Watatu wauawa baada ya kubakwa Jijini Mwanza

Jamii Africa

WANAWAKE watatu wameuawa kinyama, baada ya kubakwa na watu wasiojulikana katika kata ya Mahina, wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.

Vyanzo vya habari vimeiambia FikraPevu kwamba mauji hayo yalitokea kwa nyakati tofauti, kati ya Januari na Februali 22 mwaka huu.

Ilidaiwa kwamba wanawake hao huuawa nyakati za asubuhi; hali ambayo imeanza kusababisha hofu miongoni mwa wanawake wa mtaa wa Mahina.

Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Deus, zimewataja waliouawa kwamba ni Salome Kagusa, Vaines John pamoja na Kulwa Paul.

Inadaiwa mauaji hayo yamekuwa yakifanyika nyakati za asubuhi kati ya Januari na Februali 22 mwaka huu.

“Wa kwanza kuuawa ndani ya mwaka huu ni Salome; ambapo mwili wa Kulwa ulipatikana jana, Februari 29

Mwenyekiti huyo alisema mwili wa Kulwa uligundulika jana ukiwa umeharibika vibaya; zikiwa zimepita siku tatu baada ya kuokotwa kwa mwili wa Vaines.

Alisema mwili huo ulikuwa umetelekezwa jirani ya shule ya Alliance Accademy; shule binafsi katika mtaa wa Mahina.

Alisema mlinzi wa shule hiyo, Pius Mwita ametiwa mbaroni kutokana na tukio hilo.

Deus alisema mwili wa Vaines alikutwa na kifo wakati akitoka kisimani kuchota maji na kwamba mwili wake uliokotwa shambani huku kukiwa na mazingira ya ubakwaji.

Alifafanua pia kwamba Salome aliuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana, baada ya kubakwa.

Kwa mujibu wa Deus, mwili wa Kulwa uligunduliwa na mmewe jana zikiwa zimepita siku saba tangu mwanamke huyo alipoaga nyumbani kwake kwamba anaelekea kazini katika kata ya Nyakato.

Alisema mwanamke huyo hakurejea nyumbani na kwamba mmewe aliyetajwa kwa jina la Mpejiwa Faya alitoa taarifa katika ofisi ya serikali ya mtaa pamoja na kituo kidogo cha Poliai cha Nyakato.

Alisema kabla ya kuuona mwili, Faya  aliokota ndoo pamoja na ndala za mkewe katika eneo la nyumba alikokuwa akifanya kazi ya kutwa (kibarua).

“Ndipo Faya alipotoa taarifa katika uongozi wa mtaa na polisi Nyakato; baada ya kufika hapa tukafuatilia na kukuta mwili ukiwa umetelekezwa kwenye shimo la kupitishia maji machafu. Kusema kweli Kulwa alikuwa amevuliwa nguo zote, na kubaki kama alivyozaliwa”  alisisitiza mwenyekiti huyo.

Alisema maziko ya mwanamke huyo yalifanyika juzi baada ya Polisi kufika  katika eneo la tukio.

“Mwanamke mwingine, Esther  aliwahi kunyongwa na kuponea chupuchupu baada ya wauaji kuondoka katika eneo la tukio wakidhani kuwa tayari mwanamke huyo alikuwa amekata roho. Kwa bahati nzuri mwanamke huyo aliokotwa na wasamaria wema” alisema mwenyekiti huyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, amethibitisha juu ya kuwepo matukio haya na amesema ofisi yake inaendelea na uchunguzi kuhusiana na matukio hayo.

Habari hii ni kwa mujibu wa Juma Ng’oko wa FikraPevu – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *