counter-reply).
Hata hivyo, Hakimu Mwambapa amebainisha kuwa mahakama itatoa uamuzi kama kuna kesi ya kujibu au la siku ya 3 Mei, 2018 ambapo watakutana tena mahakamani hapo.
Kesi ilikotoka…
Katika kesi hii, Polisi walitaka JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada na mchangiaji mmoja ili waweze kuwakamata na kuwahoji wakidai kuwa kampuni ya CUSNA Investment na Oceanic Link ilichafuliwa.
JamiiForums inadaiwa ilikataa kutoa taarifa binafsi za wanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hicho cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama inayoridhia kukamatwa kwa wahusika na kuelezwa kosa lililofanywa na wahusika.
Kutokana na msimamo huo wa JamiiForums, Maxence Melo alikamatwa Disemba 13, 2016 na kufikishwa mahakamani Disemba 16, 2016 akishtakiwa kwa makosa 3 ikiwemo kuendesha mtandao wa JamiiForums bila kutumia kikoa cha .TZ ambacho kina usajili wa Tanzania.
Shtaka lingine ni lile lilofunguliwa na kampuni ya Oilcom ambayo inadai ilichafuliwa na JamiiForums kutokana taarifa iliyowekwa kwenye mtandao huo kuwa kampuni hiyo inakwepa kodi na kuchakuchua mafuta bandarini.
Kufuatilia mlolongo wa yale ambayo yamekuwa yakijiri katika kesi hizo 3 fuatilia hapa; Kinachojiri Mahakama ya Kisutu kesi ya Jamhuri dhidi ya JamiiForums